Monday, 24 February 2014

Ajali mbaya Yatokea eneo la Mikese, Morogoro, leo Asubuhi

 

 

Ankle habari. Leo asubuhi eneo la Mikese, Morogoro, tumekutana na na ajali  mbaya sana ya magari mawili, moja la mafuta, kugongana uso kwa uso na kutumbukia mtaroni na yote kushika moto. Inasadikiwa mtu mmoja ambaye ni dereva wa magari hayo kateketea kabisa kwa moto. 


 

Hakuna cha kufanyika kutokana na moto mkubwa na moshi mwingi wakati magari hayo yakiteketea

 

 

Mlipuko mkubwa wakati matenki ya mafuta yakilipuka

Askari wa kikosi cha zimamoto wakijaribu kuuzima moto huo.Picha na Mdau Sixmund

TANZANIA KUPELEKA MAJESHI SUDAN KUSINI 

 Mzinga 3c649

Serikali inatarajia kupeleka kikosi kimoja cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Sudan Kusini kwa ajili ya kulinda amani kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe anasema Dar es Salaam jana kwamba Serikali imekubali kupeleka batalioni moja baada ya kuombwa na Umoja wa Mataifa (UN).
Sudan ya Kusini imekuwa katika machafuko ambayo yamesababisha vifo vya mamia ya raia na wengine kujeruhiwa.
"Tumefanya uamuzi wa kupeleka majeshi yetu Sudan Kusini, tumefanya hivyo baada ya kuombwa na Umoja wa Mataifa kwa sababu ya ubora wa jeshi letu," Membe aliwaambia waandishi wa habari.
Anasema jukumu la kulinda amani katika Bara la Afrika ni la Waafrika wenyewe na kwamba Tanzania inajiona kwamba ina jukumu la kusaidia kupatikana kwa amani.
Anasema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon alimwomba Rais Jakaya Kikwete kusaidia kupeleka majeshi yake Sudan Kusini kusaidia kulinda amani. "Rais alikubali, sasa tuko kwenye maandalizi, nadhani Aprili jeshi letu litaondoka kuelekea Sudan Kusini," alisema Membe.

Kwa sasa Tanzania ina vikosi vya wanajeshi wa kulinda amani katika nchi za DRC, Darfur (Sudan) na Lebanon. Chanzo: mwananchi


MKUU WA MKOA WA NJOMBE ACHEFULIWA NA VYOO VYA MAKETE 

 

Tabia ya wakazi wengi wa wilaya ya Makete mkoani Njombe kujenga vyoo vidogo kiasi cha watumiaji kupata shida kuingia kujisaidia, imemchefua mkuu wa mkoa huo wakati alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo hivi karibuni

Akizungumza wilayani hapa mkuu wa mkoa wa Njombe Kapt. Aseri Msangi amesema anakerwa na tabia ya wananchi wa makete wanaojenga vyoo vidogo hali inayosababisha kero kwa watumiaji kutokana na kupata shida tangu anapoingia hadi kutoka

 Mimi nashangaa kabisa badala ya mtu kujenga choo kikubwa kitakachopelekea mtu kujisikia nafuu anapoingia kujisaidia nyie mnajenga choo ambacho mtu akiingia kwanza anainama, na pili hawezi kugeuka akiingia, yaani akiingia kwa mbele anarudi kinyume nyume" alisema Msangi


Ametoa wito kwa wananchi hao kujenga vyoo vikubwa na vyenye ubora kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza magonjwa ya matumbo ambayo yanawakumba wananchi wengi na uchunguzi kubaini kuwa ni kutokana na kukosekana kwa vyoo bora vinavyotunzwa vizuri

Taswira,Bomoabomoa Inayoendelea Jiji la Arusha

 

 

 

 

Halmashauri aya Jiji la Arusha imevunja nyumba zake338 baada ya kushinda kesi iliyofunguliwa na wapangaji Sangito Sumari na wenzake 216 katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha.

Operesheni hiyo inayojulikana kama “Operesheni Mongela”ilianza saa 12 asubuhi jana kwa kuvunja nyumba 56 eneo la Kilombero, nyumba 198 eneo la Kaloleni na nyumba 84 katika eneo la Themi.

Wengi walitegemea kuibuka vurugu wakati wa uvunjaji nyumba lakini hadi mchana hapakuwa na pingamizi kwa wapangaji badala yake wenyewe walihamisha vitu vyao mapema jana asubuhi kabla ya zoezi la kuvunja kuanza.

Hata hivyo kuvunjwa kwa nyumba hizo kumeleta neema kwa baadhi ya watu wakiwamo vijana wanaokusanya vyuma chakavu kuvamia maeneo hayo na kuokota kila aina ya chuma au kitu ambacho waliamini kinaweza kuuzwa na kuwapatia fedha.

Akiwa eneo la Kaloleni baada ya kukamiliza kuvunjwa nyumba za Kilombero, Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mongela alisema, ‘Operesheni Mongela’ ilipata baraka zote za viongozi wa Serikali wanasiasa wakiwamo madiwani wote Mbunge na Meya wa Jiji.

 

Friday, 21 February 2014

Ukraine:Hatimaye makubaliano yapatikana

 

Habari za hivi punde zinaarifu kuwa ofisi ya rais Yanukovych nchini Ukrain imetoa taarifa inayosema kwamba mwafaka umefikiwa katika mazungumzo ya usiku kucha kati ya serikali, upinzani na waakilishi wa Muungano wa Ulaya na Urusi.
Taarifa hiyo hata hivyo haikutoa maelezo zaidi kuhusu makubaliano hayo ingawa ilisema kuwa pande zote zitatia saini makubaliano yenyewe.
Duru zinasema kuwa Rais Yanukovych amekuwa akikabiliwa na shinikizo apange uchaguzi wa mapema pamoja na mageuzi ya kikatiba.
Umoja wa Ulaya umekubali kuwawekea vikwazo viongozi waliopanga ghasia zinazoikabili Ukraine kwa sasa.
Uamuzi huo uliofanyika mjini Brussels, Ubelgiji umejiri baada ya watu kadhaa kuuawa mjini Kiev, katika siku ambayo ilishuhudia umwagikaji mkubwa zaidi wa damu tangu uhuru wa Ukraine zaidi ya miaka ishirini iliyopita.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Italia, Emma Bonino, amesema vikwazo hivyo vinavyojumuisha vya usafiri na kupiga tanji mali za wahusika na kwamba vinawalenga wale waliohusika na mauaji ya waandamanaji.
Ujumbe wa Umoja wa Ulaya mjini Kiev unajaribu kuwapatanisha viongozi wa upinzani na rais Victor Yanukovych ili kuleta amani na pia kushawishi taifa hilo kuandaa mapema uchaguzi uliopangiwa kufanyika mwaka ujao.
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Ban Ki-moon amesema hali nchini Ukraine ni ya kutamausha:
Wito huo umetolewa vile vile na waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry ambaye ametaka vurugu kusitishwa nchini Ukraine akisema kuwa watu wa taifa hilo wanastahili kuwa na hali bora kuliko kile alichokitaja kuwa maafa na mateso yasiyofaa ambayo yameshuhudiwa katika barabara za mji mkuu, Kiev.
Haijabainika ni watu wangapi waliouwawa katika vurugu za Alhamisi lakini wizara ya Afya inasema tangu Jumanne, watu sabini wameuawa na zaidi ya 570 wamejeruhiwa.

 

Ghana yatoa heshima kwa Komla Dumor

 

Komla na aliyekuwa waziri mkuu wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai

Hafla mabli mbali za siku tatu kumuenzi aliyekuwa mtangazaji wa BBC Komla Dumor-aliyefariki ghafla mwezi uliopita akiwa na umri wa miaka 41,zitaanza leo nchini Ghana kabla ya maizko yake.
Baada ya kifo chake,rambirambi zilitolewa kutoka kote dunia na rais wa Ghana,John Mahama,alisema kuwa Ghana imempoteza balozi.




Kama ilivyo desturi nchini Ghana,hafla ya mazishi yake itachukua muda wa siku tatu ikianza na misa ya kuomboleza katika kanisa la Accra Roman Catholic cathedral ambapo wananchi wataruhusiwa kutazama mwili wake.

Umati mkubwa unatarajiwa kuhudhuria.
Jumamosi,wasifu wake utasomwa ukisifia yale aliyofanya nchini mwake. Ibada hiyo itafanyika katika uwanja wa Ikulu ya Ghana Ikifuatwa na ibada ya mazishi itakayohusisha familia yake pekee.
Komla Dumor alikuwa mtangazaji maarufu katika stesheni moja ya redio nchi Ghana kabla ya kujiunga na BBC miaka saba iliyopita na aliweza kufahamika kama mtangazaji wa redio na televisheni mwenye haiba kubwa duniani kote.
Katika kazi yake alipenda kuonyesha watazamaji wake kuhusu bara la Afrika na kuwawezesha kuelewa Afrika kwa kina. Kufuatia kifo chake,aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa,Kofi Annan alisema kuwa Afrika imempoteza mmoja wa talanta zake chipukizi.
Aliongeza kwamba, Komla Dumor alikuwa mtangazaji mwenye kupeana motisha aliyedhamiria kuchimbua ukweli na kutangaza ukweli kila wakati.
Maneno haya yalilingana na yale yaliyotolewa na wabunge wa Ghana siku ya Alhamisi. Katika ibada hiyo,mbunge mmoja alitaja kuwa serikali ilikuwa imekubali kuipa jina barabara moja jijini kama ishara ya kumkumbuka.

 

Ikulu ya Rais Somalia yashambuliwa

 

 

Wapiganaji wa kundi la wanamgambo la Al Shabaab nchini Somalia meshambulia Ikulu ya Rais katika mji mkuu Mogadishu.
Umoja wa mataifa unasema umefahamishwa kuwa rais wa nchi hiyo hakujeruhiwa na yu salama na kwamba shambulizi la wanamgambo hao lilitibuka.


Waziri wa mambo ya usalama wa nchi hiyo Abdi Karim Hussein, amesema baadhi ya washambuliaji wamefariki na wengine kukamatwa.
Kundi la Al- Shaabab linalopigana na utawala nchini humo limedai kuhusika na shambulio hilo na kusema makabiliano yangali yanaendelea.
Walianza mashambulizi yao, kwa kutumia gari lililokuwa na bomu ndani yake kwa kuliegesha kando ya ukuta na kisha kuanza kupigana ili kuweza kuingia ndani.
Milipuko mikubwa ilisikika pamoja na milio ya risasi.
Majeshi ya muungano wa Afrika yamekuwa yakipambana na wapiganaji hao na hata kuwafurusha kutoka mji mkuu Mogadishu. Hata hivyo bado wanadhibiti sehemu nyingi nje ya Mogadishu