Wednesday 9 April 2014

Tuzo za Kili zichague muziki bora siyo maarufu

Wasanii wa muziki wa kizazi kipya Banana Zorro (kushoto) na Ray C (kulia) baada ya kutwaa tuzo za Kili Music Awards mwanzoni mwanzoni mwa mwaka 2007 

Tuzo maarufu za muziki nchini ‘Kilimanjaro Music Award’ zinazoratibiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa kushirikiana na kampuni ya bia (TBL) zinatarajiwa kufanyika Mei 3 kwenye Uukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Basata na TBL, tuzo za mwaka huu zimefanyiwa mabadiliko katika mchakato wa kupata wateule watakaoingia katika vipengele mbalimbali.
Mabadiliko hayo ni kwamba wananchi wa kawaida walipewa fursa ya kupendekeza wanamuziki, nyimbo, vikundi, watayarishaji, video na vitu vingine wanavyodhani vinastahili kuwapo katika mchakato wa kuwapata wateule wa tuzo za muziki Tanzania tangu mwezi Februari.
Wananchi hao wa kawaida tangu Februari walipewa nafasi ya kutoa mapendekezo yao kwa kutumia mfumo wa SMS, na mtandao yaani tovuti na barua pepe.
Baada ya wananchi kutoa mapendekezo hayo, Basata, TBL na jopo la wataalamu wa tuzo hizo waliyachuja majina katika kila kipengele na kubakizsha majina matano ambapo hivi sasa wameyarudisha kwa wananchi kwa ajili kupigia kura washindi wa kila kipengele.
Washindi watakaopata kura nyingi baada ya kuchaguliwa na wananchi katika kila kipengele ndiyo watakaopewa tuzo zao katika hafla itakayofanyika Mei 3 kwenye Uukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Siku zote sisi tunaamini kwamba mabadiliko ni kitu cha muhimu katika maisha ya mwanadamu au katika shughuli tunazozifanya, lakini mabadiliko yasiwe katika kukwepa majukumu.
Tunasema hivyo kwa sababu tunaona utaratibu huu mpya umesahau kufikiria jambo moja kubwa la msingi kwa hizi ni tuzo za kutafuta muziki bora na siyo tuzo za kutafuta muziki maarufu.
Ni wazi kuwa siku zote wananchi wa kawaida huwa wanasikiliza nyimbo zinazopigwa kwenye vituo vya redio na televisheni mara kwa mara na wengi hawana utaalamu wa muziki.
Nyimbo nyingi zinazopigwa kwenye radio au kuonyeshwa kwenye televisheni ni nyimbo maarufu na siyo lazima ziwe ni nyimbo bora kwa sababu siku hizi wanamuziki hutoa fedha ili nyimbo zao zipigwe kwenye radio na kuonyeshwa kwenye televisheni.
Ndiyo maana tunasema mabadiliko ya kukimbia wajibu siyo mazuri kwani suala hili la kuchagua muziki bora linahitaji utaalamu kwa sababu kuna nyimbo nyingine ni bora, lakini hazipati nafasi ya kupigwa kwenye radio au kuonyeshwa kwenye televisheni kwa sababu wanamuziki wenye nyimbo hizo hawatoi fedha.
Hii inamaanisha katika tuzo za mwaka huu washindi watakaopatikana watakuwa ni wanamuziki, nyimbo au vikundi vinavyopata nafasi ya kupigwa kwenye readio au kuonyeshwa kwenye televisheni.
 

 

No comments:

Post a Comment