Friday 7 March 2014

Ngumi mkononi bungeni

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Magdalena Sakaya (kushoto), akizozana na Magdalena Likwina baada ya Semina ya Kupitia Vifungu vya Rasimu ya Kanuni kuahirishwa kutokana na vurugu zilizotokea bungeni jana. Picha na Silvan Kiwale  

Dodoma. Ngumi mkononi ndilo neno jepesi ambalo linafaa kutumika baada ya vurugu kubwa kutokea jana ndani ya Ukumbi wa Bunge Maalumu la Katiba kiasi cha kumlazimisha Mwenyekiti wa Muda, Pandu Ameir Kificho kuahirisha semina kabla ya wakati wake.
Semina ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, imekuwa ikianza saa 4:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana kabla ya kuendelea tena kuanzia saa 11:00 jioni hadi saa 3:00 usiku. Jana, katika kipindi cha asubuhi, semina hiyo iliahirishwa saa 6:17 licha ya kuanza saa tano asubuhi kabla ya kurejea tena saa 10 jioni.
Ngumi zilitaka kupigwa baada ya Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Abubakari Hamis Bakari kuhoji uhalali wa Christopher Ole Sendeka na Ummy Mwalimu kuchangia wakati hawakuwamo katika orodha ya wachangiaji jambo ambalo liliibua mjadala mkali na kurushiana maneno kabla ya Mwenyekiti Pandu Ameir Kificho kuahirisha semina hiyo.
Chanzo cha vurugu
Kificho alimpa Ole Sendeka nafasi ya kuchangia Kifungu namba 58 cha rasimu ya kanuni na baada ya kutoa mchango wake, Hamisi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kanuni, alisimama na kumtaka Mwenyekiti Kificho kuacha kuwateua watu ambao hawamo katika orodha ya wachangiaji.
Kificho hakumsikiliza na badala yake, alimpa nafasi mjumbe mwingine wa Bunge hilo Ummy Mwalimu ambaye pia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, kuchangia. Hata hivyo kabla hajafanya hivyo, Bakari alisimama tena na kumzuia kuchangia kwa madai kuwa hakuwamo kwenye orodha ya wachangiaji.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaendelea na utaratibu huu suala la kuchangia kanuni linaweza kutupeleka hadi miezi sita bila ya kumaliza. Haya majina hayakuwemo kwenye orodha ya wachangiaji na huyo aliyemaliza sasa Ole Sendeka, naye hakuwamo, naomba tuache mchezo huu,” alisema Bakari.
Aliendelea: “Sekretarieti inakuchomekea majina mwenyekiti na kama hivyo ndivyo, basi tunatakiwa kuwachukulia hatua kali hawa kwani tunataka kujadili hoja ambazo hazimo.”
Bakari alisema wajumbe waliotakiwa kuchangia ni wale ambao walipeleka majina kwa makatibu wa Bunge hilo pamoja na michango yao kwa maandishi ili wapewe nafasi ya kuzungumza, lakini Kificho alikuwa akiwateua wajumbe ambao hawamo katika orodha hiyo.
Kificho ajibu
“Mimi sina tatizo na jambo hilo, mkisema tuendelee basi sawa, lakini mkitaka tufanye mambo kwa uzuri inawezekana pia, jambo la muhimu ni kuwa tupo hapa kutengeneza Katiba ya wananchi siyo ya vyama.”
Kelele zilianza kusikika huku wajumbe wakiimba kuwa mwenyekiti anayumba… na kumtaka mwenyekiti atoke nje na kukiacha kiti, kwani anafanya upendeleo.

 

No comments:

Post a Comment