Wavuvi: Mradi wa gesi unatupunguzia samaki baharini
Katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili sasa upatikanaji wa
samaki wa kitoweo katika pwani ya Bahari ya Hindi, eneo la Mkoa wa
Mtwara, umekuwa mgumu.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya
hivi karibuni, umebaini kuwa mabadiliko ya hali ya hewa na zana duni za
uvuvi zinachangia hali hiyo.
Lakini wakazi wa Mtwara ambao baadhi yao
wanategemea uvuvi, wanaamini kuwa upungufu wa samaki, umechangiwa na
ongezeko kubwa la mahitaji ya samaki tofauti na uwezo wa wavuvi
kulilisha soko la walaji.
Pamoja na wavuvi kukiri kuongezeka kwa soko la
samaki, wanasema upatikanaji wake umekuwa mgumu hata kwa wale
wanaotumia zana nzuri katika uvuvi.
Wavuvi wanaamini kuwa uchimbaji wa nishati ya gesi
asilia imesababisha mabadiliko ya hali ya hewa baharini kutokana na
matumizi ya kemikali za kulipua ndani ya bahari wakati wa utafiti na
uchimbaji.
“Hapo awali kabla ya kuanza uchimbaji wa gesi
asilia baharini, tulikuwa na upepo wa matalai, upepo wa mlaji na upepo
wa umande. Pepo hizo zilikuwa mwongozo kwetu kwenye shughuli zetu za
uvuvi,” anasema Ali Hamis Kimbaumbau, mvuvi na mkazi wa mjini Mtwara.
Anafafanua kuwa pepo za matalai na umande ambazo
ni upepo wa kusini huwa ni shwari na zikiambatana na upepo ambao ulikuwa
unatoa fursa kwa wavuvi wanaotumia mitumbwi kwenda baharini. Kipindi
hicho wavuvi walikuwa wanapata samaki ingawa si kwa kiwango kikubwa.
Anabainisha kuwa kwa sasa pepo wanazopata ni za
kaskazi ambazo huambatana na upepo mkali, hali inayozuia wavuvi wenye
mitumbwi isiyotumia mashine kushindwa kwenda baharini. Wavuvi
wanaofanikiwa kwenda baharini hurudi na mapato duni.
Mvuvi mwingine, Salumu Liwanje (36) anasema
wamefikia hatua ya kuamini utafiti na uchimbaji wa gesi asilia baharini
ndiyo chanzo.
Anaeleza kuwa siku moja wakiwa baharini, eneo la
Luvula walibaini nyaya zenye umeme baharini na walirushwa wakati
walipojaribu kugusa maji hayo. Alisema baadaye walisikia sauti ya
milipuko mara kadhaa hali waliyodai inaharibu mazingira ya asili ya
bahari.
“Joto limeongezeka sana baharini. Hiyo hali si ya
kawaida, ukiingia bahari kuu utakutana na joto ambalo si la kawaida
kabisa. Sisi tulizoea nyakati za usiku baharini kunakuwa na baridi kali,
lakini hali ni kinyume kwa sasa,” anabainisha Liwanje.
“Unajua wengine tukisema mabadiliko tunayoyaona
wapo, watakaosema ni walewale wasiopenda mradi wa gesi. Sasa sisi kama
wavuvi tukigusa yale maji yaliyotandazwa nyaya tunarushwa na umeme, je
samaki wataishi eneo hilo? ” anahoji mvuvi huyo.
No comments:
Post a Comment