Wednesday 5 March 2014

Singapore mji ghali zaidi duniani

Singapore umetajwa kuwa mji ghali zaidi duniani kuishi kwa mwaka 2014 na kuipiku miji mingine 131 kwa mujibu wa taarifa ya Economist Intelligence Unit (EIU).

 

Nguvu ya sarafu ya mji huo ikiwa ni pamoja na gharama kubwa ya uendeshaji magari na kuongezeka kwa malipo ya huduma za umma kumechangia Singapore kuwa juu ya miji yote duniani kwa ughali wa maisha.

Pia ni mahali ambapo nguo zinauzwa kwa bei ya juu kabisa kuliko miji yote duniani.
Singapore imechukua nafasi ya mji wa Tokyo, amao ulikuwa unaongoza kwa ughali wa maisha mwaka 2013.
Miji mingine mitano inayoongoza kwa gharama kubwa za maisha duniani ni pamoja na Paris, Oslo, Zurich na Sydney, huku Tokyo ukiporomoka hadi nafasi ya sita.
Mji wa New York unatumiwa kama kigezo cha utafiti wa shirika la EIU kuhusu gharama za maisha katika miji mbalimbali duniani. Wanaangalia zaidi ya bei binafsi 400.

 

Magari ya umma yavuruga shughuli Nairobi

Huduma za usafiri jijini Nairobi zimekwama kufuatia hatua za wenye magari kugoma hii leo wakilalamikia nyongeza ya ada ya kuegesha magari jijini humo
.
Mgomo wa wahudumu wa magari nchini Kenya

Maelfu ya wafanyakazi wamelazimika kutembea kwa miguu na wasafiri wa kutoka jijini kwenda maeneo ya mashambani nao kulazimika kuahirisha safari zao.
Mwenyekiti wa wenye matatu katika eneo la Mlima Kenya, Bwana Michael Kariuki, ambaye aliongea na BBC akiwa nje ya lango la kuingia kwenye afisi ya Gavana wa Kaunti ya Nairobi, alisema mzozo uliopo ni mdogo na waweza kusuluhishwa haraka.
"Juzi tulikuwa na Gavana Evans Kidero na tukakubaliana kiasi tunachopaswa kulipa lakini jana tulipofika wafanyakazi wa kaunti wakakataa kiasi tulichokuwa nacho," Bwana Kariuki alisema.
Jiji la Nairobi ni mojawapo wa kaunti ambazo zimebuniwa chini ya Katiba iliyopitishwa na wapiga kura na kuidhinishwa mwaka 2010 katika hatua ya kuimarisha huduma kwa wananchi.
Kaunti hizo mpya hata hivyo zimejikuta njia panda baada ya kupata madaraka bila fedha za kuandamana nayo; ambapo zimelazimika kuongeza kodi kama njia mojawapo ya kujiimarisha kiuchumi.