TANZANIA KUPELEKA MAJESHI SUDAN KUSINI
Serikali
inatarajia kupeleka kikosi kimoja cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) huko Sudan Kusini kwa ajili ya kulinda amani kutokana na vita ya
wenyewe kwa wenyewe inayoendelea.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe anasema Dar
es Salaam jana kwamba Serikali imekubali kupeleka batalioni moja baada
ya kuombwa na Umoja wa Mataifa (UN).
Sudan ya Kusini imekuwa katika machafuko ambayo yamesababisha vifo vya mamia ya raia na wengine kujeruhiwa.
"Tumefanya
uamuzi wa kupeleka majeshi yetu Sudan Kusini, tumefanya hivyo baada ya
kuombwa na Umoja wa Mataifa kwa sababu ya ubora wa jeshi letu," Membe
aliwaambia waandishi wa habari.
Anasema
jukumu la kulinda amani katika Bara la Afrika ni la Waafrika wenyewe
na kwamba Tanzania inajiona kwamba ina jukumu la kusaidia kupatikana
kwa amani.
Anasema
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon alimwomba Rais Jakaya
Kikwete kusaidia kupeleka majeshi yake Sudan Kusini kusaidia kulinda
amani. "Rais alikubali, sasa tuko kwenye maandalizi, nadhani Aprili
jeshi letu litaondoka kuelekea Sudan Kusini," alisema Membe.
Kwa sasa Tanzania ina vikosi vya wanajeshi wa kulinda amani katika nchi za DRC, Darfur (Sudan) na Lebanon. Chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment