Tuesday, 4 March 2014

Mwelekeo mpya bungeni, Pinda atoa hoja kutuliza hali ya hewa

Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alifanikiwa kutuliza hali ya hewa bungeni baada ya kutoa mapendekezo yaliyoungwa mkono na pande zote zilizokuwa zinavutana kuhusu kupitisha baadhi ya vifungu vya Kanuni za Bunge la Katiba. 

 

Katika mapendekezo yake yaliyoungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa CCM -Zanzibar, Vuai Ali Vuai, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Pinda alisema: “Nataka kuwaomba wenzangu wote kwenye maeneo hayo (yenye malumbano) tukiwa tunayapitia kama hatutaelewana tuyaache kwa muda na kumwomba Mwenyekiti aunde timu ya watu wazima na wenye busara wajaribu kuyatazama. “Tujadiliane, tushindane kwa lugha za staha, tusitumie lugha inayoweza kukasirisha. Isiwe mimi nimesema, mimi nimesema...”
Waziri Mkuu, aliwataka wajumbe wajiepushe na lugha za kuudhi ambazo zinaweza kukwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya.
Pinda alilazimika kuingilia kati baada ya kutokea mgawanyiko mkubwa wa namna ya kupiga kura kupitisha vifungu vya rasimu.
Akiunga mkono ushauri huo, Mbowe alisema Bunge limejaa hisia za hofu ndani na nje, jambo ambalo linatia wasiwasi wa kupatikana kwa Katiba Mpya. Alisema iwapo wajumbe watashirikiana na kuweka kando masilahi ya vyama, idadi yao katika makundi, Katiba inaweza kupatikana.
Vuai alionya kuhusu matumizi ya lugha za kuudhi huku Profesa Lipumba akiwataka wajumbe kuzingatia masilahi ya Taifa kama alivyoagiza Rais Jakaya Kikwete na kutengeneza Katiba ya Watanzania wote bila ya kujali masilahi binafsi.
Upigaji kura bungeni vita
Awali, mjadala wa utaratibu wa upigaji kura katika Bunge hilo ulichukua sura mpya baada ya kudaiwa kuwapo ushawishi unaohusisha utoaji wa bahasha ili kutaka kuungwa mkono katika misimamo inayokinzana.
Habari zilizopatikana zilidai kuwa watuhumiwa katika sakata hilo ni baadhi ya wajumbe ambao ni mawaziri na mbunge mmoja wa CCM. Vigogo hao wanadaiwa kuwashawishi wajumbe ambao hawatokani na vyama vya siasa ili kupitisha agenda ya kura ya wazi kirahisi.
Akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, Mjumbe wa Bunge hilo, Julius Mtatiro ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF, alisema: “Jaribio la kuzuia kura ya siri limechukua njia za aibu, baada ya CCM kutumia fedha kushawishi wajumbe.”
Katika ujumbe huo ambao alikiri kuuandika, Mtatiro aliwataja wajumbe watatu ambao ni mawaziri kuwa waliwakaribisha wajumbe kwenye makazi yao na “kuwaandalia chakula cha kutosha, vinywaji vya kutosha na viburudisho vingine, huku wakipewa bahasha za nauli baada ya vikao hivyo vya siri.” Mmoja wa waliotajwa ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe aliyedaiwa kuwaalika wawakilishi wa wafugaji na kuwapa chakuka na bahasha.
Akijibu tuhuma hizo, pamoja na kukiri kuwakaribisha baadhi ya wajumbe na kula nao chakula, alikana tuhuma za kuwahonga ili waunge mkono msimamo wa chama hicho. Alisema Mtatiro amemdhalilisha, hivyo anawasiliana na mwanasheria wake ili kumfikisha mahakamani.

 

 

Wabunge wa Libya washambuliwa 

Wabunge wawili nchini Libya walipigwa risasi na kuumizwa baada ya kundi la waandamanaji kuwashambulia bungeni katika mji mkuu wa Tripoli.
Walioshuhudia tukio hilo, walisema kuwa wawili hao walipigwa risasi walipojaribu kutoroka kutoka katika eneo hilo.
 
Waandamanaji hao waliokuwa na ghadhabu walilishambulia bunge hilo, huku wakitaka bunge lifungwe na tarehe mpya ya uchaguzi wa mapema itangazwe.
Kumekuwa na wimbi la maandamano nchini humo kutokana na uamuzi wa bunge la nchi hiyo kuahirisha tarehe ya uchaguzi hadi baadaye mwakani.
Waliolishambulia bunge siku ya Jumapili walisema kuwa walighadhabishwa pia na “kutekwa nyara” kwa waandamanaji waliokuwa na kikao nje ya bunge.
Walisema kuwa waliohusika na utekaji nyara huo walikuwa chini ya uongozi wa waasi wanaotumikia amri ya bunge.
Waandamanaji hao ambao wengi wao ni vijana walijihami kwa visu na vijiti,wakalishambulia bunge huku wakiwa na ujumbe kwa wabunge kwa kuimba “jiuzulu,jiuzulu”, kwa mujibu wa taarifa ya ashirika la habari la AFP.
Bunge la nchi ya Libya limeshambuliwa mara kadhaa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Nuri Abu Sahmein ambaye ni spika wa bunge hilo aliambia kituo cha televisheni cha Al-Nabaa kuwa maandamano yaliyokuwa ya amani, yalivurugwa na watu waliojihami.
"Wabunge wawili walipigwa risasi pale walipojaribu kutoweka mahali hapo kwa kutumia magari yao,” alisema.
Haikuwezakana kubaini papo hapo idadi ya wabunge walioumia.
Picha zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha waandamanaji wakivuta kile kilichokusudiwa kuwa kiti cha Spika wa bunge hilo nje ya bunge na kukichoma.
Mwandishi wa BBC Rana Jawad ambaye yuko Tripoli anasema kuwa bunge la Libya limeshambuliwa mara kadhaa na makundi tofauti, yakiwemo makundi ya waasi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Uchaguzi uliokuwa wa amani ulifanywa na nchi ya Libya katika mwezi wa Julai mwaka jana, ila bado nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ingali inang’ang’ana kupata utulivu, miaka mitatu baadaye tangu kufurushwa kutoka maamlakani kwa aliyekuwa rais, hayati Muammar Gaddafi.

 

Kirusi bwete chazinduka

Taarifa ya kirusi aina ya Pithovirus sibericum ambacho kimekuwa bwete kwa miaka zaidi ya 30,000 hadi kilipopelekwa tena kwenye mabara nchini Ufaransa imeendelea kuwa taarifa kuu.

kirusi cha Pithovirus sibericum 

Kirusi hicho cha kale kimerejesha uhai wake baada ya kukaa bwete kwa miaka zaidi ya elfu 30,000 , walieleza wanasayansi .
Kilipatikana kikiwa kimezama kwenye utando wa barafu katika eneo la Siberia, lakini baada ya kuzinduliwa kikawa tena na uwezo wa kusababisha maambukizi .
Wanasayansi wa Ufaransa wanasema hata hivyo kirusi hicho si hatari kwa maisha ya binadamu na wanyama , lakini hii inaonyesha kuwa virusi wengine wanaweza kuzinduka hata baada ya kuwa bwete kwa muda mrefu.
Taarifa ya utafiti huo ilichapishwa katika kituo cha kitaifa cha sayansi nchini Ufaransa (PNAS).
Professor Jean-Michel Claverie, wa kituo cha utafiti (CNRS) katika chuo kikuu cha Aix-Marseille nchini France, alisema: " Hii ni mara ya kwanza tumeona kirusi ambacho bado kina maambukizi baada ya kipindi kirefu kama hiki.
Kirusi hiki ambacho ni kikubwa kinaweza kuonekana kwa macho tofauti na virusi vingine vinavyoonekana tu kwa kutumia microscope, na kilipatikana kikiwa kimezikwa mita 30 chini kwenye barafu iliyoganda.
Wanasayansi wanasema kubainika kwa kirusi cha Pithovirus sibericum kunaonyesha hatari kwamba virusi vya maambukizi vinavyodhaniwa kuwa vimekufa vinaweza kuibuka tena baada ya miaka mingi na kusababisha maambukizi kutokana na shughuli za binadamu.

 

Monday, 3 March 2014

Urusi yatetea hatua ya kijeshi Ukraine 

   

Hali ya taharuki bado imelikumba jimbo la Crimea.

Urusi imetetea uamuzi wake kutuma wanajeshi nchini Ukraine, katika kikao cha dharura cha baraza la usalama la Umoja wa mataifa.

Balozi wa Urusi katika umoja wa mataifa, Vitaliy Churkin, amesema kuwa rais wa Ukraine aliyeng'olewa madarakani Viktor Yanukovych alikuwa ameiomba Moscow kutuma wanajeshi ili kuwalinda raia na kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Akizungumza baada ya mkutano huo wa Baraza la Usalama, Balozi Vitaly Churkin amesema kuwa malalamishi ya bwana Yanukovich yanafanana na yale ya Urusi.
"Nadhani ni muhimu kuzingatia kwamba mtu tunayeamini kuwa ndiye rais halaIi wa Ukraine pia ana wasiwasi tulio nao kuhusu idadi kubwa ya raia wa Ukraine, kuhusu kinachoendelea. Na ametoa wito kwa Urusi kutumia majeshi yetu kuzuia mambo kuwa mabaya zaidi.''
 
Marekani imesitisha ushirikiano na Urusi

Lakini balozi wa Ukraine, Yuriy Sergeyev, amesema kuwa madai ya Urusi hayahusiani na kile kinachojadiliwa kwani bwana Yanukovich hakuwa tena rais wa Ukraine.
"Hana lolote kwa sasa. Tukizungumzia hali ilivyo kwa sasa nchini Ukraine na madaraka ya kisheria ya mbunge ambalo lilimng'oa madarakani-hata balozi Churkin hivi leo kama ulisikia alichosema, ametaja kwamba tunaamini hatawahi kuwa rais wa Ukraine. Hii ina kwamba yeye siye mtu wa kuzungumza naye na hana lolote la kuzingatiwa."
Marekani imejibu kwa kusitisha mazungumzo ya kibiashara pamoja na uekezeji kati yake na Urusi, na idara ya Ulinzi ya Pentagon imetangaza kuwa ushirikiano wote wa kijeshi kati ya Marekani na Urusi ikiwemo mazoezi ya kijeshi, ziara za bandarini na mikutano ya mipango yote imesitishwa.

 

Watu 28 wauawa nchini China

Nchini Uchina, kundi moja la watu waliojihami kwa visu limewauawa takriban watu 28 katika kituo kimoja cha treni kusini magharibi mwa mji wa Kunming.  


 

Kituo cha habari cha Xhinua kimesema kuwa zaidi ya watu mia moja walijeruhiwa.
Mashahidi wamesema kuwa washambuliaji hao waliovalia nguo nyeusi,waliwavamia abiria waliokuwa wakingojea kuabiri treni na kuwakatakata huku wengine wakiwadunga visu wale walioshindwa kukimbia kwa kasi.
Kulikuwa na takriban washambuliaji 10.
Polisi waliwapiga risasi na kuwaua washambuliaji 5 huku wakiwasaka waliosalia.
Shirika la habari la Xhinua limewalaumu watu wanaopigania kujitenga katika mkoa wa Shinjiang kwa tukio hilo.

Obama aionya Urusi kuhusu Ukrain


Rais Obama aongea na rais wa Urusi Vladmir Putni katika simu


Rais Obama amesema kuwa Urusi inakiuka sheria ya kimataifa kufuatia hatua yake ya kuingiza vikosi vyake nchini Ukrain na sasa ametoa wito kwa rais Vladmir Putin kuvirudisha vikosi hivyo katika kambi zake za jimbo la Crimea.
katika mazungumzo ya simu yaliochukua takriban dakika 90,rais Putni amemwambia Obama kwamba Urusi ina haki ya kutetea maslahi yake iwapo ghasia zaidi zitaelekea mashariki kwa Ukrain pamoja na jimbo la Crimea.

Lakini rais Obama ameonya kwamba Urusi huenda ikatengwa kisiasa na kiuchumi iwapo uvamizi huo utaendelea.
Amemwambia rais Putni kwamba wasiwasi wowote wa Urusi kuhusu hali ya raia wa Urusi wanaoishi nchini Ukrain unafaa kujadiliwa ana kwa ana na serikali ya Ukrain.
Kaimu rais wa Ukrain, Oleksandr Turchynov,ameviweka vikosi vyake vya kijeshi nchini humo katika hali ya tahadhari.
Hatua hiyo inajiri baada ya bunge la Urusi kumruhusu Rais Vladimir Putni kutuma wanejeshi nchini Ukrain.
Wakati huohuo kaimu waziri mkuu Arseniy Yatsunuk amevitaka vikosi vya kijeshi vya urusi vinavyopiga doria katika eneo la Cremia kurudi kambini.
Ameonya kuwa iwapo mzozo huo utaendelea,Urusi ipo hatarini ya kukabiliwa kijeshi mbali na kumaliza uhusiano wake na Ukrain.

 

Ukraine yajizatiti kijeshi

Ukraine imeagiza kuimarisha vikosi vyake katika kukabiliana na Urusi ambayo inaimarisha jeshi lake katika jimbo la Ukraine la Crimea.

 

Kaimu Rais wa Ukraine Olexander Turchynov ameagiza kufungwa kwa safari za anga la nchi hiyo kwa ndege zote zisizo za kiraia.
Rais wa Marekani Barack Obama ameeleza usambazaji wa majeshi ya Urusi katika jimbo hilo ni "kuingilia uhuru wa Ukraine".
Waziri mkuu mpya wa jimbo la Crimea lenye mamlaka ya kujiamulia mambo yake lenyewe, Sergiy Aksyonov, mwenye mwelekeo wa kuipendelea Urusi, amesema amemwomba Bwana Putin ili kuhakikisha usalama wa eneo hilo.
Hata hivyo serikali ya mpito ya Ukraine haimtambui Bwana Aksyonov na serikali yake ya Crimea.