Wednesday, 26 February 2014

Miili 5 yapatikana mgodini A. Kusini

 

Wachimba migodi waliookolewa wiki jana wanakabiliwa na kesi mahakamani
Miili ya wachimba migodi haramu watano, imepatikana karibu na mgodi ambao ulikuwa hautumiki nchini Afrika Kusini.
Miili ya wanaume wanne na mwanamke mmoja ilipatikana karibu na mgodi huo katika eneo la Roodepoort, Magharibi mwa Johannesburg.
Vifo vyao vimetokea wiki moja baada ya shughuli kubwa ya uokozi wa zaidi ya wachimba migodi 20 haramu waliokuwa wamekwama ndani ya mgodi Mashariki mwa Johannesburg.
Walikamatwa baada ya kuokolewa na sasa wanakabiliwa na kosa la uchimbaji haramu wa migodi.
Afrika Kusini hupoteza mamilioni ya dola katika shughuli za uchimbaji haramu wa madini kila mwaka.
Ardhi inayozingira mji wa Johannesburg ina migodi mingi ambayo haitumiki na ambayo huvutia wachimba migodi haramu kutoka katika eneo hilo na nchi jirani za ,Lesotho, Msumbiji na Zimbabwe.
Mvuto wake hasa huwa ni kwamba zinaweza kuwa na madini ya dhahabu.
Wakati nyingi ya migodi hizo hazina faida za kifedha, bado zina mabaki ya dhahabu kiasi cha kuwavutia watu wengi wasio na ajira.
Waokozi wanasema kuwa bado huenda kuna wachimba migodi haramu zaidi ndani ya migodi hiyo.

 

Uganda yahofia kunyimwa misaada

Waziri wa mambo ya nje nchini Uganda, Sam Kutesa amesema ana wasiwasi kuwa Marekani huenda ikasitisha msaada wake kwa taifa hilo baada ya Rais Yoweri Museveni kuidhinisha sheria dhidi ya ushoga nchini humo.

 

Bwana Kutesa amesema kuwa watu sharti wawe na maadili na kukubali msaada.
Balozi wa Marekani nchini Uganda Scott DeLisi, awali aliitaka serikali ya Uganda, kubatilisha sheria hiyo.
Alisema alihitaji kufafanuliwa zaidi sheria hiyo, kabla ya Marekani kujua ikiwa itaendelea na mipango yake ya misaada kwa nchi hiyo hasa miradi ya kupambana dhidi ya HIV na Ukimwi..
Sheria hiyo mpya, inatoa adhabu kali kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na kupiga marufuku kile inachosema kusambaza vitendo vya ushoga.


Asasi za DRC zataka el Bashir ashikwe.

Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, DRC, yamesema kuwa Serikali ya nchi hiyo itachukuliwa kuwa dhaifu iwapo hamkamati Rais wa Sudan, Omar el Bashir.

 

Rais wa Sudan Omar el bashir

Mashirika yapatayo 90 yalitoa wito Serikali ya DRC imkamate el Bashir ambaye alikuwa mjini Kinshasa kushiriki katika vikao vya muungano wa COMESA.
Mmoja wa waandalizi wa maandamano ya kushinikiza Serikali imkamate kiongozi huyo wa Khartoum, Bwana Andre Kito Masimango, amesema:
"kuna barua ambayo inasema kuwa mahali po pote ambapo El Bashiri anapatikana anapaswa kukamatwa na kupelekwa kwenye mahakama ya kimataifa."
Mkerektwa huyo wa haki za kibinadamu anasema kuwa Rais El Bashir anapaswa kukamatwa kwa heshina ya waathirika wa dhuluma inayodaiwa kufanywa nchini Sudan na hata DRC yenyewe.
Watu kadhaa ambao wametoa maoni kwenye mtandao wa BBC wamesema kuwa lilikuwa kosa kwa Serikali ya DRC kumkaribisha Rais El Bashar kwa mkutano wa COMESA huku ikijua kuwa anatafutwa.
Hata hivyo kuna wale wanaosema kuwa msimamo wa Umoja wa Afrika (AU) ambao unasema kiongozi anayetawala hapaswi kukamatwa unapaswa kuzingatiwa ili El Bashir asikamatwe ugenini DRC.

 

Marekani yaonya Urusi kutoivamia Ukraine



 Marekani imeionya serikali ya Moscow isithubutu kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Ukraine.
Hatua hii inawadia siku moja tu baada ya Urusi kuamuru kufanyika kwa mazoezi ya kijeshi yanayoshirikisha askari wapiganaji laki moja na nusu kwenye mpaka wake na Ukraine .
Kujitokeza kwa wanajeshi wa Urusi kwenye mpaka na Ukraine kumeimarisha uhasama ulioko kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, John Kerry amesema kuwa Urusi inapaswa kukubali ushauri ya kwamba mataifa ya kigeni yasiingile mambo ya ndani ya Ukraine.
Alisema kuwa kujiingiza kijeshi katika hali ilivyo nchini Ukraine kwa hivi sasa ni kosa kubwa.
Mawaziri wa ulinzi kutoka mataifa ya muungano wa NATO wametoa taarifa ambapo wamesema kuwa wanachama wake wataendelea kuunga mkono uhuru na hadhi ya taifa la Ukraine.
Serikali ya Marekani imesema kuwa imetenga mbinu mbalimbali inazotazamia kutumia kuimarisha Ukraine kiuchumi, huku kukiendelea kuwa na hofu kuwa huenda taifa hilo likashindwa kuendelea kulipa madeni yake.
Kwa wakati huu msaada wa kijeshi pekee kwa Ukraine hautoshi kwani taifa linalotaka kusaidia lazima kwanza liimarishe hali ya kukubaliwa kwake katika taifa hili ambalo limegawanyika kwa imani yake kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi.
Wabunge kadhaa wa Marekani wameonya kuwa Jumuiya ya Ulaya na Marekani wasipotoa msaada wa pesa taslimu Urusi huenda ikafanya hivyo.

 

 

Tuesday, 25 February 2014

Wasiwasi wa Ukraine kusambaratika

Rais wa mpito wa Ukraine, Olexander Turchynov, ameonya kuhusu tisho la kusambatarika kwa nchi hiyo kufuatia kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa Rais,

 

 

 

 

 

 

 

Rais wa mpito Olexander Turchynov asema tangazo litatolewa Alhamisi

Viktor Yanukovych.
Matamshi yake yanakuja wakati ambapo upinzani ukitokota katika maeneo ya Ukraine ambapo Kirusi kinazungumzwa dhidi ya serikali ya mpito.
Bunge la Ukraine limechelewa kuiunda serikali ya mseto.
Tangazo lilitarajiwa siku ya Jumanne kufuatia kung'atuliwa mamlakani aliyekuwa Rais Viktor Yanukovych, lakini Rais wa mpito Olexander Turchynov, amesema kuwa litatolewa siku ya Alhamisi ili kuruhusu mashauriano kuendelea.
Turchynov ameelezea wasiwasi wake kwa kile alichokitaja kama hatari ya kugawanyika kwa baadhi ya maeneo nchini Ukraine.
Kumetolewa waranti ya kukamatwa Yanukovych kwa madai ya kuhusika na mauaji ya waandamanaji, lakini hajulikani aliko.
Wanadiplomasia wakuu wa Umoja wa Ulaya wanakutana katika mji mkuu Kiev kujadili usaidizi wa kifedha kwa serikali ya mpito, huku nchi hiyo ikitishiwa na mdororo wa kiuchumi kufuatia maandamano ya miezi mitatu.
Jumuiya ya Kimataifa
Kumekuwa na wasiwasi katika jumuiya ya kimataifa kuwa huenda Ukraine ikagawanyika mara mbili; upande mmoja ukiwa karibu na Umoja wa Ulaya, na mwingine ukiegemea upande wa Urusi.
 
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza, William Hague, anasafiri kwenda Washington-Marekani, kulijadili suala hili.
Katika taarifa aliyoitoa bungeni, alisema kuwa Ukraine inahitaji msaada wa dharura wa fedha wa kimataifa ili kuimarisha uchumi wake unaozorota.
Ingawa kumekuwa na msimamo mkali kutoka kwa Urusi, Hague, amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa Umoja wa Ulaya na Urusi kufanya kazi pamoja.
Hague alisema, 'Azimio letu kuu ni kuendeleza demokrasia, kutetea haki za kibinaadam, na kufuatwa kwa sheria nchini Ukraine.
Hii sio kuhusu uamuzi wa Ukraine kuchagua kati ya Umoja wa Ulaya ama Urusi. Ni kuhusu kuielekeza nchi hiyo katika njia ya kidemokrasia katika siku zijazo'.

Wanamgambo waua wanafunzi Nigeria

Wanamgambo wa Kiislam wa kundi la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria wametuhumiwa kushambulia shule moja na kuwaua wanafunzi kadhaa.
Polisi nchini Nigeria wameliambia Shirika la Habari la Uingereza, Reuters kwamba wote waliouawa ni wavulana na kwamba baadhi ya miili ya wanafunzi hao imeungua na kubaki majivu.
\
Taarifa ya jeshi la Nigeria imesema shambulio hilo limefanyika katika jimbo la Yobe.
Wakaazi wa mji wa Buni Yadi katika jimbo hilo, wamesema washambuliaji hao walivamia usiku na kuwachinja baadhi ya wanafunzi.
Wamesema baadhi waliuawa kwa kupigwa risasi.
Walimu katika chuo cha serikali ya shirikisho katika mji wa Buni Yadi wameliambia shirika la habari la AP kwamba wanafunzi wapatao 40 waliuawa katika shambulio hilo ambalo lilianza mapema Jumanne asubuhi.
Jeshi limethibitisha kwamba shambulio hilo limetokea katika hosteli za wanafunzi lakini limesema haliwezi kutoa taarifa zaidi kwa sasa.
Kundi la Boko Haram limekuwa likishutumiwa kuendesha vitendo vya mauaji kaskazini mwa Nigeria, yakiwemo mauaji ya mapema mwezi huu katika jimbo la Yobe.
Boko Haram, lina maana ya"Elimu ya Magharibi ni dhambi" katika lugha ya Kihausa, mara kwa mara limekuwa likishambulia shule katika siku za nyuma.
Watu kadhaa wameuawa katika mashambulio mawili yaliyotokea wiki iliyopita. Katika tukio moja, wanamgambo hao wa Boko Haram, waliteketeza kijiji kizima na kuwapiga risasi wakaazi wa eneo hilo waliokuwa wakijaribu kutoroka.

Msaada wa Marekani kwa Uganda

   

John Kerry asema Uganda inakiuka haki za binaadamu

Marekani haikufurahishwa na hatua ya Uganda kuidhinisha sheria dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.
Waziri wa mashauri ya Kigeni wa Marekani, John Kerry amesema tangu Uganda iidhinishe mswada huo miaka minne iliyopita, Marekani ilieleza wazi kwamba sheria hiyo inakiuka jukumu la kuhakikisha kuwepo haki za binaadamu ambalo tume ya haki za binaadamu Uganda inatambua linaambatana na sheria ya Uganda.
Kerry amesema,' Baada ya kuidhinishwa sheria hii, tunaanza ukaguzi wa ndani wa uhusiano wetu na serikali ya Uganda, kuhakikisha kwamba pande zote za uhusiano wetu, ukiwemo miradi ya msaada, zinapinga sera na sheria zinazowaonea watu na tuwe na uhusiano unaodhihirisha maadili yetu'.

Tamko hilo limetolewa siku moja baada ya rais Yoweri Museveni kukaidi shinikizo la kimataifa na kutia saini sheria hiyo iliyo zusha mzozo, inayoharamisha mapenzi ya jinsia moja Uganda, hatua iliyozusha hisia kali.
Baadhi ya mataifa ya magharibi tayari yanatishia kukatiza msaada wa moja kwa moja kwa serikali ya Uganda.

Marekani inasema kuidhinishwa kwa sheria hiyo kunatishia hatari ya kurudi nyuma katika uwajibikaji wa Uganda kulinda haki za raia wake na kutishia jamii ya wapenzi wa jinsia moja Uganda.