Wednesday 9 April 2014

Miyeyusho ayayushwa

Dar es Salaam. Pambano la bondia Francis Miyeyusho na Ronald  Pontillas wa Ufilipino lililokuwa lifanyike leo limeahirishwa hadi Aprili 12, kutokana na sababu ambazo ziko juu ya uwezo wa waandaaji.
Katibu Mkuu wa Chama cha Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST), Anthony  Lutha, alisema pambano la Miyeyusho limeahirishwa kutokana na sababu ambazo ziko juu ya uwezo wao.
Promota wa pambano hilo, Mussa Kova alisema, pambano la Miyeyusho  na Pontillas limeahirishwa baada ya  kocha wa bondia huyo kupewa taarifa tofauti kutoka hapa nchini.
“Pontillas aliambiwa pambano halitakuwepo na kiongozi wa ngumi (alimtaja jina) na alimwambia kuwa Miyeyusho ana pambano Aprili 26, hivyo hawezi kucheza Aprili 5 na kweli walipoangalia kwenye mtandao boxrec wakaliona hilo pambano hivyo wakaghairi kuja,” alisema Kova.
Alisema pambano hilo limesogezwa mbele hadi Jumamosi ijayo ambapo sasa Miyeyusho atapigana na bondia mwingine wa Ufilipino, Angelito Merin.

 

Tuzo za Kili zichague muziki bora siyo maarufu

Wasanii wa muziki wa kizazi kipya Banana Zorro (kushoto) na Ray C (kulia) baada ya kutwaa tuzo za Kili Music Awards mwanzoni mwanzoni mwa mwaka 2007 

Tuzo maarufu za muziki nchini ‘Kilimanjaro Music Award’ zinazoratibiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa kushirikiana na kampuni ya bia (TBL) zinatarajiwa kufanyika Mei 3 kwenye Uukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Basata na TBL, tuzo za mwaka huu zimefanyiwa mabadiliko katika mchakato wa kupata wateule watakaoingia katika vipengele mbalimbali.
Mabadiliko hayo ni kwamba wananchi wa kawaida walipewa fursa ya kupendekeza wanamuziki, nyimbo, vikundi, watayarishaji, video na vitu vingine wanavyodhani vinastahili kuwapo katika mchakato wa kuwapata wateule wa tuzo za muziki Tanzania tangu mwezi Februari.
Wananchi hao wa kawaida tangu Februari walipewa nafasi ya kutoa mapendekezo yao kwa kutumia mfumo wa SMS, na mtandao yaani tovuti na barua pepe.
Baada ya wananchi kutoa mapendekezo hayo, Basata, TBL na jopo la wataalamu wa tuzo hizo waliyachuja majina katika kila kipengele na kubakizsha majina matano ambapo hivi sasa wameyarudisha kwa wananchi kwa ajili kupigia kura washindi wa kila kipengele.
Washindi watakaopata kura nyingi baada ya kuchaguliwa na wananchi katika kila kipengele ndiyo watakaopewa tuzo zao katika hafla itakayofanyika Mei 3 kwenye Uukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Siku zote sisi tunaamini kwamba mabadiliko ni kitu cha muhimu katika maisha ya mwanadamu au katika shughuli tunazozifanya, lakini mabadiliko yasiwe katika kukwepa majukumu.
Tunasema hivyo kwa sababu tunaona utaratibu huu mpya umesahau kufikiria jambo moja kubwa la msingi kwa hizi ni tuzo za kutafuta muziki bora na siyo tuzo za kutafuta muziki maarufu.
Ni wazi kuwa siku zote wananchi wa kawaida huwa wanasikiliza nyimbo zinazopigwa kwenye vituo vya redio na televisheni mara kwa mara na wengi hawana utaalamu wa muziki.
Nyimbo nyingi zinazopigwa kwenye radio au kuonyeshwa kwenye televisheni ni nyimbo maarufu na siyo lazima ziwe ni nyimbo bora kwa sababu siku hizi wanamuziki hutoa fedha ili nyimbo zao zipigwe kwenye radio na kuonyeshwa kwenye televisheni.
Ndiyo maana tunasema mabadiliko ya kukimbia wajibu siyo mazuri kwani suala hili la kuchagua muziki bora linahitaji utaalamu kwa sababu kuna nyimbo nyingine ni bora, lakini hazipati nafasi ya kupigwa kwenye radio au kuonyeshwa kwenye televisheni kwa sababu wanamuziki wenye nyimbo hizo hawatoi fedha.
Hii inamaanisha katika tuzo za mwaka huu washindi watakaopatikana watakuwa ni wanamuziki, nyimbo au vikundi vinavyopata nafasi ya kupigwa kwenye readio au kuonyeshwa kwenye televisheni.
 

 

Yala: Shule iliyogeuka ‘kisiwa’

Sehemu ya Shule ya msingi Yala ikiwa  imejaa maji.

Yala ni shule ya msingi iliyopo katika Kijiji cha Yala Kata ya Luhanga Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya na ipo umbali wa kilomita 40 kutoka Barabara Kuu ya Mbeya-Iringa, ili kufika shuleni hapo inakulazimu kutembea kwa mguu kutokana na magari na pikipiki kushindwa kufika.
Shule hiyo ina muda wa zaidi ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, imezungukwa na mito minne ambayo imekuwa ikijaa maji kipindi cha masika na kusababisha kukatika kwa mawasiliano na ukosefu wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu.
Kutokana na tatizo hilo la mito kujaa maji shule hiyo imekuwa ikigeuka kuwa kisiwa na kusababisha wanafunzi na walimu kushindwa kufika shuleni kwani mito hiyo haina madaraja ya kuwawezesha kupita na kufika shuleni hapo.
Wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo wamekuwa wakitoka katika Vitongoji vya Mwashikamile, Ruaha, Waninyika, Mtakuja, Yala na Lusaka na wote hushindwa kuvuka mito hiyo na kufika shuleni huku walimu pia wakikumbwa na adha hiyo kutokana na shule hiyo kutokuwa na nyumba za kuishi Walimu.
Jairos Mpale ni Mwenyekiti wa serikali ndogo ya maendeleo ya Mwashikamile katika Kijiji cha Yala anasema kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa zaidi kwa mwaka huu ukilinganisha na miaka mingine.Hii ni kutokana na mvua zinanyesha kwa wingi na wanafunzi wamekaa nyumbani muda mrefu bila kwenda shule.
“Watoto wetu wameshindwa kwenda shuleni hapo tangu shule zote zilipofunguliwa Januari, kutokana na mito kujaa maji na kuna mamba wengi na viboko hivyo ni vigumu kuvuka kwenda katika Shule ya Yala na watoto wetu wamekosa masomo na hatujui ni lini wataanza masomo,” anasema.
Naye Mtendaji wa kijiji cha Yala shule ilipo, Isaac Ngera anasema kuwa tatizo hilo huwa linajitokeza mara kwa mara katika msimu wa mvua na mito hiyo imekuwa ikijaa na kusababisha wananchi kushindwa kupata huduma mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja elimu, afya na majisafi na salama.
Aliitaja mito iliyojaa maji kuwa ni Itambo na lwashimala na vitongoji vilivyopo ng`ambo ya mito hiyo ni Ruaha na Woninyika kwa upande wa Kusini kuna vitongoji vya Mtakuja na Lusaka ambavyo vipo ng`ambo ya Mto Itambo na yote imejaa maji hakuna mawasiliano na upande wa pili.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Stephano Mlewa anasema kuwa kwa sasa hali ni mbaya katika shule hiyo kwani hakuna mwanafunzi anayefika shuleni hapo.
“Siyo kwa wanafunzi pekee hata kwa Walimu ni tatizo kubwa kwani wanaishi katika kitongoji ambacho kipo mbali na shule hiyo na inawalazimu wavuke mito miwili ambayo kwa sasa imejaa maji hivyo hakuna masomo,” anasema.
Anasema kuwa shule hiyo pia ina changamoto ya madarasa kwani ina jumla ya vyumba vya madarasa vinne pekee na wanafunzi wapo kuanzia darasa la kwanza hadi la saba hivyo husoma kwa kupokezana.
Ofisa Elimu Wilaya ya Mbarali, Henerico Batinoluho anasema kuwa shule ina wanafunzi zaidi ya 400 na kwamba mwaka huu shule ilifunguliwa Januari 6, lakini wamefanikiwa kuingia darasani katika kipindi cha wiki moja pekee.

WHO: uvumi wa maambukizi ya Ebola ukome

  

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema kuwa kuzuka kwa Homa ya Ebola Magharibi mwa Afrika ni mojawapo ya changamoto kubwa zaidi ambazo limewahi kukabiliana nayo.
Shirika hilo limesema kuwa italichukua hadi miezi minne kuthibiti ugonjwa huo. Wakati huohuo shirika la kutoa misaada ya matibabu ya bure, Medicins Sans Frontieres, limesema kuwa linaendelea kufanya mashauriano na viongozi wa kijamii katika Wilaya moja Kusini mwa Guinea, ambalo lilisimamisha shughuli zake baada ya vituo vyake kadhaa kushambuliwa na wakaazi wa eneo hilo.
Msemaji wa shirika hilo katika mji mkuu wa Guinea wa Conakry - Sam Taylor - amesema inaeleweka kwamba watu wana uoga mkubwa.
"Sio taharuki, kimsingi huu ni uoga. Na tunaelewa hilo. Ni ugonjwa wa kugovya na pia ni mpya nchini Guinea, na kuna uvumi unaosambaa na pia kuna habari za kuotosha zinazoenea; na tunachohitaji kuona kwa wingi sasa ni watu kwenda kwa jamii mbalimbali kueleza ugonjwa huu, jinsi unavyoenea, na jinsi usivyoenea," alisema Bwana Taylor.
Ugonjwa huo umewaua watu 111 katika nchi za Guinea na Liberia tangu uchipuke mwezi uliopita.