Monday, 24 March 2014

Bunge la Katiba Njiapanda

“Kama tunataka serikali ya tatu lazima tuitengenezee misingi ya uhakika na kuhoji nani atayeidhamini serikali ya tatu virungu, pingu, magari ya kuwasha, majeshi au bunduki.”
Dar es Salaam. Kwa neno moja unaweza kusema kwamba wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi kwa ujumla wako “njiapanda”.
Hii ni baada ya hotuba ya ufunguzi wa Bunge hilo iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kuibua mambo mazito ambayo kimsingi yanatofautiana na mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Huku wananchi wakijiuliza nini hatima ya Bunge hilo baada ya hotuba hiyo, baadhi ya wajumbe ambao wiki hii ndiyo wanaanza kujadili rasimu hiyo, watakuwa katika wakati mgumu wa kuamua wafuate maoni ya nani, kati ya viongozi hao wawili.
Ingawa Rais Kikwete amesema mara kadhaa kuwa wajumbe wa Bunge la Katiba ndiyo waamuzi. Mambo mengi aliyoibua yanaonyesha kutokubaliana kwake na baadhi ya maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu, ambayo Jaji Warioba amewahi kusema kuwa yanatakiwa kuheshimiwa.
Wakizungumzia tofauti hizo, mjumbe wa Bunge la Katiba, Ezekiah Oluoch alisema kauli za Rais Kikwete na Jaji Warioba zimezidi kuwagawa wajumbe wa Bunge hilo kwa maelezo kuwa tangu awali wajumbe hao walikuwa wamegawanyika katika makundi mawili; ya wanaotaka muundo wa Muungano uwe wa serikali tatu na wale wanaotaka serikali mbili.
Alisema kama suala la muundo wa Serikali likishindikana kupatiwa mwafaka ni vyema likarudishwa kwa wananchi ili wapige kura ya maoni kuchagua aina wanayoitaka, kisha suala hilo lirejeshwe tena katika Bunge la Katiba kwa ajili ya kuboreshwa.
“Rais alipoanza kuzungumza alikuwa kama mkuu wa nchi lakini mwisho wa hotuba yake aligeuka kuwa mwenyekiti wa CCM. Kifupi alichokizungumza kimekwenda tofauti na wadhifa wake,” alisema.
Naye Deo Filikunjombe alisema: “Nadhani kwa hotuba hizi mbili, kazi ya wajumbe wa Bunge la Katiba itakuwa rahisi. Maana sasa wameshajua uzuri na ubaya wa serikali tatu na mbili.
“Hata kama kutakuwa na tofauti, wananchi ndiyo watakuwa wa mwisho kuamua kama Katiba hii ipite au isipite. Tunachotakiwa wajumbe ni kuwa makini na uamuzi wetu.”
Naye Yusuf Manyanga alisema: “Bunge la Katiba limejaa watu wenye busara. Sidhani kama tutashindwa kuelewana maana hata katika biashara ya utumbo inzi ni wengi lakini utumbo unauzika.”
Katika hotuba yake aliyoitoa Ijumaa iliyopita Rais Kikwete aligusia mambo saba ya msingi yaliyomo katika rasimu ya Katiba na kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha kuwa mengine hayawezekani kutekelezeka.

 

Sitta ‘amkataa’ Warioba bungeni

Mwenyekiti wa Bunge maalumu la katiba, Samuel Sitta 

Dodoma. Jaribio la kutaka kumrejesha bungeni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ili ajibu masuala yaliyoibuliwa na Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya kufungua Bunge limegonga mwamba.
Uamuzi wa kukataa ombi hilo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta wakati akijibu mwongozo ulioombwa na Mjumbe wa Bunge, Julius Mtatiro, akisema hadhani kama ni sahihi ombi hilo kutekelezwa.
Awali Mtatiro aliomba mwongozo kwa mwenyekiti, akitaka kujua iwapo kuna haja ya kumrejesha Jaji Warioba kutoa ufafanuzi juu ya baadhi ya hoja za Rais Kikwete ambazo zimekinzana na maoni ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba.
Mtatiro alisema: “Mtoa hoja mahususi alikuwa ni Jaji Warioba na Rais Kikwete alialikwa kama mgeni rasmi kufungua Bunge, lakini badala yake alikuja kujibu hotuba ya Warioba.
“Kwa sababu Rais alikaribishwa kama mgeni rasmi, lakini  alijibu  hoja za Warioba, je, hatuoni kama kuna haja ya kumrejesha mtoa hoja mahususi aje kujenga hoja  kutokana na alichosema Rais Kikwete?” alihoji Mtatiro ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF.
Katika ufafanuzi wake, Sitta alisema tayari amepokea kwa maandishi kutoka kwa baadhi ya wajumbe kuzungumzia suala hilo, jambo ambalo litafanyika lakini si kwa kumwita tena Jaji Warioba. Tunapenda kupata muda wa kuzungumzia  suala hili ili kuliweka sawa, hotuba zote mbili ambazo ni muhimu zitaandaliwa ili kupitiwa kuona kama malalamiko yanayotolewa yana hoja,” alisema Sitta.
Tangu Rais Kikwete ahutubie Bunge Ijumaa na kutoa hoja kinyume na mapendekezo ya Rasimu ya Katiba, hasa muundo wa Muungano, kumeibuka mijadala ya ama kuipinga au kuiunga mkono, huku wengine wakieleza kuwa imekiuka sheria.

 

 

 

Marekani kusaidia UG kupambana na Kony


Kiongozi wa waasi wa LRA Joseph Kony

 Serikali ya Marekani inatuma ndege ya kivita na kikosii maalum cha jeshi kusaidia Uganda katika juhudi za kumsaka kiongozi wa kundi la waasi la Lord's Resistance Army, Joseph Kony.Msemaji wa baraza la usalama la Marekani, Caitlin Hayden, amesema kuwa wanajeshi wa Afrika wataendelea kuongoza operesheni hiyo, ingawa watapata ushauri kutoka kwa vikosi vya Marekani.Alisema kuwa ndege hiyo itawekwa nchini Uganda ingawa itatumika katika nchi zingine ambako waasi wa LRA wamekuwa wakijificha.Marekani ilituma vikosi vyake mara ya kwanza nchini Uganda mwaka 2011 kusaidia Uganda katika harakati za kumtafuta Joseph Kony.

 

529 wahukumiwa kifo Misri

Mahakama nchini Misri imewahukumu kifo watu 529 ambao wanasemekana kuwa wafuasi wa Rais aliyeng'olewa mamlakani Mohammed Morsi.
Watu hao walikabiliwa ma mashitika mbali mbali yakiwemo mauaji ya polisi na kuwavamia polisi.
Wafuasi hao wa chama kilichopigwa marufuku, cha Muslim Brotherhood, ni sehemu ya kundi lengine kubwa la watu zaidi ya 1,200 wanaoaminika kuwa wafuasi wa Morsi.
Maafisa wa utawala nchini Misri wamekuwa wakiendesha msako mkubwa dhidi ya wafuasi wa vuguvugu hilo, tangu Morsi kuondolewa mamlakani mwezi Julai mwaka jana.
Maelfu wamekamatwa huku mamia wakiuawa.
Mahakama hiyo ilitoa hukumu baada ya vikao viwili pekee ambapo mawakili wa watuhumiwa walilalamika kuwa hawakupewa muda wa kuwasilisha kesi yao vyema.
Mauaji wanayodaiwa kufanywa na watuhumiwa yalitokea Kusini mwa Misri, mwezi Agosti, baada ya vikosi vya usalama kuvunja kambi mbili za wafuasi wa Morsi waliokuwa wanataka arejeshwe mamlakani

 

Makahaba watumia Vibaya Hijab Kenya

Makahaba katika baadhi ya sehemu za mji mkuu wa Kenya , Nairobi, wametupilia Mbali vazi la 'Mini skirt na kuanza kutumia Hijab kama njia ya kuwavutia wateja wao, jambo ambalo limekashifiwa vikali na wakuu wa dini ya Kiislamu.
Hijab huvaliwa na wanawake wa Kiislamu kama ishara ya kumcha Mungu, lakini makahaba katika mtaa wa Eastleigh, viungani mwa Nairobi wanatumia Hijab ili kuwafanya wateja wao kudhania kua wanatoka sehemu za Pwani.
Taarifa hii ni kwa mujibu wa mtandao wa shirika la habari la Nation mjini Nairobi.
Mwanamke mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kuwa yeye hupata wateja maradufu kwani huvalia vazi hilo la Hijab, wengi wa wateja wake wakimuona kama mwenye nidhamu.
Uchunguzi ulibaini kuwa wanawake wasio wa kiislamu wanavalia vazi hilo ili kuwavutia wanaume ambao wanaamini kuwa wao wana maadili zaidi ya wale wanaovalia nguo fupi au 'Mini Skirt'.
Nguo fupi ni mavazi yaliyozoeleka kwa makahaba sehemu nyingi duniani
Taarifa hiyo imemnukuu Imam mkuu wa msikiti wa Jamia mjini Nairobi, Mohamed Swalihu akisema kuwa ni jambo la kusikitisha sana kuwa Hijab inatumika kwa njia isiyopaswa na makahaba huku akiongeza kuwa pia wanaume wanalitumia vazi hilo kuendesha shughuli za uhalifu jambo ambalo amelitaja kuwa la kishetani linalostahili kukashifiwa vikali.
Hata hivyo chama cha makahaba nchini Kenya kimewatetea makahaba hao wanaotumia hijab huku likidai kwamba wanafanya hivyo ili kukidhi mahitaji ya wateja wao.
Mratibu wa muungano huo, Bi Phelister Abdalla, aliiomba serikali kuhalalisha ukahaba kwa madai ya viwango vya juu vya ukosefu wa ajira.
Mahojiano na makahaba katika mtaa wa Eastleigh yalibaini kwamba wanaume hawakuwa na haja ya wanawake wenye kuvalia nguo fupi badala yake wakipendelea wanawake wa kiislamu na wale wa kutoka Ethiopia.

Monday, 17 March 2014


RIDHIWANI AANZA MBIO ZA KUSAKA KURA JIMBO LA CHALINZE‏


Meneja wa Kampeni za Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndg. Steven Kazidi (kushoto) akimuinua mkono juu kwa ishara ya kumnadi Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo (CCM), Ndg. Ridhiwani Jakaya Kikwete wakati wa mkutano wa kwanza wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha Matipwili, Saadani Wilayani Bagamoyo jana Machi 14,2014.
Mgombea Ubunge katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Chalinze (CCM), Ndg. Ridhiwani Jakaya Kikwete akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Matipwili, Saadani Wilayani Bagamoyo, wakati wa mkutano wa kwanza wa kampeni zake ulioanza rasmi jana Machi 14,2014.Baada ya kumaliza Mkutano na Wananchi wa Kijiji cha Matipwili, Mgombea Ubunge katika Uchaguzi Mdogo Jimbo la Chalinze,Ndg. Ridhiwani Jakaya Kikwete alifika katika Kijiji cha Gongo ndani ya Tarafa ya Saadani na kukutana na wananchi wa Kijiji hicho na kuzungumza nao kama aonekanavyo pichani.

Mbunge wa Arumeru Mshariki , Joshua Nassari aumbuka bungeni




Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Joshua Nassari, juzi alijikuta akiumbuka bungeni baada ya kushindwa kutaja kanuni aliyoitumia, kuomba mwongozo. 
 
Hali hiyo ilitokea muda mfupi kabla ya wajumbe kupiga kura za kumchagua Mwenyekiti wa Bunge hilo.
 
Kuumbuka kwa mjumbe huyo ambaye pia ni Mbunge wa Arumeru Mshariki, kulitokana na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho, kumtaka kutaja kanuni aliyoitumia.
 
Hata hivyo, baada ya kusita kwa muda Nassari bila kutaja kanuni aliyoitumia, alisema wajumbe wengi hawajasikia utaratibu unaotumika katika upigaji kura kwa sababu walichelewa kwenye msongamano wa watu getini.
 
“Wengi wetu tumeingia tukiwa tumechelewa kwa sababu wengi tunapita katika geti moja. Ningependa ufafanuzi wako kuhusu aina ya kura tunayokwenda kupiga ni ya wazi au ya siri,”alisema.
 
Hata hivyo, kificho alimjibu kuwa kura zitakazopigwa kumchagua mwenyekiti zitakuwa ni za siri.
 
Hatua hiyo imekuja muda mfupi baada ya Bunge hilo kupitisha kanuni za uendeshaji wake ambapo hata hivyo nyingine bado zimekuwa na mgongano wa maridhiano kwa baadhi ya wajumbe kutaka ufafanuzi zaidi.