Wafanyabiashara Mwika walalamikia ushuru magari
Moshi. Wafanyabiashara wa mazao ya ndizi na
maparachichi katika Soko la Mwika lililopo Wilaya ya Moshi mkoani
Kilimanjaro wamelalamikia ongezeko la ushuru wa magari makubwa katika
soko hilo.
Hali hiyo imesababisha wenye magari kuhamisha
magari yao na kuyapeleka Soko la Mamsera wilayani Rombo na kuwaacha
wananchi wa Mwika wakishindwa kuuza bidhaa zao.
Wafanyabiashara hao walikuwa wakiuza bidhaa hizo
kwa wafanyabiashara wakubwa wa jijini Dar es Salaam, Kenya na mikoa ya
jirani, lakini kwa sasa bidhaa hizo haziuziki baada ya wafanyabiashara
wakubwa kukimbia ushuru ulioongezwa na wakala kutoka Sh 40,000 hadi Sh
60,000
Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Dk. Agustino Mrema
alikiri kupokea malalamiko hayo na tayari amewasiliana na mkurugenzi wa
halmashauri hiyo kufuatilia malalamiko.
Mrema alimuomba mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi
kuingilia kati na kukaa na wakala pamoja na wafanyabiashara, ili
kutoharibu biashara katika soko la kimataifa ambalo linawaleta
wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya
Moshi, Fulgence Mponji hakuweza kupatikana kuzungumzia malalamiko hayo.
baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana.
No comments:
Post a Comment