Wafanyakazi Muhimbili walilia Sh800 mil zao
Dar es Salaam. Wafanyakazi wa Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili (MNH) wameulalamikia uongozi wa hospitali hiyo kwa
kushindwa kuwalipa fedha zao na kuzitumia kinyume na utaratibu
uliopangwa.
Fedha zinazotajwa kutolipwa ni pamoja na Sh800
milioni za posho ya awamu ya tatu zinazotokana na mapato ya wateja wa
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambazo imedaiwa zilitumika kununulia
vifaa tiba vya hospitali hiyo na fedha za likizo za tangu mwaka jana.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyakazi hao
walisema hawajalipwa posho hizo tangu Januari, 2013 baada ya kuelezwa na
mkurugenzi wa hospitali hiyo kuwa fedha hizo zitaelekezwa kununulia
vifaa vya hospitali.
“Tunashindwa kuelewa hawa viongozi wetu! wanatumia
fedha kwa maelekezo tofauti, hii inasababisha kuwapo na migogoro ndani
ya kazi,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Mtoa habari huyo alisema wafanyakazi wameshangazwa
na kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Marina Njelekela
kudai hawatalipwa posho na kwamba fedha hizo zitanunulia vifaa.
“Tunatakiwa kulipwa fedha hizo kama tahadhari.
Mfano unaweza ukamuhudumia mgonjwa wa Ukimwi na ikatokea katika kumtibia
akakuambukiza hela hii unayolipwa ndiyo kazi yake,” alisema.
Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha alikiri uongozi wa MNH kutumia fedha hizo kwa matumizi mengine.
Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii, Dk. Seif Rashid
alisema alipata taarifa hizo na walikaa kikao na Bodi, mkurugenzi na
chama cha Tughe kujadiliana suala hilo kwa kuwa ni la kisheria zaidi.
“Hili suala lipo kisheria zaidi. Niliwaagiza
waende wakakae pamoja wajadiliane waweze kupata mwafaka ili wawalipe
wafanyakazi hao,” Dk. Seif.
No comments:
Post a Comment