Monday 31 March 2014

Kweli Serikali itadhibiti ada kubwa vyuoni?

Kwa muda mrefu wananchi wa kada mbalimbali wamekuwa wakilalamika kuhusu karo kubwa zinatozwa shuleni na katika vyuo vya elimu ya juu.
Kuna shule hapa nchini ambazo ada yake kwa mwaka inazidi kiwango kinachotozwa katika baadhi ya vyuo vikuu.
Hata hivyo, tatizo linatajwa kuwa kubwa zaidi kwenye vyuo vikuu. Kwa mfumo ulivyo nchini wanafunzi wanapoomba nafasi vyuoni, wanaweza kupangiwa chuo chohote.
Hali hii imekuwa ikiwaathiri wanafunzi wanaotoka katika familia masikini, kwa sababu wanajikuta wamepangiwa chuo kinachotoza karo kwa kiwango kikubwa.
Vyuo ni tofauti na shule kwa sababu mzazi ndiye anayeamua wapi ampeleke mwanawe kulingana na uwezo wa fedha alionao.
Inawezekana hili linalotokea katika taasisi za elimu ya juu ndilo lililoisukuma Serikali kuanzisha kile ilichokiita kama mfumo mpya wa upangaji ada kwa vyuo vikuu.
Akizindua mfumo huo hivi karibuni, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alisema utasaidia kudhibiti viwango vya ada vinavyotozwa kwa wanafunzi.
Alisema Serikali imeanzisha mfumo huo utakaoanza kutumika mwaka huu katika vyuo vyote, kwa lengo la kudhibiti ada kulingana na fani zinazotolewa.
Kwa mujibu wa Dk. Kawambwa, mfumo huu ambao baadaye utaendelea hadi shule za sekondari na msingi, umepatikana kupitia kikosi kazi cha wataalamu ambacho pamoja na majukumu mengine kilipewa kazi ya kutathmini gharama.
Dk. Kawambwa alisema moja ya faida ya utaratibu huo mpya ni kudhibiti taasisi zinazotoza ada kubwa kwa sababu za binafsi ikiwamo biashara.
Itakumbukwa pia kuwa, Aprili 2013 akifungua mkutano mkuu maalumu wa Chama cha Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyokuwa vya Serikali (Tamongsco) uliofanyika mkoani Mbeya, Rais Jakaya Kikwete alisema: “Elimu ni huduma muhimu na haki kwa mtoto kwa hiyo si vyema kugeuzwa kuwa biashara ya faida kubwa.’’
Pamoja na nia njema ya Serikali, nina shaka na utekelezaji wa mfumo huu. Kila ninapoutazama kwa jicho la ndani sioni zaidi ya ugumu katika kuutekeleza.

 

Sasa tuseme ajali za mabasi zimetosha ajali hizi basi

Pamoja na ubora huo, pia mafunzo ya madereva yaangaliwe upya ili kabla ya mtu kupewa leseni awe ameiva, leseni pia tunashauri zidhibitiwe.

Kwa mara nyingine, nchi yetu imepata janga jingine kubwa baada ya ajali mbili kutokea katika mikoa ya Pwani na Kilimanjaro mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha vifo kwa watu zaidi ya 30.
Ajali ya kwanza ilitokea Hedaru wilayani Same, Kilimanjaro ambayo imesababisha vifo vya waombolezaji 12. Nyingine ni ile iliyotokea Rufiji mkoani Pwani ambayo imeua watu 22 na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Tunachukua nafasi hii kipekee kuwapa pole majeruhi wa ajali hizi, tukiwaombea ili wapate nafuu haraka na kuendelea na majukumu yao.
Aidha, tunawapa pole waliofiwa na ndugu, jamaa na marafiki zao katika ajali hizi, hasa kipindi hiki kigumu cha majonzi. Hakuna shaka, ajali hizi ni mfululizo wa matukio ya kusikitisha yanayoendelea kutokea katika barabara nyingi nchini.
Ajali hizi hazitokani na uzembe wa madereva pekee, bali matumizi duni ya barabara zetu ikiwamo nyakati wa mvua za masika au hata kiangazi kutokana na vumbi. Tunashauri kila mtumiaji wa barabara awe makini, atimize wajibu wake ipasavyo.
Tukitumia mfano wa ajali za Same na Rufiji, jambo linalofanana ni magari yaliyohusika katika ajali hizo kugongwa na mengine kwa nyuma. Haya yametokea wakati kuna madai kuwa magari yamekuwa yakiachwa barabarani kwa muda mrefu yakiharibika bila kuondolewa.
Hii, tunasema inaweza kuwa sababu ya magari kugongana na kuuua abiria. Huu, bila shaka ni ushahidi wa jinsi ambavyo madereva, baadhi yao wasivyokuwa makini katika kuendesha vyombo vya moto. Tunashauri, wasimamizi wa uchunguzi wa magari, usalama wake wawe makini ili magari yanayoruhusiwa kuingia barabarani, kubeba abiria yawe kwenye ubora na viwango vinavyostahili.
Pamoja na ubora huo, pia mafunzo ya madereva yaangaliwe upya ili kabla ya mtu kupewa leseni awe ameiva, leseni pia tunashauri zidhibitiwe.
Ni wazi, kuruhusu magari yakiwamo malori madogo maarufu kama kirikuu kubeba abiria jioni au usiku ni mambo ambayo hayakubaliki na ni hatari. Hali hii inatokea katika maeneo mengi nchini ikiwamo Dar es Salaam, ambako askari wapo barabarani mchana kutwa.
Tunasema, udhaifu huu umekuwa sababu ya vifo, nasi kama jamii tunabaki kimya.
Tunashangazwa, kwa mfano, na ruhusa nyingine kwa magari madogo ya mizigo (pick-up), ya familia kama Toyota Noah na mengi yakiwa chakavu kuruhusiwa kubeba abiria.
Tunasema hivyo kwa muwa ndivyo ilivyotokea Same. Ni jambo linalosikitisha kwa kuachwa liendelee huku askari wa usalama barabarani wakishuhudia kana kwamba ni jambo la kawaida. Ruhusa hizi kwa malori madogo kubeba abiria ni jambo linalofanyika Dar es Salaam, mahali ambako kuna askari wengi wa usalama barabarani, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa. Ukimya huu katika roho za watu ni wa nini?

 

Mvua zaleta maafa makubwa Dar, mikoani

Mkazi wa Kijiji cha Bulembo mkoani Kagera, Godena Joseph akitafakari baada ya shamba lake la migomba kuharibiwa na mvua iliyoambatana na upepo. Picha na Issa Ibrahim.  

ar/Pwani/Kagera. Mvua zilizonyesha maeneo mbalimbali nchini tangu wiki iliyopita, zimesababisha maafa, uharibifu wa mali, miundombinu na kuacha zaidi ya familia 150 bila makazi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa athari za kifamilia zimeukumba zaidi Mkoa wa Kagera ambako familia zaidi ya 125 zinahitaji msaada baada ya nyumba zao kuezuliwa paa na mashamba ya migomba kuharibiwa.
Ingawa maeneo mengi ya nchi yameathirika, hali inaonekana ni ya kiwango cha juu zaidi katika mikoa ya Dar es Salaam, Bukoba, Lindi na Mtwara.
Jijini Dar es Salaam, maeneo kadhaa yamejaa maji na hata kusababisha watu kuyakimbia makazi yao kama vile Jangwani, Bonde la Mto Msimbazi na Mbweni ambako Serikali ilipima viwanja na kuvigawa kwa wananchi.
Mkoani Kagera, maeneo yaliyoathirika zaidi ni ya vijiji vya Bulembo, Kata ya Kamachumu wilayani Muleba.
Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage alisema: “Hali siyo nzuri na timu ya watalaamu ipo eneo la tukio ili kufanya tathmini zaidi kuhusu kadhia hiyo.
“Watu wa Msalaba Mwekundu wanajaribu kurejesha paa upya katika baadhi ya nyumba zilizoezuliwa.”
Mkazi wa Kijiji cha Bulembo, Richard Kichabeba alisema familia zilizokumbwa na tatizo la nyumba zao kuezuliwa paa, zinaishi nje na mbaya zaidi nyumba zinazidi kuporomoka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
“Hakuna muhogo wala mgomba. Mawe na upepo vimevuruga kila kitu,” alisema mkazi huyo na kuongeza kuwa mbaya zaidi hata hizo paa zao hazijulikani zimeangukia wapi.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi alisema kuwa uongozi wa wilaya hiyo umelazimika kuifunga kwa muda usiojulikana Barabara ya Msata – Bagamoyo baada ya maji kuifunika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Halima Kihemba alisema kuwa hivi sasa Kata mbili za Ruvu na Kwala hazifikiki baada ya madaraja kubomoka.
Alisema kuwa madaraja mawili ya Mto Ndwati na Msua yamefurika maji hali iliyosababisha mafuriko makubwa, hivyo aliwataka wakazi wa vijiji hivyo kuchukua tahadhari.

 

Sitta ampa barua Mtikila aende kwa JK

Mwenyekiti wa Bunge la Katiba,Samuel Sitta.

Dodoma. Ombi la Mjumbe wa Bunge la Katiba, Mchungaji Christopher la kutaka Bunge hilo livunjwe, limekuwa zito kwa Mwenyekiti Samuel Sitta.
Kutokana na ugumu huo, Sitta amelazimika kumpatia barua Mtikila ili awasilishe hoja yake kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye kisheria ana mamlaka hayo ya kuvunja Bunge la Katiba, ambalo limekuwa likionekana kwenda mrama.
Mtikila, ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Kidemokrasia na mjumbe wa Bunge la Katiba aliwasilisha barua yenye hoja binafsi akitaka bunge hilo livunjwe na wajumbe warejee makwao kwa madai kuwa chombo hicho cha kutunga Katiba mpya hakijali maslahi ya umma na uongozi umekuwa haumtendei haki.
Majibu ya barua hiyo yalikuwa hivi: “Nimeagizwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu nikujulishe kwamba Bunge Maalumu halina uwezo wala mamlaka ya kujitangaza kwamba ni haramu na hivyo livunjwe ; na kwamba hoja hiyo haistahili kuwa hoja ya Bunge Maalumu,” inasomeka barua hiyo iliyoandikwa na katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad.
Akizungumza na Mwananchi jana, Sitta alikiri kumpatia barua hiyo Mtikila ili aende kwa Rais Kikwete kwa sababu hoja yake kutaka kuvunjwa Bunge haiwezi kusikilizwa na chombo hicho kwa kuwa mwenye madaraka ya kuvunja Bunge ni Rais pekee.
“Ni kweli ametuletea hoja ya kuvunja Bunge. Ameandika mambo mengi, akitumia lugha ya uchochezi, kama kudai kwamba ‘Tanganyika imekuwa koloni la Zanzibar kwa muda mrefu’, lugha ya namna hii hatuwezi kuikubali,” alisema Sitta.
Sitta alisema siyo kila kitu ambacho mjumbe anasema, ni lazima kifuatwe katika mchakato huu wa kuandika Katiba Mpya.
“Mtu akija anasema anataka Bunge livunjwe amfuate aliyetuteua, siyo sisi wenyewe kujivunja,” alisema Sitta.
Alisema hoja ya Mtikila, ambaye alitishia kufungua kesi ya kuzuia Bunge la Katiba kufanya kazi, ya kutaka Bunge kuvunjwa imekwenda kinyume kabisa na taratibu za Bunge.
“Hoja hii imekwenda nyuzi 180 kwa sababu aliyetuteua alitaka sisi tutunge katiba kutokana na rasimu, ili sisi tupeleke kwa wananchi rasimu iliyopendekezwa,” alisema.
Mchungaji Mtikila alikiri kupokea barua kutoka Ofisi ya Bunge ikimweleza jambo moja; apeleke hoja yake kwa Rais Kikwete aliyeteua Bunge la Katiba.
Hata hivyo, alisema hakusudii kwenda kumuona Rais Kikwete baada ya kushauriwa kupitia barua ya Bunge kutokana na kutoa hoja ya kutaka kuvunjwa kwa bunge hilo.

Ukawa waanza mapambano nje ya Bunge

Mjumbe wa Bunge la Katiba wa kundi la Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa), Ismail Jussa akionyesha moja ya nukuu za kitabu cha Profesa Issa Shivji wakati wa mkutano na waandishi Dodoma jana. Kushoto ni mjumbe mwenzake, Tundu Lissu. Picha na Salima Shao

Dar /Dodoma/Mwanza. Ni dhahiri kwamba mjadala wa msomi wa Sheria, Profesa Issa Shivji umewavuruga wanasiasa waumini wa serikali mbili ambao baadhi yao jana walimshukia wakidai kuwa “mzee huyu ni ndumila kuwili na kigeugeu.”
Shivji juzi alitoa mjadala kuhusu muundo wa Muungano na kuishutumu Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyopendekeza serikali tatu, kuwa ilipotosha maoni ya wananchi. Alipotakiwa kuzungumzia madai dhidi yake, Profesa Shivji alisema: “Nyie ni waandishi wa habari someni, angalieni wapi mimi nilisema Serikali tatu, wanaosema ninatumiwa na CCM hayo ni maoni yao siwakatazi kuzungumza wanachofikiria.”
Jana Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika kampeni yake nje ya Bunge la Katiba, ulimtaka Profesa Shivji kuwaomba radhi wananchi kwa kile wanachodai kwamba amekuwa kigeugeu kwenye maandishi na matamshi yake kuhusu muundo wa Muungano.
Katika mkutano wake wa kuelimisha wananchi kuhusu Katiba Mpya mjini Mwanza uliojaa polisi kila kona, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa alisema wanamshangaa Profesa Shivji kwa mawazo yake yasiyoeleweka kuhusu muundo wa Muungano.
“Kwa kweli tunaamini watu ambao ni wasomi kama Profesa Shivji wanaweza kuwasaidia wananchi kupata katiba nzuri, lakini anachokifanya sasa ni siasa, jambo ambalo siyo jema,” alisema Dk. Slaa na kuongeza:
“Ukawa tunamtaka awaombe radhi wananchi, kwani amewadhalilisha kwa kuwa kigeugeu. Mara ya kwanza tunakumbuka alikuwa muumini wa Serikali tatu leo anageuka na kuanza kuhubiri serikali mbili, huu ni upuuzi kwa msomi kama yeye kufanya hivyo.”
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema CCM wanaogopa Rasimu ya Katiba kwa sababu wamezoea uchakachuaji.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Abdulkarim Kambaya alisema Rais Kikwete amewachezea akili wananchi, kwani awali alikuwa anaonyesha yupo upande wao lakini kupitia hotuba yake bungeni amewakana na kuibeba CCM.
Lissu, Jussa nao wanena
Pia baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jana walimshambulia kwa maneno Profesa Isa Shivji kuwa ni ‘ndumilakuwili’.
Kwa nyakati tofauti, wajumbe Tundu Lissu na Ismail Jussa walisema kuwa Profesa Shivji “alibebwa na CCM na kulishwa maneno kwa masilahi ambayo hayajulikani.”
Akizungumzia hotuba hiyo, Jussa aliyeweka wazi masilahi yake kuwa ni mwanafunzi wa Profesa Shivji, alisema msomi huyo aliyekuwa tegemeo la wanyonge, alifanya upotoshaji mkubwa ambao umetoa vitisho kwa wananchi.

 

Ripoti ya CAG yaibua utata kisheria

“Tangu uhuru, taarifa ya CAG inawasilishwa katika mkutano wa Bunge wa Aprili kila mwaka. Kwa hali ya sasa, Rais atakaa na taarifa hiyo kwa zaidi ya miezi miwili akisubiri Bunge kukutana.”PICHA|MAKTABA

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kupokea taarifa kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, utata wa kisheria umegubika suala hilo kutokana na ukweli kuwa ibara ya 143 (4) ya Katiba inataka Rais aiwasilishe bungeni taarifa hiyo ndani ya siku saba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema jana kuwa suala hilo lina madhara katika utendaji wa Serikali.
“Kuna madhara makubwa katika mzunguko wa uwajibikaji, kwani ni rahisi Serikali kuichezea taarifa ya CAG kabla haijawa ya umma. CAG anakagua fedha za Serikali kwa niaba ya wananchi kupitia Bunge. Hivyo ni lazima Bunge la Katiba lipishe Bunge la Muungano ili kupokea taarifa ya CAG,” alisema Zitto.
Aliongeza: “Tangu uhuru, taarifa ya CAG inawasilishwa katika mkutano wa Bunge wa Aprili kila mwaka. Kwa hali ya sasa, Rais atakaa na taarifa hiyo kwa zaidi ya miezi miwili akisubiri Bunge kukutana.”
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema siku hizo saba ni baada ya Bunge kuanza.
“Hakuna utata wowote hapo, ukisoma vizuri kifungu hicho kinasema, Rais atamuagiza waziri anayehusika kupeleka taarifa hiyo bungeni siku saba baada ya Bunge kuanza, siyo siku aliyokabidhiwa. Kitu muhimu hapo ni pale kikao cha Bunge kinapoanza bila kujali kinaanza lini,” alisema Balozi Sefue.
“Katika hali ya kawaida, Bunge la Bajeti lilipaswa kuanza Aprili 8. Bunge la Katiba linahitaji pesa kutoka kwenye bajeti. Sioni namna Bunge la Katiba kuendelea kwa sasa. Itabidi liahirishwe mpaka Agosti,” alisema.
Suala la kuahirisha vikao vya Bunge la Katiba kupisha Bunge la Bajeti lilielezwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyesema atamshauri Rais Kikwete kuangalia uwezekano huo.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila akizungumzia uwezekano huo, alisema Bunge hilo litasubiri ratiba ya shughuli za Bunge la Katiba.
Dk Kashilila alisema Kamati ya Uongozi wa Bunge la Katiba inatarajiwa kutoa ratiba ya shughuli zake kuelekea Bunge la Bajeti.
“Inapofika Juni, Serikali inatakiwa kuidhinishiwa fedha kwa ajili ya matumizi yake, kwa hiyo mpango uliopo ni kuhakikisha kabla ya Juni 30, Bunge la Bajeti liwe limeanza kazi zake,” alisema.

TZ, Kenya lawamani kwa kukwamisha biashara A.Mashariki

Kilimanjaro. Tanzania na Kenya zinakwamisha kuanza kazi kwa Kituo cha pamoja cha Mpakani (OSBP) cha Holili wilayani Rombo, ambapo ujenzi wake ulikamilika tangu Desemba mwaka jana.
Kituo hicho ni kwa ajili ya ukaguzi wakati wa kuvuka mpaka wa Tanzania na Kenya, ambapo wananchi wa nchi hizo mbili watakaguliwa katika kituo kimoja badala ya viwili kama ilivyo sasa.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mipaka wa Taasisi ya Trademark East African (TMEA), Theo Lyimo alisema ujenzi wa kituo hicho umefadhiliwa na taasisi hiyo kwa Dola 5.7 milioni (Sh. 9.1 bilioni).
Lyimo aliwaeleza waandishi wa habari wa Tanzania na Kenya waliotembelea vituo vya Holili na Taveta. “Vituo hivi vikianza kazi kama mtu anatoka Tanzania kwenda Kenya atakaguliwa Taveta upande wa Kenya, ambako katika kituo hicho kutakuwa na maofisa wa nchi hizo mbili wa TRA, Uhamiaji na Afya ,” alisema.
Lyimo alisema jengo jingine linajengwa katika mpaka huo lipo katika eneo la Taveta upande wa Kenya litakalogharimu Dola 6.7 milioni (Sh.10.7 bilioni ) ambalo litakamilika katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Alisema pia kwa wasafiri wanaotoka Kenya kwenda Tanzania watakaguliwa katika eneo la Holili upande wa Tanzania ambako pia kutakuwa na maofisa wa nchi hizo mbili.

 

Wafanyabiashara Mwika walalamikia ushuru magari

Moshi. Wafanyabiashara wa mazao ya ndizi na maparachichi katika Soko la Mwika lililopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamelalamikia ongezeko la ushuru wa magari makubwa katika soko hilo.
Hali hiyo imesababisha wenye magari kuhamisha magari yao na kuyapeleka Soko la Mamsera wilayani Rombo na kuwaacha wananchi wa Mwika wakishindwa kuuza bidhaa zao.
Wafanyabiashara hao walikuwa wakiuza bidhaa hizo kwa wafanyabiashara wakubwa wa jijini Dar es Salaam, Kenya na mikoa ya jirani, lakini kwa sasa bidhaa hizo haziuziki baada ya wafanyabiashara wakubwa kukimbia ushuru ulioongezwa na wakala kutoka Sh 40,000 hadi Sh 60,000
Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Dk. Agustino Mrema alikiri kupokea malalamiko hayo na tayari amewasiliana na mkurugenzi wa halmashauri hiyo kufuatilia malalamiko.
Mrema alimuomba mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi kuingilia kati na kukaa na wakala pamoja na wafanyabiashara, ili kutoharibu biashara katika soko la kimataifa ambalo linawaleta wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Fulgence Mponji hakuweza kupatikana kuzungumzia malalamiko hayo. baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana.

 

Programu ya kompyuta kuvuruga ATM wiki ijayo

Kwa mujibu wa Microsoft asilimia kubwa ya benki katika nchi zinazoendelea zinatumia programu ya Windows XP katika kuendesha ATM, hivyo kuwa moja ya waathirika wa mpango huo.

Dar es Salaam. Wiki moja kabla ya kusitishwa huduma za programu ya kompyuta (OS) ya Windows Xp, imefahamika kuwa waathirika wakubwa watakuwa ni benki na taasisi za fedha ambazo hutumia mfumo huo katika mashine za kutolea fedha (ATMs)
Shirika la Microsoft limethibitisha kuwa benki ni miongoni mwa taasisi nyingi zitakazoathirika na mabadiliko hayo.
Baadhi zimeanza kufanyia kazi tatizo hilo, ikiwamo benki moja ambayo jana alasiri ilituma ujumbe kwa wateja wake kuwa, “Ndugu mteja, kuanzia Jumamosi saa 2:00 usiku Aprili 5, mpaka Jumapili saa 12:00 asubuhi tutakuwa tunaboresha mashine zetu za ATM, hivyo kadi yako haitafanya kazi kwa kipindi hiki. Asante.”
Kwa mujibu wa Microsoft asilimia kubwa ya benki katika nchi zinazoendelea zinatumia programu ya Windows XP katika kuendesha ATM, hivyo kuwa moja ya waathirika wa mpango huo.
Katikati ya Machi, Microsoft ilitangaza kusitisha huduma zote zinazohusiana na bidhaa zake za Windows Xp kufikia Aprili 8, mwaka huu. Pia shirika hilo litasitisha ufanisi wa programu ya kuzuia na kupambana na virusi ya Microsft Security Essentials katika mfumo wa Windows Xp, hivyo kufanya urahisi wa kompyuta zinazoitumia kukosa ulinzi.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Twiga Hosting, Jacob Urassa alisema Watanzania hawatakiwi kupuuza onyo hilo kwa kuwa ikifika Aprili 9 usalama wa taarifa zao utakuwa hatarini.
“Windows XP ni dhaifu mara tano zaidi ya Windows 7 na 8, kwa hiyo Microsoft wameona ni bora wakaitoa sokoni. Kwa maana hiyo ATM na kompyuta zote zinazotumia programu hizo hazitakuwa na ulinzi wa uhakika,” alisema Urassa ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Teknolojia ya Mawasiliano (IT).
Alisema kuwa kuna idadi kubwa sana ya Watanzania wanaoendelea kutumia bidhaa hizo zikiwemo taasisi kubwa nchini hivyo kuna haja kubwa ya kuchukua hatua za kubadilika na teknolojia.
Naye, Ofisa Uhusiano wa Benki ya Posta, Noves Moses aliwatoa wasiwasi wateja wake kuwa licha ya kusitishwa kwa matumizi ya Windows XP, bado benki hiyo itaendelea kutoa huduma zenye kiwango kile kile.

 

Magaidi waua watu 6 Kenya 

Watu sita wameuawa na wengine 25 kujeruhiwa vibaya katika shambulizi la kigaidi katika eneo la California mtaa wa Eastleigh, viungani mwa mji wa Nairobi.

Waathiriwa wa shambulizi wakipelekwa hospitalini 

Kamanda wa Polisi mjini Nairobi Benson Kibue amesema kuwa milipuko miwili ilitokea wakati magaidi waliporusha vilipuzi katika mikahawa miwili midogo.
Mlipuko wa tatu ulitokea katika kituo cha mabasi ya uchukuzi kilichoko karibu na zahanati za afya ya mama na mtoto.
Miongoni mwa waliojeruhiwa walikuwa ni wanawake waliokuwa wanauza mboga na bidhaa zingine za rejareja.
Kwa mujibu wa polisi wale waliouawa walikuwa wamekwama ndani ya mkahawa huo baada ya mlango kufungwa kutoka nje na washambulizi waliorusha bomu ndani .
Waathiriwa walikuwa wameenda kununua chakula cha jioni.
Idadi kubwa ya wakimbizi wa kisomali wanaishi katika mtaa wa Eastleigh.
Inaarifiwa washambuliaji walitumia maguruneti au mabomu ya kutengezwa nyumbani kufanya mashambulizi hayo
Mashambulizi haya yanawadia siku moja tu baada ya mtu anayeshukiwa kuwa gaidi kufa kilipuzi alichokuwa akikiunganisha kilipolipuka .
Isitoshe wakenya bado wanaomboleza vifo vya waumini 6 waliouawa katika kanisa moja mjini likoni Mombasa majuma mawili yaliyopita.
Mtaa wa Eastleigh unafahamika kama ''Mogadishu ndogo'' kutokana na idadi kubwa ya wasomali wanoishi hapo wengi wakiwa ni wakimbizi.
Mtaa huu ambao ni kitovu cha biashara umepigwa darubini na serikali ya Kenya haswa baada ya visa vingi vya ugaidi kuhusishwa na kundi la wapiganaji wa kiisalmu la Al Shaabab ambao wamepinga vikali kuweko kwa majeshi ya Kenya nchini Somalia kama sehemu ya AMISOM.

Kesi dhidi ya Rais Kenyatta yaahirishwa

Rais Uhuru Kenyatta 

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC imehairisha kesi dhidi ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta hadi tarehe saba Oktoba mwaka huu.
Rais Kenyatta anatuhumiwa kwa makosa ya jinai kufuatia machafuko ya baada ya uchaguzi wa mkwaka 2007 - 2008, madai ambayo ameyakanusha.
Mahakama kuu ya ICC, kupitia mwendesha mashitaka Fatou Bensouda, imekuwa ikiitaka serikali ya Kenya kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuendesha kesi zinazowakabili Rais Kenyatta na naibu wake bwana Ruto.
Hii ni mojawapo ya sababu kuu ya kubadili tarehe ya kusikizwa kwa kesi hii.
Upande wa mashitaka umesema kuwa unaipa Kenya muda wa ziada ili kutafuta na kuwasilisha baadhi ya stakabadhi za benki zinazohitajika katika kesi hiyo.
Kumekuwa na malalamishi kutoka kwa upande wa mashitaka kuwa serikali ya Kenya inalenga kuzuia stakabadhi hizo kufikishwa mahakamani jambo ambalo mawakili wa bwana Kenyatta wamekanusha.
Miongoni mwa yale yanayohitajika kotini ni pamoja na taarifa ya maelezo ya fedha anazomiliki bwana Kenyatta.
Kesi hii imekumbwa na matatizo ya mashahidi kujiondoa na shutuma za mahakama hii kuonea viongozi wa bara Afrika.