Bunge Maalumu la Katiba sasa vululu vululu
Dodoma. Matarajio ya Bunge Maalumu la Katiba
kukamilisha kanuni kwa maridhiano yaliyeyuka tena jana huku mambo ndani
ya ukumbi yakionekana kuwa vululuvululu kwa baadhi ya wajumbe kuzungumza
nje ya utaratibu na wengine kurushiana vijembe.
Baadhi ya wajumbe waliamua kutoleana lugha chafu
na kuweka kando hoja za msingi zinazowafanya watofautiane na
kuchelewesha kazi ya kuandika Katiba Mpya.
Hali ilichafuka mchana wakati wajumbe walipokutana
kupitisha kanuni baada ya mmoja wao, Felix Mkosamali kuomba mwongozo
kwa Mwenyekiti wa muda, Pandu Ameir Kificho. Hata hivyo, Kificho
alimtaka kukaa chini kwa muda kwa maelezo kuwa wajumbe waliofika katika
kikao hicho walikuwa wachache, hivyo mwongozo wake kama ulikuwa
unahitaji majibu ingekuwa vigumu kutolewa.
Baada ya muda alisimama, James Mbatia na kuomba
mwongozo, akihoji sababu za kutaka kuanza kikao cha kupitisha kanuni
hizo wakati wajumbe hawajapewa vitabu vya rasimu ya kanuni zenyewe.
“Mwenyekiti ulitangaza asubuhi kuwa tutagawiwa
kanuni kabla ya saa tisa lakini hadi sasa tunataka kusomewa kanuni
wakati hatujagawiwa kanuni hizo,” alihoji Mbatia.
Kificho alitoa ufafanuzi kuwa kanuni hizo zilikuwa
bado zinadurufiwa na kuwataka wajumbe wawe na nidhamu kwani
anapotangaza wanapiga kelele.
Ghafla alisimama Mkosamali tena na kuwasha kipaza
sauti na kuhoji kitendo cha mwenyekiti huyo kumpa Mbatia nafasi ya kutoa
mwongozo wakati yeye amenyimwa... “Mwenyekiti hivi unaongozaje kikao,
inakuwaje mimi nikuombe mwongozo uninyime na mwenzangu umpe? Mwenyekiti
nakuheshimu sana, lakini sijui unatumia kanuni ipi kutoa nafasi kwa
mjumbe wakati mimi ulinizuia nisiseme,” alihoji Mkosamali.
Baada ya kauli hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Hawa Ghasia aliwasha kipaza sauti na kwa sauti ya juu
alisema “Mtoto mdogo hana adabu.” Kauli hiyo iliibua hasira za Mjumbe
mwingine, Moses Machali ambaye naye aliwasha kipaza sauti na kumjibu:
“Kubwa jinga halina adabu,” kauli iliyoibua miguno ndani ya Bunge.
Hata hivyo, licha ya Mwenyekiti kutoa onyo kwa
kauli hizo kwamba hazifai, Mkosamali alisimama katika sehemu yake na
kusema kuwa hakuna mtoto mdogo na kwamba tangu lini mtoto aliishinda
CCM.
Chanzo cha tatizo
Chanzo cha mvurugano huo ambao wiki iliyopita
kidogo usababishe ngumi kurushwa bungeni, ni mfumo wa upigaji kura
katika kupitisha ibara za rasimu, ambao jana uliendelea kuwagawa wajumbe
na kufanya ukumbi huo kuonekana kama eneo la mzaha.
Kauli za ‘ndiyoooo’, ‘hapanaaaa’ na vitendo vya
kugonga meza viliongezeka katika kipindi cha asubuhi baada ya Mwenyekiti
wa Kamati ya Kuandaa Kanuni, Profesa Costa Mahalu kuwaleza wajumbe kuwa
kamati yake haijafikia mwafaka wa ama iwe kura za siri au wazi na
kwamba suala hilo limerejeshwa kwa wajumbe wenyewe.
No comments:
Post a Comment