Thursday 27 March 2014

Rais akistaafu afutiwe kinga’

 

Dar es Salaam. Wakati Bunge la Katiba likiwa bado halijaanza kujadili Rasimu ya Katiba, taasisi moja ya viongozi wa dini imetoa maoni mapya ikitaka Rais wa nchi awe tu na kinga anapokuwa madarakani, akiondoka awajibike kwa matendo yake.
Mapendekezo hayo yalitolewa Dar es Salaam jana na Baraza la Wadhamini la Taasisi ya Viongozi wa Dini Tanzania (IRCPT), lilipokutana kwa ajili ya kutafakari kwa pamoja juu ya mchakato wa Katiba Mpya.
Mkutano wa Baraza hilo linalojumuisha Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Titus Mdoe, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Musa Salum na Padri John Solomon, uliongozwa na kaulimbiu ya ‘Katiba Moja Kwa Watanzania Wote, Pamoja Tutafika’.
Mwenyekiti wa IRCPT, Jaji Mstaafu Raymond Mwaikasu alisema tafakari inahitajika kuhusu kinga ya Rais na kwamba wao wanapendekeza awe nayo anapokuwa madarakani, lakini kinga hiyo iondolewe anapoachia madaraka, ili awajibishwe pale alipokosea.
Jaji Mwaikasu alisema pamoja na kwamba waliwasilisha maoni kwa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hatua ya sasa inawalenga watu wenye lengo la kuingia Ikulu wakiwa na mawazo ya kujinufaisha wao, ndugu, jamaa na marafiki zao badala ya kuwatumikia wananchi.
“Hili linapaswa kutazamwa kwenye Katiba yetu mpya na sisi hatutakuwa wa kwanza kufanya hivyo, ila itasaidia kuwafanya viongozi kufuata maadili na iwapo itatokea Rais kuvunja Katiba, apelekwe mahakamani na akikutwa na hatia, awajibike hata kwa kujiuzulu,” alisema Jaji Mwaikasu. Naye Sheikh Salum alisema mali zote ni miliki ya Mungu, hivyo zinapaswa kugawanywa kwa usawa na ikitokea mtu akajimilikisha ni jambo lisilokubalika, hivyo ziwepo sheria za kuwabana viongozi wa aina hiyo.
Askofu Mdoe alisema Rasimu ya Katiba ni nzuri ingawa hakuna kitu kinachokamilika kwa asilimia 100, hivyo mazuri yaboreshwe, upungufu usahihishwe na yaliyokosekana yapatiwe fursa.
Alisema malumbano yanayoendelea kwenye Bunge la Katiba hayana tija kwani yana mwelekeo wa masilahi ya kisiasa badala ya masilahi ya umma.
“Wamebadilisha hali waliyotakiwa kuwa nayo, wanarudi katika makundi hasa ya kisiasa na mijadala kuwa ya kichama zaidi, wakifika bungeni wawe wazalendo wajadili na kuacha ushabiki,” alisema Askofu Mdoe.
Muundo wa Muungano
Kuhusu mjadala wa serikali mbili au tatu, Jaji Mwaikasu alisema hauna tija isipokuwa jambo muhimu ni kujenga msingi imara wa kuheshimiwa kwa Katiba itakayopitishwa. “Tunaambiwa Katiba imevunjwa, tunafanya nini? muhimu ni kuangalia viongozi wanaohusika wanadhibitiwa vipi, vinginevyo itakuwa ni bure,” alisema.
Alibainisha kuwa tatizo Bunge la Jamhuri ya Muungano limelala na walioteuliwa kutetea wanatetea mikate yao, hivyo akapendekeza kuwapo haja ya wananchi nao kupewa meno ya kuhakikisha Katiba inalindwa, ili pale itakapothibitika Rais amevunja Katiba wachukue hatua.

 

No comments:

Post a Comment