Thursday, 27 March 2014

Seif: Hatuko tayari kujadili serikali mbili

Zanzibar. Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama chake cha CUF hakiko tayari kujadili mfumo wa Muungano wa serikali mbili kama inavyotetewa na wabunge wa CCM na Rais Jakaya Kikwete.
Amesema tayari amewaandikia barua Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuwaeleza juu ya msimamo huo.
Maalim Seif alitoa msimamo huo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kibandamaiti mjini Unguja.
Isitoshe, alisema CUF imebaini kuwa kuna njama za kufuta kipengele katika Katiba ya Zanzibar kinachosema; “Zanzibar ni nchi” na kwamba hiyo ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu kwa kuwa Wazanzibari kamwe hawatakubali kufanya hivyo.
Maalim Seif alisema haikuwa mwafaka kwa Rais Kikwete kukosoa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba yanayotaka mfumo wa Muungano kuwa wa serikali tatu.
Alisema Jaji Warioba aliweka kando itikadi yake ya CCM katika utendaji wake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuja na uamuzi huo kwa vile ndiyo tiba ya kero za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Mapendekezo yaliyowasilishwa na Jaji Warioba hayakuwa maoni yake, yale ni maoni ya wananchi, Tanganyika imevaa koti la Muungano, ametoa ushahidi wake ili kujenga mwafaka katika kuendeleza Muungano wenye mfumo wa serikali tatu,” alisema Maalim Seif.
Alisema Muungano wa serikali mbili hauvumiliki na kama kuna watu wanaendelea kuutetea mfumo huo, Zanzibar inaweza kutumia sheria yake ya kura ya maoni kuwauliza wananchi wanaotaka na wasiotaka jambo hilo.
“Nimemwandikia barua Rais Kikwete, nakala nimempelekea Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, Tanzania Bara wanataka Zanzibar iondoe kifungu cha Katiba kinachosema Zanzibar ni nchi, jambo hilo halitapita...tutafanya kampeni wananchi walikatae,” alieleza Katibu Mkuu huyo wa CUF.
Alisema ni jambo la kusikitisha katika hotuba yake alijisahau kama ni mkuu wa nchi na analihutubia Bunge Maalumu badala yake akaegemea kuwa mwenyekiti wa CCM.
Alisema haikuwa sahihi kutoa vitisho na kutaja ikiwa Serikali ya Muungano chini ya Serikali tatu italegalega, jeshi litachukua madaraka ya nchi.
“Rafiki na ndugu yangu Kikwete, usifikiri huu ni wakati ule wa Julius Nyerere, akisema yeye hakuna wa kumpinga. Mambo yamebadilika, usijifanye ni Nyerere mpya, hakuna atakayekusikiliza na kubabaika,” alisisitiza Maalim Seif.

Rwanda na A.Kusini kusuluhisha mgogoro

Rais Jacob Zuma wa Afrika-Kusini na Paul Kagame wa Rwanda wamekubaliana mjini Luanda Angola, kuanzisha mazungumzo ya pamoja ya kumaliza mzozo wao wa kidiplomasia

Jaribio la kumuua Kayumba Nyamwasa lilitibuka Afrika Kusini
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulianza kuzorota pale Rwanda ilipowafukuza maafisa sita wa ubalozi wa Afrika Kusini, saa chache baada ya Afrika Kusini kuwatimua wanadiplomasia watatu wa Rwanda kuondoka nchini humo karibu wiki tatu zilizopita.
Afrika Kusini ilichukua hatua hiyo baada ya nyumba ya mpinzani mmoja wa Rwanda anayeishi Afrika Kusini Kayumba Nyamwasa kushambiliwa.
Lakini Serikali ya Rwanda ilisema hatua ya kuwatimua maafisa sita wa ubalozi wa Afrika Kusini mjini Kigali ni ya haki na ilizingatia uchokozi ambao ulianzishwa na serikali ya Afrika Kusini yenyewe kwa kufukuza maafisa watatu wa ubalozi wa Rwanda.
Rwanda ilisema kuwa Afrika Kusini ndio ilianza uchokozi kwa kuwatimua mabalozi wake watatu 

Jenerali Kayumba Nyamwasa, ambaye aliwahi kuwa mkuu wa majeshi nchini Rwanda, hakuwa nyumbani wakati wa shambulio hilo.
Nyumba yake iliharibiwa huku komputa na baadhi ya nyaraka zilichukuliwa.
Mkutano wa usalama uliofanyika mjini Luanda ulijadili hali kati ya nchi hizo mbili huku viongozi hao wawili wakikikutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu mzozo huo kutokea.
Rais Zuma alisema kuwa wamekubaliana kusuluhisha mgogoro huo na pia kupata taarifa ya pamoja ili kuweza kusuluhisha tofauti kati yao.
Kadhalika Rais Zuma aliongeza kwamba serikali yake inatekeleza wajibu wake wa kimataifa kwa kuwapa hifadhi watu wanaoomba. Viongozi hao wawili wamekubaliana kukutana kwa ajili ya kuzungumzia swala hilo baadaye.

Obama kukutana na Papa Francis


Obama Kukutana na Papa Francis

Rais Barrack Obama wa Marekani anatarajiwa kukutana na kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis, katika makao yake makuu huko Vatican.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Obama kukutana na papa Francis.
Wawili hao wanatarajiwa kujadili namna ya kupunguza tofauti iliyopo kati yao katika maswala mengi mbali na kujaribu kuinua maisha ya watu maskini duniani baada ya takwimu kuonyesha kuwa tofauti ya mapato kati ya matajiri na Masiki inaendelea kupanuka .
Aidha viongozi hao wawili wanatazamiwa kujadili hali ilivyo Nchini Ukraine, na swala la upatikanaji wa amani mashariki ya kati.
Mwafaka baina ya mitazamo tata kuhusiana na maswala ya uavyaji mimba, matumizi ya dawa za kupanga uzazi na ndoa ya jinsia moja pia inatarajiwa kuwa kati ya mada itakayojadiliwa .

 

Mkuu wa Jeshi kugombea Urais Misri

 Mkuu wa majeshi na waziri wa ulinzi Misri, Abdul Fattah al-Sisi, ametangaza kujiuzulu jeshini ili kugombea katika uchaguzi wa urais mwezi ujao.Wagombea wote wanapaswa kuwa raia.

Akizungumza Kwenye hotuba ya Televisheni huku akiwa amevalia sare ya kijeshi Abdel Fattah El Sissi amesema yeye sio mwanajeshi tena baada ya miaka 44 na kwamba amechukua hatua hiyo ili aweze kutimiza jukumu lingine muhimu.
Ni Bayana kwana Sisi hatakua na kibarua kigumu kujipatia ushindi katika uchaguzi wa Urais. Anaungwa mkono na idadi kubwa ya raia wa Misri na hadi sasa hana wapinzani wowote.
Baadhi ya waliotaka kugombea urais wamejiondoa wakidai kwamba hawataweza kuendesha kampeni zao kwa njia huru.
Wafuasi wake Sisi wanamuona kama kiongozi imara ambaye anaweza kurejesha amani na udhabiti nchini Misri baada ya miaka mingi ya machafuko.
Wakosoaji wake wanasema ana msimamo mkali na amechangia pakubwa katika kusambaratisha na kuhujumu upinzani nchini Misri.
Mkuu huyo wa jeshi atakabiliwa na majukumu mazito ya kufufua uchumi uliofifia , kupambana na uasi na kuileta pamoja nchi iliyogawanyika. Ameahidi kutekeleza mabadiliko makubwa lakini akaonya kuwa hawezi kufanya miujiza.

Tuesday, 25 March 2014

Kuhusu shambulizi la Kanisa Mombasa na mtoto ambae mpaka sasa ana risasi kichwani

Home » General News » Kuhusu shambulizi la Kanisa Mombasa na mtoto ambae mpaka sasa ana risasi kichwani

Kuhusu shambulizi la Kanisa Mombasa na mtoto ambae mpaka sasa ana risasi kichwani

Screen Shot 2014-03-25 at 8.53.23 AM
Idadi ya waliofariki kutokana na shambulizi la Kanisa Mombasa Kenya March 23 2014 imefikia sita ambapo wote hao vifo vyao vimetokana na majereha ya risasi huku wengine tisa waliokua wakipata matibabu hospitali wakiruhusiwa kwenda nyumbani.
Mkuu wa Polisi Kenya amesema bado hawajafutilia mbali kwamba lilikua shambulio la kigaidi ambapo kwa mujibu wa Erick Ponda ambae ni mwandishi wa habari wa DW Mombasa alieongea na millardayo.com akisema mpaka March 24 2014 jioni watu 59 walikua wamekamatwa na Polisi kwenye msako wakituhumiwa kuhusika na shambulio hilo.
Wakati huohuo, mtoto ambae bado kichwani kwake kuna risasi aliyopigwa kwenye shambulio hilo amepelekwa kwenye hospitali ya binafsi kwa matibabu maalum kwa sababu anahitaji kufanyiwa upasuaji ili kuokoa maisha yake.
Mama mzazi wa mtoto huyu alifariki kwenye hili shambulio hivyo kwa sasa mtoto yuko na ndugu wa mama yake ambae namkariri akisema ‘haendelei vizuri manake amekua akinisumbua hawezi kulala, ana maumivu makali sana kichwani kutokana na hiyo risasi ndani ya kichwa’
Viongozi wa kidini wakiongozwa na Askofu Julius Atsango wamewataka wenzao wa dini ya kiislamu kuisaidia serikali kuwakamata wanaosingizia dini kutekeleza mashambulizi

 

Monday, 24 March 2014

Zanzibar yashauriwa kurekebisha Katiba

 

 Alisema wakati Katiba ya Zanzibar ikieleza hivyo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sura ya 1 inaelezaa kuwa Tanzania ni nchi moja na eneo lake la mipaka ni kuanzia Tanzania Bara hadi Visiwani

Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeshauriwa kufanya marekebisho ya Katiba kabla ya Uchaguzi Mkuu Mwaka 2015 ili kuondoa vifungu vinavyogongana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ushauri huo umetolewa na mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar, Ali Hassan Khamis wakati akiwasilisha mada juu ya hali ya kisiasa na mchakato wa Katiba ya Muungano katika kongamano lililoandaliwa na Jumuiya za CCM, lililofanyika kwenye Ukumbi wa Tawi la Kiembesamaki Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Alisema migongano inayojitokeza katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar imetokana na marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 iliyogongana na Katiba ya Muungano na kusababisha mjadala mkubwa katika mchakato wa mabadiliko ya katiba unaoendelea.
Alisema marekebisho hayo ya Katiba ya Zanzibar yameongeza migongano hasa sura ya 1(1) inayoeleza kuwa Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyozungukwa na bahari yake, ambayo kabla ya Muungano wa Tangayika na Zanzibar ilikuwa ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Alisema wakati Katiba ya Zanzibar ikieleza hivyo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sura ya 1 inaelezaa kuwa Tanzania ni nchi moja na eneo lake la mipaka ni kuanzia Tanzania Bara hadi Visiwani.
Aliwaeleza washiriki hao kuwa kifungu cha 2(a) cha Katiba ya Zanzibar kimempa uwezo Rais wa Zanzibar kuigawa Zanzibar katika mikoa na wilaya kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Alisema marekebisho hayo ya 10 yamechangia kwa kiwango kikubwa kuibua migogoro ndani ya Muungano na kutaka Katiba ya Zanzibar iandikwe upya na wananchi wapewe nafasi ya kuijadili na kuamua.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Vilevile alieleza katika marekebisho hayo ya 10 kuna vitu viliondolewa lakini havikuwa na ulazima kama wakuu wa mikoa kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLW), wakati ni watendaji wakuu wa shughuli za Serikali katika kuwahudumia wananchi kwenye maeneo yao.
“Wakati umefika katiba yetu ya Zanzibar iangaliwe upya iendane na Katiba ya Jamhuri ya Muungano vinginevyo tutaendelea kuendeleza migogoro na kuathiri msingi mzima wa Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar,” alisema Ali Hassan Mkuu wa Wilaya ya Kati wa zamani visiwani humo.
Akifafanua zaidi alisema hata muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), una kasoro Zanzibar kutokana na sera ya CCM kuwa ni moja kati ya Zanzibar na Tanzania Bara lakini mfumo huo wa Serikali umezingatiwa upande marekebisho hayo ya kati mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Chama chetu ni kimoja, ni sehemu gani sera yetu imesema CCM ikishinda itaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa wakati hilo Tanzania Bara halipo,” alisema.

 

Ikulu: Kujadili hotuba ya JK kupoteza muda

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salva Rweyemamu

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salva Rweyemamu amesema kuendelea kuijadili hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyotoa kwenye Bunge la Katiba mwishoni mwa wiki ni kupoteza muda.
Akizungumza na gazeti hili jana, Rweyemamu aliushangaa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuendelea kutoa matamko yanayoipinga hotuba hiyo, akisema haumtendei haki mkuu huyo wa nchi na Watanzania wote kwa ujumla. Alisema kama Mtanzania, Rais alitoa maoni yake na amekuwa muungwana kwa kuwaambia kwamba bado wana fursa ya kujadili na kuleta mapendekezo yao, lakini wajali zaidi masilahi ya taifa.
“Hiyo ni propaganda isiyokuwa na maana kwa taifa na hata hatima ya Katiba yenyewe. Ningependa kuwakumbusha kwamba Watanzania wamewapeleka Dodoma wakajadili Katiba na siyo kufanya propaganda, tunawataka wafanye kazi,” alisema Rweyemamu.
Kwa mujibu wa Rweyemamu, umoja huo wenye viongozi kutoka vyama vya upinzani haumtendei haki Rais kwani kama Mtanzania, mkuu huyo wa nchi ana fursa ya kutoa maoni yake.
“Wasifikiri kwa kumjibu hivyo Rais wanajibizana na CCM. Rais ni mkuu wa nchi ana maoni yake, lakini zaidi ya yote, Bunge la Katiba siyo mahali pa kufanya siasa. Kama wanataka siasa tunawaomba warudi maofisini mwao wakafanye siasa, pale tumewatuma kazi,” alisisitiza.
Rweyemamu alibainisha kuwa mchakato wa kutunga Katiba unahitaji busara na busara hiyo haiwezi kupatikana kama watu waliotumwa kuwawakilisha wananchi wameamua kufanya siasa.
“Tunahitaji watu wote wawe CCM, CUF, Chadema na vyama vingine waache siasa,” alisema.
Wakati huohuo, bungeni Dodoma limeibuka kundi la wajumbe, wengi wao kutoka CCM wakiipongeza hotuba hiyo ya Rais Jakaya Kikwete na kuwakosoa watu wanaotishia kumpeleka Rais mahakamani kwa madai ya kuvunja kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuingilia mchakato wa maoni.
Mjumbe wa kundi hilo linalojiita Tanzania Kwanza, Evod Mmanda alisema siyo kweli kuwa Rais amevunja sheria kwani alihutubia Bunge baada ya kupitishwa kwenye kanuni za Bunge kifungu cha 75(1) ambacho kinaeleza mwenyekiti anaweza kumwalika mgeni rasmi kulihutubia Bunge.
Walioambatana na Mmanda ni Dk Emmanuel Nchimbi, Said Nkumba, Mohamed Thabit Kombo, Waride Jabu, Seleman Jafo na Charles Mwijage.