Ikulu: Kujadili hotuba ya JK kupoteza muda
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salva Rweyemamu
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mawasiliano ya
Rais Ikulu, Salva Rweyemamu amesema kuendelea kuijadili hotuba ya Rais
Jakaya Kikwete aliyotoa kwenye Bunge la Katiba mwishoni mwa wiki ni
kupoteza muda.
Akizungumza na gazeti hili jana, Rweyemamu
aliushangaa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuendelea kutoa matamko
yanayoipinga hotuba hiyo, akisema haumtendei haki mkuu huyo wa nchi na
Watanzania wote kwa ujumla. Alisema kama Mtanzania, Rais alitoa maoni
yake na amekuwa muungwana kwa kuwaambia kwamba bado wana fursa ya
kujadili na kuleta mapendekezo yao, lakini wajali zaidi masilahi ya
taifa.
“Hiyo ni propaganda isiyokuwa na maana kwa taifa
na hata hatima ya Katiba yenyewe. Ningependa kuwakumbusha kwamba
Watanzania wamewapeleka Dodoma wakajadili Katiba na siyo kufanya
propaganda, tunawataka wafanye kazi,” alisema Rweyemamu.
Kwa mujibu wa Rweyemamu, umoja huo wenye viongozi
kutoka vyama vya upinzani haumtendei haki Rais kwani kama Mtanzania,
mkuu huyo wa nchi ana fursa ya kutoa maoni yake.
“Wasifikiri kwa kumjibu hivyo Rais wanajibizana na
CCM. Rais ni mkuu wa nchi ana maoni yake, lakini zaidi ya yote, Bunge
la Katiba siyo mahali pa kufanya siasa. Kama wanataka siasa tunawaomba
warudi maofisini mwao wakafanye siasa, pale tumewatuma kazi,”
alisisitiza.
Rweyemamu alibainisha kuwa mchakato wa kutunga
Katiba unahitaji busara na busara hiyo haiwezi kupatikana kama watu
waliotumwa kuwawakilisha wananchi wameamua kufanya siasa.
“Tunahitaji watu wote wawe CCM, CUF, Chadema na vyama vingine waache siasa,” alisema.
Wakati huohuo, bungeni Dodoma limeibuka kundi la
wajumbe, wengi wao kutoka CCM wakiipongeza hotuba hiyo ya Rais Jakaya
Kikwete na kuwakosoa watu wanaotishia kumpeleka Rais mahakamani kwa
madai ya kuvunja kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuingilia
mchakato wa maoni.
Mjumbe wa kundi hilo linalojiita Tanzania Kwanza,
Evod Mmanda alisema siyo kweli kuwa Rais amevunja sheria kwani
alihutubia Bunge baada ya kupitishwa kwenye kanuni za Bunge kifungu cha
75(1) ambacho kinaeleza mwenyekiti anaweza kumwalika mgeni rasmi
kulihutubia Bunge.
Walioambatana na Mmanda ni Dk Emmanuel Nchimbi, Said Nkumba, Mohamed Thabit Kombo, Waride Jabu, Seleman Jafo na Charles Mwijage.
No comments:
Post a Comment