Friday 7 March 2014

Suleiman Abdallah: Mwanafunzi wa IFM aliyechora nembo ya ukumbi wa Julius Nyerere

SULEIMAN Abdallah (24) ni mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) jijini Dar es Salaam ambaye hivi karibuni aliweka historia kwa kushinda kuchora nembo ya ukumbi maarufu jijini Dar es Salaam.
Abdallah anayechukua shahada ya Mawasiliano ya Habari na Teknolojia (ICT) aliibuka mshindi wa kuchora nembo hiyo ya Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) kati ya washiriki 272.

 “Ninaamini kuwa katika shindano hili la kubuni nembo ya jengo hili la kimataifa mimi nilikuwa wa mwisho kutuma kwani nilituma saa 1:45 usiku wa siku ya deadline (siku ya mwisho),” anasema Abdallah.
Nikiwa mmoja wa waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa nembo hiyo ya jengo hilo la kimataifa wiki mbili zilizopita uliofanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, nilipata nafasi ya kuzungumza na kijana huyo. Kijana huyo ambaye mara zote ni mcheshi na akitaniana na ndugu pamoja na wanafunzi wenzake huku akionesha furaha ya kuwa mshindi, anasema kuwa ushindi wake ni wa familia na kampuni yake yenye wenzake watatu.

Abdallah ni kitinda mimba akiwa na pacha wake, Hannat, katika familia ya mama Lulua Chandoma na baba Said Chandoma wenyeji wa Pemba katika mji wa Zanzibar. Abdallah anasema alipata ushindani mkubwa katika uchoraji wa nembo hiyo kutoka kwa marafiki zake huku akiungwa mkono na wazazi wake.

Anabainisha kuwa katika shindano hilo aliweza kujinyakulia Sh milioni tano na cheti maalumu, zawadi ambazo alisema anazipeleka katika kampuni ikiwa ni moja ya hamasa kuongeza juhudi katika shughuli zake. Abdallah anasema akiwa mdogo alipenda kuchora michoro mbalimbali lakini alipofika kidato cha sita alianza kuchora picha kwa kutumia utaalamu wa kompyuta ujulikanao kama Photoshop.

Anasema lakini alipofika chuo kikuu akiungana na wenzake wawili ambao alisoma nao awali, waliamua kuanzisha kampuni na kutengeneza nembo, ‘banners’, mabango na stika mbalimbali huku wakiendelea na masomo. Anasema mwaka huu walianza kutengeneza kwa kutumia utaalamu wa kwenye kompyuta wa Illustrator ambao anakiri kuwa yote wanafanya kwa kipaji na utundu kwani hawafundishwi popote shuleni.
“Uchoraji huu nimeufanya tangu mtoto na nimekuwa kila mara nikijifunza mwenyewe, hivyo kwa kushirikiana na wenzangu mwaka jana tuliamua kuanzisha kampuni yetu wenyewe,”anasema. Anawataja wenzake katika kampuni yao iitwayo Alpha Arts akimaanisha kuwa sanaa wanayofanya kwanza, ni Owen Patrik (23) wanayesoma naye IFM na Edwin Mmuni (23) anayesoma chuo cha Arusha.

Akizungumzia jinsi wanavyofanya kazi huku mmoja akiwa Arusha anasema mara nyingi hutumia simu kwa kupiga na wakati mwingine hutumia utaalamu wa kujadili pamoja kwa simu kwa wakati mmoja (Conference Call). Anasema kwa sasa wanamalizia usajili wa kampuni hiyo ambayo wamempa kazi Mwanasheria kusimamia usajili kutokana na kuwa wao wako vyuoni huku wakiendelea na kazi wanazopata kwenye kampuni yao.
Abdallah anasema wanatarajia ifikapo Aprili mwaka huu watazindua rasmi kampuni yao pamoja na tovuti itakayoonesha kazi zao zote walizowahi kufanya. Kushiriki Shindano la Nembo Abdallah anasema siku tatu kabla ya kufikia tarehe ya mwisho ya shindano ndipo mmoja wa marafiki zao aliwataarifu kuwepo wa shindano hilo na kuwataka kujaribu.

Anasema wote walipatwa na shauku ya kufanya hivyo lakini kutokana na siku hiyo kuwa na kazi nyingine katika kampuni yao ambazo zilishalipiwa na wateja zilitakiwa kuchukuliwa siku hiyo. Kutokana na hali hiyo, kulitokea ubishani mkubwa baina yao ambapo wapo waliotaka kumalizia kazi waliolipwa kwani ubunifu wa nembo ni kubahatisha tu huku yeye akiwataka kufanya zote.

Mwisho yeye akikazania jambo lililowafanya wenzake kujitoa wakati wameshaanza ubunifu wa awali kwa pamoja hivyo yeye akaamua kuendelea na ubunifu wa nembo hiyo. Anasema wakati mwisho wa kupeleka nembo hizo za ushindani ikiwa Desemba 31 mwaka jana, yeye siku ya Desemba 30 ndipo alipofika na kuliona jengo lenyewe ambalo awali alikuwa halifahamu.

“Baada ya kuliona kwani awali nilitengeneza nembo yenye sura ya Baba wa Taifa nikaamua kulibadilisha na kuweka picha ya jengo kama unavyoona na kutengeneza mandhari ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuweka mnazi na alama ya bahari,” anasema. Alisisitiza kuwa alitengeneza akiwa na madhumuni ya kujaribu tu kwani aliamini zipo kampuni kubwa zitakazoshiriki hivyo yeye kuwa vigumu kushinda ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki katika shindano kama hilo.

Abdallah anasema akiwa na wenzake walituma mara 10 nembo hiyo baada ya kukamilika siku hiyohiyo ya mwisho kuanzia saa 10 jioni hadi saa 1:45 usiku ilipokubali kwenda. “Siku hiyo, mtandao ulikuwa ukisumbua sana kutokana na kuwa ni mwisho wa mwaka hivyo tulijaribu kutuma lakini ilikuwa imekataa na mara nyingine nilikuwa nakata tamaa kabisa lakini ilipofika muda huo ikakubali,”anasema.

Abdallah anasema kuwa baada ya kushinda shindano hilo amepata mwamko na yuko tayari kushiriki mashindano yoyote yanayokuja mbele yake. Huku akiwataka vijana wenzake kuwa tayari kujaribu na siyo kuogopa na kudhani kuna watu maalum watashiriki masuala mbalimbali.

Anasema hata siku moja hakuwahi kutegemea kazi ya mikono yake kutumika katika jengo kub- wa kama hilo ambalo linatambulika ndani na nje ya nchi huku likibeba heshima ya jina la Baba wa Taifa. Anasema yeye na pacha wake ni watoto wa mwisho kati ya saba wa baba na mama Chandoma, wa kike wanne na wa kiume watatu.

Anasema familia hiyo inaishi Boko jijini Dar es Salaam huku pacha wake akimaliza Diploma ya masuala ya Masoko na kufanya kazi katika Kampuni ya Samsung. Anasema amesoma Shule ya Msingi Mwenge huku Kidato cha kwanza hadi cha nne akisoma Shule ya Sekondari ya Dar es Salaam.

Anasema baadaye kidato cha tano na sita alisoma Sekondari ya Makongo na kuchukua masomo ya HGE (Historia, Jiografia na Uchumi) kisha baadaye kujiunga na IFM. Akimzungumzia Abdallah, mama yake mzazi Lulua Chandoma anasema tangu akiwa mtoto mwanawe huyo alipenda kuchora mara kwa mara kiasi ambacho kuta zote za nyumba na geti zilijaa michoro tofauti ya ubunifu.

Anasema familia imepata furaha ya ajabu na kumtaka ajiendeleze zaidi na wao kuendelea kumpa ushirikiano kwani katika shindano hilo alipeleka nembo mbili na baba yake alimchagulia ile aliyoshinda. Naye Meneja wa Ukumbi huo, Deus Kulwa anataja sifa za nembo iliyoshinda kuwa ni na alama ya jengo lenyewe, rangi ya dhahabu inayoonesha hadhi ya jengo hilo kuwa ni dhahabu.

Pili ni rangi ya bluu inayoonesha jengo lipo Pwani karibu na bahari, anga ya dunia na mnazi ambao ni alama ya zao la Pwani. Akizungumza kwa niaba ya Kampuni yao, Mmuni anasema suala hilo ni la kujivunia na itatumika kutangaza kampuni hiyo ya vijana wadogo ambao wamethubutu kwa nia ya kujiajiri.

Akizungumza wakati wa kuzindua nembo hiyo, Membe alisema kupitia kituo hicho Serikali imejiandaa kuleta ulimwengu Tanzania na nembo hiyo iwe chachu ya Watanzania wote kutumia kituo hicho kwa mikutano mbalimbali, sherehe na hata zile za kijamii kama harusi.
“Ni vema Watanzania wote kuleta mikutano ya taasisi, kampuni za kimataifa na hata sherehe mbalimbali ili kumuenzi Baba wa Taifa kwa kutumia kituo hicho ambacho ni kitega uchumi cha Serikali,” anasema Membe. Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa AICC, Elishilia Kaaya anasema katika mchakato wa kupata nembo hiyo ilishirikisha Watanzania kwa kutumia vyombo vya habari ambapo walishiriki Watanzania 272 waliowasilisha nembo za ubunifu 352.

Alisema nembo iliyoshinda ilionesha sura na mandhari ya kituo kilipo huku wakiwa na mikakati ya kujenga vituo vingine kama hivyo Zanzibar na Iringa ambacho kitawezesha ukanda wa Kusini kuwa na utalii wa mikutano. Alisema kituo hicho kimekabidhiwa rasmi kwa uongozi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) ili kukisimamia na uongozi huo umedhamiria kituo hicho kutofunikwa na kivuli cha AICC kwa kukipatia nembo yake stahili.

Kituo hicho kilizinduliwa Machi mwaka jana na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping, alipokuwa katika ziara yake ya kiserikali ya siku mbili nchini. Jengo hilo limejengwa na Serikali China, ujenzi wake umegharimu dola za Marekani milioni 29.7 (Sh bilioni 47.5) likiwa na uwezo kuhodhi Mikutano minne kwa mara moja, yenye idadi ya watu 1,600.

Kituo hicho cha mikutano kipo kitalu namba 10 katika makutano ya barabara za Garden na Shaaban Robert kikiwa kimejengwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya China. Kazi za kituo hicho ni kuendesha mikutano, kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini kupitia mikutano na kuangalia na kutunza majengo ya kituo hiki.

Katika kuendesha mikutano, kituo kina jumla ya kumbi 16 ambapo ukumbi mkubwa kabisa una uwezo wa kuchukua hadi watu 1,003; kumbi za ukubwa wa kati zenye uwezo kuchukua kati ya watu 150 mpaka watu 300, na kumbi zingine ndogo 11 zenye uwezo wa kuchukua hadi watu 50 kila moja.
Pia Kituo kina kumbi kwa ajili ya sherehe mbalimbali kama harusi na shughuli za burudani likiwepo eneo la juu la wazi na Lobby tatu ambazo hutumika kwa ajili ya Mchapalo na wakati mwingine kwa ajili ya maonesho. Kumbi zote za mikutano katika Kituo cha JNICC zimefungwa vifaa mbalimbali vya kisasa vinavyosaidia kuwezesha mikutano kwenda vizuri.Chanzo Habari Leo

No comments:

Post a Comment