Mvua zaleta maafa makubwa Dar, mikoani
Mkazi wa Kijiji cha Bulembo mkoani Kagera, Godena Joseph akitafakari
baada ya shamba lake la migomba kuharibiwa na mvua iliyoambatana na
upepo. Picha na Issa Ibrahim.
ar/Pwani/Kagera. Mvua zilizonyesha maeneo
mbalimbali nchini tangu wiki iliyopita, zimesababisha maafa, uharibifu
wa mali, miundombinu na kuacha zaidi ya familia 150 bila makazi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa
athari za kifamilia zimeukumba zaidi Mkoa wa Kagera ambako familia
zaidi ya 125 zinahitaji msaada baada ya nyumba zao kuezuliwa paa na
mashamba ya migomba kuharibiwa.
Ingawa maeneo mengi ya nchi yameathirika, hali
inaonekana ni ya kiwango cha juu zaidi katika mikoa ya Dar es Salaam,
Bukoba, Lindi na Mtwara.
Jijini Dar es Salaam, maeneo kadhaa yamejaa maji
na hata kusababisha watu kuyakimbia makazi yao kama vile Jangwani, Bonde
la Mto Msimbazi na Mbweni ambako Serikali ilipima viwanja na kuvigawa
kwa wananchi.
Mkoani Kagera, maeneo yaliyoathirika zaidi ni ya vijiji vya Bulembo, Kata ya Kamachumu wilayani Muleba.
Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage
alisema: “Hali siyo nzuri na timu ya watalaamu ipo eneo la tukio ili
kufanya tathmini zaidi kuhusu kadhia hiyo.
“Watu wa Msalaba Mwekundu wanajaribu kurejesha paa upya katika baadhi ya nyumba zilizoezuliwa.”
Mkazi wa Kijiji cha Bulembo, Richard Kichabeba
alisema familia zilizokumbwa na tatizo la nyumba zao kuezuliwa paa,
zinaishi nje na mbaya zaidi nyumba zinazidi kuporomoka kutokana na mvua
zinazoendelea kunyesha.
“Hakuna muhogo wala mgomba. Mawe na upepo
vimevuruga kila kitu,” alisema mkazi huyo na kuongeza kuwa mbaya zaidi
hata hizo paa zao hazijulikani zimeangukia wapi.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi alisema
kuwa uongozi wa wilaya hiyo umelazimika kuifunga kwa muda usiojulikana
Barabara ya Msata – Bagamoyo baada ya maji kuifunika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Halima
Kihemba alisema kuwa hivi sasa Kata mbili za Ruvu na Kwala hazifikiki
baada ya madaraja kubomoka.
Alisema kuwa madaraja mawili ya Mto Ndwati na Msua
yamefurika maji hali iliyosababisha mafuriko makubwa, hivyo aliwataka
wakazi wa vijiji hivyo kuchukua tahadhari.
No comments:
Post a Comment