Saturday 12 April 2014

JINSI MAFURIKO YANAVYOLITESA JIJI LA DAR..ANGALIA PICHA 

Raia wa Guinea Bissau kuchagua rais mpya


Uchaguzi wa urais na maeneo bunge unafanyika katika taifa dogo la afrika magharibi Guinea Bissau.
Ni uchaguzi wa Kwanza tangu kufanyika kwa mapinduzi miaka miwili iliopita -ikiwa ni hatua ya hivi karibuni ya kijeshi ambayo imesaidia kuhakikisha kwamba hakuna raisi aliyechaguliwa ambaye amefanikiwa kuiongoza Guinea Bissau kwa kipindi chote alichochaguliwa tangu taifa hilo lijipatie Uhuru wake kutoka kwa Ureno mnamo mwaka 1974.
Kiongozi wa mapinduzi hayo Antonio Indjai aliikabidhi mamlaka serikali ya raia mnamo mwaka 2012 iliopewa wajibu wa kuandaa Uchaguzi huo.
Indjai alifunguliwa mashtaka nchini marekani kwa madai ya kufanya biashara ya mihadarati pamoja na kuwauzia silaha waasi wa Colombia.Wagombea 13 wanawania wadhfa wa urais.
Iwapo mmoja wao hatashinda kwa wingi wa kura basi uchaguzi huo utaenda kwa awamu ya pili mnamo mwezi May.

Boko Haram ladaiwa kuwaua watu laki moja

Sasa imebainika kuwa wanamgambo wa kiislamu kazkazini mwa Nigeria wamewaua zaidi ya watu laki moja na arubaini na tano katika misururu ya mashambulizi juma lililopita.
Sineta wa jimbo la kazkazini mashariki la Borno Ahmed Zannah ameiambia BBC kwamba mauaji hayo yalifanyika katika maeneo matatu tofauti yaliopo mashambani.
Amesema kuwa taassi moja ya kutoa mafunzo ya elimu ndio iliokuwa ya kwanza kulengwa ambapo wanamgambo hao waliwaua walimu watano kabla ya kuwatekanyara wake zao kadhaa.
Wapiganaji hao wanaoshukiwa kutoka katika kundi la wanamgambo wa Boko haram baadaye walivamia vijiji viwili katika eneo la mashambani karibu na mpaka na Cameroon.

Iran haitabadili balozi wake katika UN

Abutalebi

Makamo wa waziri wa mashauri ya nchi za nje wa Iran amesema nchi yake haifikirii kumteua mtu mwengine kuiwakilisha nchi katika Umoja wa Mataifa.
Taarifa iliyotolewa na Abbas Araqchi imesema Iran itatumia sheria kupinga uamuzi wa Marekani wa kumkatalia visa Hamid Abutalebi kuingia Marekani, ili kuwa mwakilishi mpya wa Iran katika Umoja wa Mataifa mjini New York.
Bwana Abutalebi amehusishwa na kundi lilovamia ubalozi wa Marekani mjini Teheran mwaka wa 1979, na nchini Marekani baadhi ya wanasiasa wamepinga vikali uteuzi wa mwanabalozi huyo.
Marekani haikuwahi kumkatalia visa mwakilishi katika Umoja wa Mataifa, wenye makao yake makuu mjini New York.

Wednesday 9 April 2014

Miyeyusho ayayushwa

Dar es Salaam. Pambano la bondia Francis Miyeyusho na Ronald  Pontillas wa Ufilipino lililokuwa lifanyike leo limeahirishwa hadi Aprili 12, kutokana na sababu ambazo ziko juu ya uwezo wa waandaaji.
Katibu Mkuu wa Chama cha Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST), Anthony  Lutha, alisema pambano la Miyeyusho limeahirishwa kutokana na sababu ambazo ziko juu ya uwezo wao.
Promota wa pambano hilo, Mussa Kova alisema, pambano la Miyeyusho  na Pontillas limeahirishwa baada ya  kocha wa bondia huyo kupewa taarifa tofauti kutoka hapa nchini.
“Pontillas aliambiwa pambano halitakuwepo na kiongozi wa ngumi (alimtaja jina) na alimwambia kuwa Miyeyusho ana pambano Aprili 26, hivyo hawezi kucheza Aprili 5 na kweli walipoangalia kwenye mtandao boxrec wakaliona hilo pambano hivyo wakaghairi kuja,” alisema Kova.
Alisema pambano hilo limesogezwa mbele hadi Jumamosi ijayo ambapo sasa Miyeyusho atapigana na bondia mwingine wa Ufilipino, Angelito Merin.

 

Tuzo za Kili zichague muziki bora siyo maarufu

Wasanii wa muziki wa kizazi kipya Banana Zorro (kushoto) na Ray C (kulia) baada ya kutwaa tuzo za Kili Music Awards mwanzoni mwanzoni mwa mwaka 2007 

Tuzo maarufu za muziki nchini ‘Kilimanjaro Music Award’ zinazoratibiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa kushirikiana na kampuni ya bia (TBL) zinatarajiwa kufanyika Mei 3 kwenye Uukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Basata na TBL, tuzo za mwaka huu zimefanyiwa mabadiliko katika mchakato wa kupata wateule watakaoingia katika vipengele mbalimbali.
Mabadiliko hayo ni kwamba wananchi wa kawaida walipewa fursa ya kupendekeza wanamuziki, nyimbo, vikundi, watayarishaji, video na vitu vingine wanavyodhani vinastahili kuwapo katika mchakato wa kuwapata wateule wa tuzo za muziki Tanzania tangu mwezi Februari.
Wananchi hao wa kawaida tangu Februari walipewa nafasi ya kutoa mapendekezo yao kwa kutumia mfumo wa SMS, na mtandao yaani tovuti na barua pepe.
Baada ya wananchi kutoa mapendekezo hayo, Basata, TBL na jopo la wataalamu wa tuzo hizo waliyachuja majina katika kila kipengele na kubakizsha majina matano ambapo hivi sasa wameyarudisha kwa wananchi kwa ajili kupigia kura washindi wa kila kipengele.
Washindi watakaopata kura nyingi baada ya kuchaguliwa na wananchi katika kila kipengele ndiyo watakaopewa tuzo zao katika hafla itakayofanyika Mei 3 kwenye Uukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Siku zote sisi tunaamini kwamba mabadiliko ni kitu cha muhimu katika maisha ya mwanadamu au katika shughuli tunazozifanya, lakini mabadiliko yasiwe katika kukwepa majukumu.
Tunasema hivyo kwa sababu tunaona utaratibu huu mpya umesahau kufikiria jambo moja kubwa la msingi kwa hizi ni tuzo za kutafuta muziki bora na siyo tuzo za kutafuta muziki maarufu.
Ni wazi kuwa siku zote wananchi wa kawaida huwa wanasikiliza nyimbo zinazopigwa kwenye vituo vya redio na televisheni mara kwa mara na wengi hawana utaalamu wa muziki.
Nyimbo nyingi zinazopigwa kwenye radio au kuonyeshwa kwenye televisheni ni nyimbo maarufu na siyo lazima ziwe ni nyimbo bora kwa sababu siku hizi wanamuziki hutoa fedha ili nyimbo zao zipigwe kwenye radio na kuonyeshwa kwenye televisheni.
Ndiyo maana tunasema mabadiliko ya kukimbia wajibu siyo mazuri kwani suala hili la kuchagua muziki bora linahitaji utaalamu kwa sababu kuna nyimbo nyingine ni bora, lakini hazipati nafasi ya kupigwa kwenye radio au kuonyeshwa kwenye televisheni kwa sababu wanamuziki wenye nyimbo hizo hawatoi fedha.
Hii inamaanisha katika tuzo za mwaka huu washindi watakaopatikana watakuwa ni wanamuziki, nyimbo au vikundi vinavyopata nafasi ya kupigwa kwenye readio au kuonyeshwa kwenye televisheni.
 

 

Yala: Shule iliyogeuka ‘kisiwa’

Sehemu ya Shule ya msingi Yala ikiwa  imejaa maji.

Yala ni shule ya msingi iliyopo katika Kijiji cha Yala Kata ya Luhanga Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya na ipo umbali wa kilomita 40 kutoka Barabara Kuu ya Mbeya-Iringa, ili kufika shuleni hapo inakulazimu kutembea kwa mguu kutokana na magari na pikipiki kushindwa kufika.
Shule hiyo ina muda wa zaidi ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, imezungukwa na mito minne ambayo imekuwa ikijaa maji kipindi cha masika na kusababisha kukatika kwa mawasiliano na ukosefu wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu.
Kutokana na tatizo hilo la mito kujaa maji shule hiyo imekuwa ikigeuka kuwa kisiwa na kusababisha wanafunzi na walimu kushindwa kufika shuleni kwani mito hiyo haina madaraja ya kuwawezesha kupita na kufika shuleni hapo.
Wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo wamekuwa wakitoka katika Vitongoji vya Mwashikamile, Ruaha, Waninyika, Mtakuja, Yala na Lusaka na wote hushindwa kuvuka mito hiyo na kufika shuleni huku walimu pia wakikumbwa na adha hiyo kutokana na shule hiyo kutokuwa na nyumba za kuishi Walimu.
Jairos Mpale ni Mwenyekiti wa serikali ndogo ya maendeleo ya Mwashikamile katika Kijiji cha Yala anasema kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa zaidi kwa mwaka huu ukilinganisha na miaka mingine.Hii ni kutokana na mvua zinanyesha kwa wingi na wanafunzi wamekaa nyumbani muda mrefu bila kwenda shule.
“Watoto wetu wameshindwa kwenda shuleni hapo tangu shule zote zilipofunguliwa Januari, kutokana na mito kujaa maji na kuna mamba wengi na viboko hivyo ni vigumu kuvuka kwenda katika Shule ya Yala na watoto wetu wamekosa masomo na hatujui ni lini wataanza masomo,” anasema.
Naye Mtendaji wa kijiji cha Yala shule ilipo, Isaac Ngera anasema kuwa tatizo hilo huwa linajitokeza mara kwa mara katika msimu wa mvua na mito hiyo imekuwa ikijaa na kusababisha wananchi kushindwa kupata huduma mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja elimu, afya na majisafi na salama.
Aliitaja mito iliyojaa maji kuwa ni Itambo na lwashimala na vitongoji vilivyopo ng`ambo ya mito hiyo ni Ruaha na Woninyika kwa upande wa Kusini kuna vitongoji vya Mtakuja na Lusaka ambavyo vipo ng`ambo ya Mto Itambo na yote imejaa maji hakuna mawasiliano na upande wa pili.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Stephano Mlewa anasema kuwa kwa sasa hali ni mbaya katika shule hiyo kwani hakuna mwanafunzi anayefika shuleni hapo.
“Siyo kwa wanafunzi pekee hata kwa Walimu ni tatizo kubwa kwani wanaishi katika kitongoji ambacho kipo mbali na shule hiyo na inawalazimu wavuke mito miwili ambayo kwa sasa imejaa maji hivyo hakuna masomo,” anasema.
Anasema kuwa shule hiyo pia ina changamoto ya madarasa kwani ina jumla ya vyumba vya madarasa vinne pekee na wanafunzi wapo kuanzia darasa la kwanza hadi la saba hivyo husoma kwa kupokezana.
Ofisa Elimu Wilaya ya Mbarali, Henerico Batinoluho anasema kuwa shule ina wanafunzi zaidi ya 400 na kwamba mwaka huu shule ilifunguliwa Januari 6, lakini wamefanikiwa kuingia darasani katika kipindi cha wiki moja pekee.

WHO: uvumi wa maambukizi ya Ebola ukome

  

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema kuwa kuzuka kwa Homa ya Ebola Magharibi mwa Afrika ni mojawapo ya changamoto kubwa zaidi ambazo limewahi kukabiliana nayo.
Shirika hilo limesema kuwa italichukua hadi miezi minne kuthibiti ugonjwa huo. Wakati huohuo shirika la kutoa misaada ya matibabu ya bure, Medicins Sans Frontieres, limesema kuwa linaendelea kufanya mashauriano na viongozi wa kijamii katika Wilaya moja Kusini mwa Guinea, ambalo lilisimamisha shughuli zake baada ya vituo vyake kadhaa kushambuliwa na wakaazi wa eneo hilo.
Msemaji wa shirika hilo katika mji mkuu wa Guinea wa Conakry - Sam Taylor - amesema inaeleweka kwamba watu wana uoga mkubwa.
"Sio taharuki, kimsingi huu ni uoga. Na tunaelewa hilo. Ni ugonjwa wa kugovya na pia ni mpya nchini Guinea, na kuna uvumi unaosambaa na pia kuna habari za kuotosha zinazoenea; na tunachohitaji kuona kwa wingi sasa ni watu kwenda kwa jamii mbalimbali kueleza ugonjwa huu, jinsi unavyoenea, na jinsi usivyoenea," alisema Bwana Taylor.
Ugonjwa huo umewaua watu 111 katika nchi za Guinea na Liberia tangu uchipuke mwezi uliopita.

Wednesday 2 April 2014

Mugabe asusia mkutano kuhusu CAR

Maelfu ya waisilamu wametoroka vita CAR na kukimbilia nchi jirani ya CAR

Viongozi wa Ulaya na Afrika wanatarajiwa kuanza kujadili mgogoro unaotokota katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati, katika mkutano maalum unaofanyika kando na kongamano la viongozi wa Ulaya mjini Brussels.
Rais Robert Mugabe amesusia kongamano hilo baada ya Muungano wa Ulaya kukataa kumwondolea marufuku ya muda ya Visa mkewe Grace.
Bwana Mugabe aliungwa mkono na Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, ambaye pia ameamua kuususia mkutano huo kama ishara ya kumuunga mkono Mugabe.
Zuma alisema kuwa muda umewadia wa Ulaya kukoma kuwaangalia waafrika kama sio watu.
Muungano wa Ulaya tayari umezindua kikosi cha jeshi lake nchini CAR, na kuelezea mipango yake kutuma wanajeshi 1,000 kuwasaidia wanajeshi wa Afrika na wale wa Ufaransa wanaoshika doria nchini humo.
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa waisilamu 19,000 wanakabiliwa na tisho la kuuawa nchini humo.
Maswala ya Uchumi na Uhamiaji pia yatapewa kipaombele kwenye mkutano huo.
Viongozi 30 wanatarajiwa kuhudhuria kongamano lenyewe wakiwemo marais wa Afrika.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon atahudhuria mkutano kuhusu CAR pamoja na viongozi wa Afrika na wale wa Muungano wa Ulaya.
Ameahidi kufAnya kila awezalo kuhakikisha anaimarisha juhudi za kukabiliana na migogoro ya kimataifa.

 

Zuma kujieleza kuhusu nyumba yake

 
Rais Jacob Zuma anatarajiwa kufika mbele ya kamati ya Bunge la A-Kusini kujieleza kuhusu kashfa ya kufuja pesa za umma zilizotumiwa kukarabati nyumba yake ya kifahari.

Ukarabati huo uligharimu dola million 23 na Bw Zuma ameamrishwa na mkaguzi au mlinzi wa mali ya umma nchini humo alipe baadhi ya pesa hizo .
Zuma alisema Jumatatu kuwa sio sawa kwake kutakiwa alipe sehemu ya pesa zilizotumiwa kwa ukarabati wa nyumba yake kwani sio yeye aliayeamuru ukarabati huo.
Alisema kuwa maafisa wa serikali ndio walioagiza ukarabati huo bila ya kumshauri.
Zuma alizungumza kwa mara ya kwanza Jumatatu tangu kashfa hiyo kujulikana akisema kuwa halipi chochote kwani hakuomba ukarabatai kufanywa.