Wednesday 26 February 2014

Miili 5 yapatikana mgodini A. Kusini

 

Wachimba migodi waliookolewa wiki jana wanakabiliwa na kesi mahakamani
Miili ya wachimba migodi haramu watano, imepatikana karibu na mgodi ambao ulikuwa hautumiki nchini Afrika Kusini.
Miili ya wanaume wanne na mwanamke mmoja ilipatikana karibu na mgodi huo katika eneo la Roodepoort, Magharibi mwa Johannesburg.
Vifo vyao vimetokea wiki moja baada ya shughuli kubwa ya uokozi wa zaidi ya wachimba migodi 20 haramu waliokuwa wamekwama ndani ya mgodi Mashariki mwa Johannesburg.
Walikamatwa baada ya kuokolewa na sasa wanakabiliwa na kosa la uchimbaji haramu wa migodi.
Afrika Kusini hupoteza mamilioni ya dola katika shughuli za uchimbaji haramu wa madini kila mwaka.
Ardhi inayozingira mji wa Johannesburg ina migodi mingi ambayo haitumiki na ambayo huvutia wachimba migodi haramu kutoka katika eneo hilo na nchi jirani za ,Lesotho, Msumbiji na Zimbabwe.
Mvuto wake hasa huwa ni kwamba zinaweza kuwa na madini ya dhahabu.
Wakati nyingi ya migodi hizo hazina faida za kifedha, bado zina mabaki ya dhahabu kiasi cha kuwavutia watu wengi wasio na ajira.
Waokozi wanasema kuwa bado huenda kuna wachimba migodi haramu zaidi ndani ya migodi hiyo.

 

Uganda yahofia kunyimwa misaada

Waziri wa mambo ya nje nchini Uganda, Sam Kutesa amesema ana wasiwasi kuwa Marekani huenda ikasitisha msaada wake kwa taifa hilo baada ya Rais Yoweri Museveni kuidhinisha sheria dhidi ya ushoga nchini humo.

 

Bwana Kutesa amesema kuwa watu sharti wawe na maadili na kukubali msaada.
Balozi wa Marekani nchini Uganda Scott DeLisi, awali aliitaka serikali ya Uganda, kubatilisha sheria hiyo.
Alisema alihitaji kufafanuliwa zaidi sheria hiyo, kabla ya Marekani kujua ikiwa itaendelea na mipango yake ya misaada kwa nchi hiyo hasa miradi ya kupambana dhidi ya HIV na Ukimwi..
Sheria hiyo mpya, inatoa adhabu kali kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na kupiga marufuku kile inachosema kusambaza vitendo vya ushoga.


Asasi za DRC zataka el Bashir ashikwe.

Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, DRC, yamesema kuwa Serikali ya nchi hiyo itachukuliwa kuwa dhaifu iwapo hamkamati Rais wa Sudan, Omar el Bashir.

 

Rais wa Sudan Omar el bashir

Mashirika yapatayo 90 yalitoa wito Serikali ya DRC imkamate el Bashir ambaye alikuwa mjini Kinshasa kushiriki katika vikao vya muungano wa COMESA.
Mmoja wa waandalizi wa maandamano ya kushinikiza Serikali imkamate kiongozi huyo wa Khartoum, Bwana Andre Kito Masimango, amesema:
"kuna barua ambayo inasema kuwa mahali po pote ambapo El Bashiri anapatikana anapaswa kukamatwa na kupelekwa kwenye mahakama ya kimataifa."
Mkerektwa huyo wa haki za kibinadamu anasema kuwa Rais El Bashir anapaswa kukamatwa kwa heshina ya waathirika wa dhuluma inayodaiwa kufanywa nchini Sudan na hata DRC yenyewe.
Watu kadhaa ambao wametoa maoni kwenye mtandao wa BBC wamesema kuwa lilikuwa kosa kwa Serikali ya DRC kumkaribisha Rais El Bashar kwa mkutano wa COMESA huku ikijua kuwa anatafutwa.
Hata hivyo kuna wale wanaosema kuwa msimamo wa Umoja wa Afrika (AU) ambao unasema kiongozi anayetawala hapaswi kukamatwa unapaswa kuzingatiwa ili El Bashir asikamatwe ugenini DRC.

 

Marekani yaonya Urusi kutoivamia Ukraine



 Marekani imeionya serikali ya Moscow isithubutu kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Ukraine.
Hatua hii inawadia siku moja tu baada ya Urusi kuamuru kufanyika kwa mazoezi ya kijeshi yanayoshirikisha askari wapiganaji laki moja na nusu kwenye mpaka wake na Ukraine .
Kujitokeza kwa wanajeshi wa Urusi kwenye mpaka na Ukraine kumeimarisha uhasama ulioko kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, John Kerry amesema kuwa Urusi inapaswa kukubali ushauri ya kwamba mataifa ya kigeni yasiingile mambo ya ndani ya Ukraine.
Alisema kuwa kujiingiza kijeshi katika hali ilivyo nchini Ukraine kwa hivi sasa ni kosa kubwa.
Mawaziri wa ulinzi kutoka mataifa ya muungano wa NATO wametoa taarifa ambapo wamesema kuwa wanachama wake wataendelea kuunga mkono uhuru na hadhi ya taifa la Ukraine.
Serikali ya Marekani imesema kuwa imetenga mbinu mbalimbali inazotazamia kutumia kuimarisha Ukraine kiuchumi, huku kukiendelea kuwa na hofu kuwa huenda taifa hilo likashindwa kuendelea kulipa madeni yake.
Kwa wakati huu msaada wa kijeshi pekee kwa Ukraine hautoshi kwani taifa linalotaka kusaidia lazima kwanza liimarishe hali ya kukubaliwa kwake katika taifa hili ambalo limegawanyika kwa imani yake kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi.
Wabunge kadhaa wa Marekani wameonya kuwa Jumuiya ya Ulaya na Marekani wasipotoa msaada wa pesa taslimu Urusi huenda ikafanya hivyo.