Askofu Mtetemela awatuliza wananchi
Dodoma. Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania,
Donald Mtetemela amewahakikishia Watanzania kuwa Katiba itapatikana kwa
wakati.
Hata hivyo, amesema kuna haja kwa Watanzania wa
dini zote kuliombea Bunge Maalumu la Katiba lifanye mambo kwa
kumshirikisha Mwenyezi Mungu ili mchakato wa Katiba uende vizuri.
Askofu Mtetemela, ambaye ni mmoja wa mjumbe wa Bunge hilo, alitoa ushauri huo jana kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Alisema kuyumba kwa Bunge la Katiba kwa sasa
kunatokana na misimamo ya vyama vya siasa na kwamba kitendo hicho
kimesababisha kuchelewa kwa kazi ya msingi.
“Mambo ya misimamo hayawezi kuzuilika na wala si
kosa kila kikundi kuwa na msimamo wake, lakini kinachotakiwa ni wajumbe
kufuta mambo ya vyama vichwani mwao na hasa pale panapokuwa na hoja ya
msingi,” alisema kiongozi huyo wa kiroho.
“Watanzania waendelee kutuombea kwa nguvu zote.
Sina shaka tutatoka hapa tukiwa wamoja kwa sababu tunaimba wimbo mmoja
wa kutaka kitu kizuri mbele yetu,” alisisitiza Askofu Mtetemela.
Askofu Mtetemela alisema kuwa katika hatua za
awali kulikuwa na misukosuko mikubwa ndani ya Bunge, lakini sasa kuna
mwelekeo wa kuridhisha kutokana na wajumbe kuelewa wajibu wao katika
mchakato huu.
No comments:
Post a Comment