Friday 28 February 2014

Kenya: Wajumbe wa ODM wazua vurugu

Vurugu zimezuka katika uchaguzi wa kuwachagua maafisa wapya wa chama kikuu cha upinzani cha ODM nchini Kenya, chake aliyekuwa waziri mkuu wa taifa hilo Raila Odinga.

 

Bwana Odinga anatarajiwa na wengi kuwa atagombea kiti cha urais 2017

 Polisi waliwasili katika ukumbi wa uwanja wa michezo wa kimataifa wa Kasarani viungani mwa jiji la Nairobi kurejesha utulivu baada ya baadhi ya wafuasi wa chama hicho waliodaiwa kuwa walinda usalama kurusha vita pamoja na masanduku ya kupigia kura wakijaribu kuvuruga uchaguzi huo.

Ugomvi ulizuka baada ya kuzuka madai kuwa kulikuwa na orodha ya wajumbe bandia iliyokuwa ikisambazwa pamoja na makaratasi bandia ya kupigia kura. Mbunge maalum Isaac Mwaura ambaye anaishi na ulemavu wa ngozi-Albino-alionekana akisukwasukwa na wajumbe baada ya kuzua zahama kuhusu madai hayo ya udanganyifu katika zoezi hilo la upigaji kura.
Chama cha ODM ndicho chama kikubwa zaidi cha kisiasa nchini Kenya kikiwa na idadi kubwa ya wabunge katika bunge la kitaifa pamoja na Senate. Chama hicho kimemudu mgao mkubwa zaidi wa pesa za kufadhili shughuli za vyama vya kisiasa kutoka kwa serikali ya Kenya.
Kutokana na raslimali za chama hicho uchaguzi wa leo umeonekana kuzua msisimko mkali pamoja na patashika baina ya wanasiasa mashuhuru ambao wanagombania vyeo mbali mbali.
Bwana Odinga ambaye alishindwa na rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu uliokumbwa na madai ya udanganyifu mwezi Machi mwaka uliopita anatetea kiti chake kama kiongozi wa chama, dalili kwamba huenda akagombea tena kiti cha urais mwaka 2017.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa zoezi la upigaji kura Bwana Odinga alizungumzia maswala mbali mbali yanayohusiana na usalama nchini Kenya pamoja na kuiponda serikali ya mpinzani wake Rais Uhuru Kenyatta kwa kushindwa kuleta suluhu ya matatizo ya kiuchumi yanayowakabili wakenya.

 

No comments:

Post a Comment