Tuesday, 4 March 2014

Mamilioni ya Airtel ‘Mimi ni Bingwa’ yaenda Bukoba

Dar es Salaam. Promosheni ya ‘Mimi ni Bingwa’ imemtangaza Rashid Jacob Kagombola, mkazi wa Bukoba mkoani Kagera kuwa mshindi wa Sh50 milioni katika droo kubwa ya bahati nasibu iliyochezeshwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania mwishoni mwa wiki Dar es Salaam.
Akimtangaza mshindi huyo, Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando alisema: “Leo hii tumefikia mwisho wa Promosheni yetu ya ‘Mimi ni Bingwa’ ambayo imewanufaisha Watanzania wengi. Limekuwa ni zoezi la mafanikio likishirikisha idadi kubwa ya wateja waliojiunga katika promosheni hii iliyokuwa na vipengele tofauti.”
“Ningependa kuwashukuru wateja wetu kwa kushiriki promosheni hii tangu ilipoanza mwishoni mwa Novemba mwaka jana. Airtel bado ina mipango mingine mingi inakuja, tukilenga kuendelea kurudisha kile tulichonacho kwa wateja wetu na kuisaidia jamii inayotuzunguka kukuza viwango vyao vya maisha.”
Alisisitiza kuwa mbali na zawadi hiyo ya Sh50 milioni kutolewa, washindi wa awamu ya pili na ya tatu wa safari iliyogharimiwa kila kitu ya kwenda kuangalia mechi ya Klabu ya Manchester United wataondoka nchini mwezi huu pale klabu hiyo itakapocheza tena kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Naye mshindi wa Promosheni hiyo, Rashid Jacob, akizungumza kwa njia ya simu kutoka Bukoba, aliipongeza Airtel Tanzania kwa kuanzisha promosheni hiyo ambayo amedai imesaidia kubadili maisha ya wateja wake na kuwa na mabadiliko chanya katika jamii na nchi nzima kwa jumla.
“Hii ni miujiza inayotokea maishani mwangu. Siwezi kuamini nami nimeingia katika orodha ya mamilionea Tanzania. Kwangu ni kama kutimia kwa ndoto kwa sababu ya Airtel. Naishukuru Airtel Tanzania. Hakika hizi milioni 50 zitabadilisha maisha yangu kabisa na zawadi nitakayoipatia Airtel ni kubaki kuwa mteja wao mwaminifu wakati wote,” alisema Kagombola.
Wakati wa promosheni hiyo, washiriki wawili wa Mimi ni Bingwa wa kila siku walizawadiwa Sh2 milioni , wawili wa Sh5 milioni katika droo za kila wiki na mmoja tiketi mbili za safari iliyogharimiwa kila kitu kwenda jiji la Manchester.

 

Kardinali Pengo aweka wazi msimamo wa Kanisa

 Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo akiwaonesha waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, nakala ya gazeti la Mwanachi lililoandika habari kuhusu msimamo wa Kanisa juu ya suala la serikali tatu. Picha na Venance Nestory  

Dar es Salaam/Iringa. Siku mbili baada ya Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kutoa waraka wa kulitaka Bunge Maalumu la Katiba kutopuuza mapendekezo ya muundo wa serikali tatu, Askofu Mkuu wa Jimbo Mkuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameibuka na kusema msimamo huo siyo wa Kanisa Katoliki nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kardinali Pengo pamoja na kukiri kuwa tume ilitoa maoni hayo, alikanusha kuwa taarifa zilizotolewa na moja ya magazeti kuwa msimamo wa Kanisa Katoliki ni serikali tatu.
“Maoni ya Tume hayawezi kuwa ni msimamo wa kanisa. Kanisa Katoliki lina utaratibu wa kutoa misimamo yake na huwa inatolewa na Mwenyekiti wa TEC,” alisema.
Hata hivyo, Rais wa TEC, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kutoka Jimbo la Iringa, alisema jana kuwa alikuwa na shughuli nyingi, hivyo asingeweza kuzungumzia suala hilo, labda wiki ijayo.
Akizungumza katika makazi yake mjini Iringa, Askofu Ngalalekumtwa alisema: “Mniache, nina shughuli nyingi…labda mnitafute wiki ijayo,” alisema.
Vilevile, Pengo ambaye alirejea msimamo wake binafsi wa kuunga mkono Muungano wa serikali mbili, alisema kwa namna Rasimu ya Katiba ilivyo, hakuna kigezo cha kulazimisha Kanisa Katoliki litoe msimamo.
Alisema Kanisa Katoliki lingeweza kutoa msimamo iwapo Rasimu ya Katiba ingekuwa na dosari zinazohusu imani au maadili.
“Kwa mfano, (Rasimu) ingekuwa inasema, hakuna Mungu lazima tungekuja juu kwa sababu inaingilia imani yetu,” alisema Kardinali Pengo na kufafanua:
“Vilevile tungeweza kusema inakwenda kinyume na maadili iwapo inaruhusu kuua wazee au inaunga mkono ndoa za jinsi moja.”
Tamko la Tume
Tamko la tume hiyo inayoongozwa na Askofu Mkuu wa Tabora, Paulo Ruzoka liliweka bayana kuwa muundo wa serikali mbili haukutatua matatizo ya msingi na badala yake ulilimbikiza kero zilizosababisha Zanzibar kujiundia katiba yake mwaka 2010 bila kushauriana na Tanzania Bara.
Tamko hilo la kurasa 15 lililosambazwa kwa baadhi ya Wajumbe wa Bunge la Katiba, lilitolewa baada ya mkutano wa kitaifa wa Wajumbe wa Kamati za Majimbo za Haki na Amani za Kanisa hilo na Chama cha Wanataaluma Wakatoliki Tanzania (CPT), uliofanyika jijini Dar es Salaam Februari 5 na 6 mwaka huu.

 

Sitta apiga jaramba kuongoza Bunge

 

Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho, akizungumza na mjumbe wa Bunge hilo, Samuel Sitta (kushoto), ndani ya Ukumbi wa Bunge, Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman   

Dodoma. Siku moja baada ya kuteuliwa na CCM kuwania uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema ameanza kupitia sheria na kanuni zitakazomwezesha kuliongoza huku akiahidi kutenda haki kwa wajumbe wote iwapo atachaguliwa.
Akizungumza mjini Dodoma jana, Sitta alisema: “Nawashukuru wote waliokuwa wakiniunga mkono na niseme wazi kuwa nitatenda haki kwa wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba.”
Alisema kazi kubwa aliyonayo baada ya uteuzi huo ni kuhakikisha kuwa anazipitia sheria na kanuni zinazoongoza bunge hilo na sheria nyingine kwa kuwa ndizo nyenzo zake za utendaji kazi.
Akizungumzia mchakato wa uteuzi ndani ya chama hicho na mchuano uliokuwapo kati yake na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge alisema: “Hii ni hatua ya awali na ya kawaida tu ndani ya CCM. Mara nyingi chama changu kikiona kuna mambo yanayoleta msuguano, basi huamua kuteua jina moja kwa ajili ya kugombea. Wameteua majina mawili kwa demokrasia kabisa. Ninakishukuru chama changu kwa kuniteua na kwa sasa najiandaa na uchaguzi.”
Suluhu: Nitafanya maajabu
Kwa upande wake, Mjumbe wa bunge hilo aliyeteuliwa na CCM kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassan aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba ana uwezo mkubwa wa kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba na hana shaka katika uteuzi wake.
Samia ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), alijisifu akisema ana rekodi nzuri ambayo haitiliwi shaka kwa weledi wake na haoni tatizo kwa yeye kupewa nafasi hiyo.
“Nina rekodi nzuri ya kuongoza Serikali kwa muda mrefu na sijapata doa lolote, kwa hiyo sioni ugumu wowote,” alisema.
Samia aliwahi pia kuwa Waziri wa Ajira na Wanawake na baadaye, Waziri wa Utalii katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kabla ya kuwa Waziri wa Nchi, katika Ofisi ya Makamu wa Rais.
Kinana na mchakato
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alizungumzia mchakato uliompitisha Sitta kuwania nafasi hiyo na kusema ulilenga kuzuia mgawanyiko ndani ya chama.
Hata hivyo, alisema Chenge aliamua kwa hiari yake kujitoa baada ya kukubaliana na Sitta walipoitwa na uongozi wa chama kwa ushauri. Akizungumza katika mahojiano maalumu mjini Dodoma, Kinana alisema: “Kiutaratibu, yeyote ilimradi awe mjumbe wa Bunge la Katiba, angeweza kujitokeza kugombea uenyekiti. CCM, walijitokeza wawili walionyesha nia; Sitta na Chenge.






Mauaji zaidi yatokea Nigeria



Ghasia zaidi zimetokea Kaskazini Mashariki mwa Nigeria ambapo watu 13 wameuawa.
Mkaazi wa kijiji cha Jakana karibu na mji wa Maiduguri jimbo la Borno amesema takriban watu 40 wameuawa katika shambulio lililofanywa na kundi la Boko Haram JUmatatu usiku.
Kaskazini mwa Nigeria imeshuhudia mashambulio ya kundi la Boko Haram licha ya operesheni ya jeshi inayoendelea.
Hapo Jumapili usiku watu 30 waliuawa katika shambulio mji wa Mafa na watu wengine 90 waliuawa katika siku ya Jumamosi katika shambulio la bomu mjini Maiduguri.

Keqiang asema mageuzi ni sharti China 


Li Keqiang akihutubia bunge la Uchina.
Waziri mkuu wa China, Li Keqiang, ameuambia mkutano wa kila mwaka, wa bunge la taifa hilo mjini Beijing, kwamba maendeleo ya kiuchumi yanasalia kuwa jukumu kubwa zaidi la serikali, lakini marekebisho ya kimsingi ni sharti yatekelezwa japo ni machungu.
Bwana Li amewaambia maelfu ya wajumbe katika bunge la taifa hilo, Great Hall of the People, kwamba shabaha ya kila mwaka ya ukuaji wa kiuchumi itasalia kuwa asilimia saba nukta tano.
Akizungumzia tatizo la uchafuzi, amesema kuwa moshi mkubwa unaondelea kutanda katika miji mikubwa ya China, ni onyo la kiasili dhidi ya maendeleo yasiokuwa na mpango.
Waziri huyo mkuu wa China kadhalika ametangaza marufuku dhidi ya majengo mapya ya serikali kama sehemu ya kile alichokitaja kuwa mapambano bila huruma dhidi ya ufisadi.

 

Obama ataka wachunguzi kutumwa Ukraine

 

Hali ya wasiwasi imekumba jimbo la Crimea.
Rais Obama ametangaza mapendekezo ambayo huenda yakatoa suluhu kwa mzozo wa Ukraine, ikiwemo kuwatuma wachunguzi wa kimataifa na kuanzishwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Moscow na serikali mpya mjini Kiev.
Bwana Obama amejadili swala hilo kwa njia ya simu na chanzela wa Ujerumani, Angela Merkel.
Wachunguzi hao watalenga kulinda haki za watu wa kabila la Urusi waliopo katika jimbo la Crimea; na kwa upande wake Urusi itahitajika kuwaondoa wanajeshi wake katika jimbo hilo. Pendekezo hilo huenda likajadiliwa pembezoni mwa mkutano utakaofanyika nchini Ufaransa (Jumatano) ambao utawaleta pamoja wajumbe kutoka Marekani, Urusi na kwingineko kwa ajili ya kuijadili Lebanon.
Hapo awali waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry, amelaani kile amekitaja kuwa kitendo cha uchukozi kutoka Urusi dhidi ya Ukraine. Wakati wa ziara yake mjini Kiev ambapo aliweka shada la maua kuwakumbuka waandamanaji waliouwawa mwezi uliopita, bwana Kerry ameshutumu Moscow kwa kutumia uongo na vitisho kuficha ukweli.
Mwandishi wa BBC Sarah Reinsford aliyepo mjini Kiev amesema kuwa wakati akiweka shada la maua katika maeneo walikouwawa mamia ya waandamanaji mjini humo, John Kerry alikaribishwa na umati wa watu waliokuwa wakiomba msaada wa marekani.
Na hilo ndilo lililomleta hapa; kutoa msaada wa hali na mali na pia wa kisiasa kwa serikali ya mpito ya Ukraine, na pia ahadi ya msaada wa kifedha na wa kiufundi kusaidia katika kuimarisha uchumi, amesema mwandishi wetu.

Rais Putin.

Lakini zaidi ya yote bwana Kerry ameleta ujumbe kwa Moscow.
" Nadhani ni bayana kwamba Urusi imekuwa ikifanya bidii kubuni dhana ya kuiwezesha kutekeleza uvamizi zaidi. Urusi imezungumzia raia wachache wanaozungumza kirusi ambao wamezingirwa. Ukweli ni kwamba hawajazingirwa! Ukweli ni kwamba serikali mpya ya Ukraine imewajibika ipasavyo kwa kuhimiza utulivu na kujiepusha na uchokozi," amesema Bwana Kerry.
Haukuna ushahidi, amesisitiza, kwa madai ya urusi kwamba wanajeshi wake wanalinda raia wanaozungumza lugha ya kirusi nchini Ukraine akiishutumu moscow kwa kutumia uongo na vitisho kuficha ukweli.
Katika karne ya ishirini na moja, bwana Kerry ameonya, haiwezekani kuvamia taifa jingine na kisha kuamrisha matakwa yako yatekelezwe kwa kutumia mtutu wa bunduki. Na kisha akamhimiza rais Putin kuwaondoa wanajeshi wake katika jimbo la Crimea na kushughulikia malalamishi yake kupitia njia za kisheria na amani.
Lau sivyo, ameonya, kwamba Urusi itakabiliwa na vikwazo zaidi vya kiuchumi na kisiasa.

 

CHAMA KIPYA CHA SIASA ACT CHAIONDOA CHADEMA KIGOMA RASMI LEO SOMA HAPA LIVE!!


HATIMAYE CHADEMA YAFUTWA RASMI KIGOMA NA ACT-TANZANIA

CHAMA KIPYA CHA ACT CHASHUSHA BENDERA ZA CHADEMA KIGOMA

CHAMA cha Alliance For Change and Transparency Mkoa wa Kigoma,kimeshusha Bendera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA tawi la Ujiji stendi ya zamani na kupandisha bendera ya (ACT) wakati wa uzinduzi rasmi wa matawi sita katika manispaa ya kigoma ujiji.


Akizungumza na wananchi wa eneo hilo, Katibu wa ACT Mkoa Athuman Kabogo alidai lengo la kushusha bendera hiyo ni hatua ya kukataa kugeuzwa kuwa vibaraka wa watu wengine kwa kukosa haki ya kuhoji na kuwania nyadhifa za chama hicho na
hivyo kuanzisha ACT kama chama cha wanyonge kinachoweza kuwasikiliza na kutoa haki kwa kila mmoja.

Kabogo aliwataka wanachama wahitaji, wachukue kadi za ACT ili chama kipate usajili kamili kwa mujibu wa sheria,kanuni na taratibu husika pamoja na kutoa michango endelevu ,ikiwa ni jitihada za makusudi kuhakikisha chama kinasonga mbele
kwa maslahi ya Taifa.

�Wananchi nyie ni chachu ya chama kuwepo kwenye mchakato wa uchaguzi mdogo wa wenyeviti wa serikali za mitaa kwa kukiamini na kukipatia ridhaa kiweze kuleta
mabadiliko ya kimaendeleo� alisema Juma Ramadhan aliyekuwa katibu kampeni wa CUF kigoma.

Kwa upande wa Katibu ACT Kanda Magharibi Wiston Moga alisema, lengo la chama ni kuleta mabadiliko kwenye ulingo wa siasa,ambapo wao wamedhamiria kutetea maslahi ya umma kwa lengo la kuondoa mfumo wa maslahi binafsi ambayo ni chachu ya vyama vya siasa kushindwa kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi.

Katika ziara hiyo ya uzinduzi wa matawi ya chama husika,ACT kimefanikiwa kufungua matawi kwenye kata sita kati ya kata 19 zilizopo katika manispaa ya kigoma ujiji,huku baadhi ya viongozi kutoka UPD,CHADEMA na CUF wakijiunga na chama hicho
kwa kudai wanahitaji chama chenye uchungu na kukabiliana na changamoto za wanyonge.

Hata hivyo wanachama 3500 wa chama cha Democrasia na Maendeleo Chadema katika tawi la Ujiji mkoani Kigoma wamehamia chama kipya cha Alliance For Change and Transparency (ACT).