Mamilioni ya Airtel ‘Mimi ni Bingwa’ yaenda Bukoba
Dar es Salaam. Promosheni ya ‘Mimi ni Bingwa’
imemtangaza Rashid Jacob Kagombola, mkazi wa Bukoba mkoani Kagera kuwa
mshindi wa Sh50 milioni katika droo kubwa ya bahati nasibu
iliyochezeshwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania mwishoni mwa
wiki Dar es Salaam.
Akimtangaza mshindi huyo, Meneja Uhusiano wa
Airtel Tanzania, Jackson Mmbando alisema: “Leo hii tumefikia mwisho wa
Promosheni yetu ya ‘Mimi ni Bingwa’ ambayo imewanufaisha Watanzania
wengi. Limekuwa ni zoezi la mafanikio likishirikisha idadi kubwa ya
wateja waliojiunga katika promosheni hii iliyokuwa na vipengele
tofauti.”
“Ningependa kuwashukuru wateja wetu kwa kushiriki
promosheni hii tangu ilipoanza mwishoni mwa Novemba mwaka jana. Airtel
bado ina mipango mingine mingi inakuja, tukilenga kuendelea kurudisha
kile tulichonacho kwa wateja wetu na kuisaidia jamii inayotuzunguka
kukuza viwango vyao vya maisha.”
Alisisitiza kuwa mbali na zawadi hiyo ya Sh50
milioni kutolewa, washindi wa awamu ya pili na ya tatu wa safari
iliyogharimiwa kila kitu ya kwenda kuangalia mechi ya Klabu ya
Manchester United wataondoka nchini mwezi huu pale klabu hiyo
itakapocheza tena kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Naye mshindi wa Promosheni hiyo, Rashid Jacob,
akizungumza kwa njia ya simu kutoka Bukoba, aliipongeza Airtel Tanzania
kwa kuanzisha promosheni hiyo ambayo amedai imesaidia kubadili maisha ya
wateja wake na kuwa na mabadiliko chanya katika jamii na nchi nzima kwa
jumla.
“Hii ni miujiza inayotokea maishani mwangu. Siwezi
kuamini nami nimeingia katika orodha ya mamilionea Tanzania. Kwangu ni
kama kutimia kwa ndoto kwa sababu ya Airtel. Naishukuru Airtel Tanzania.
Hakika hizi milioni 50 zitabadilisha maisha yangu kabisa na zawadi
nitakayoipatia Airtel ni kubaki kuwa mteja wao mwaminifu wakati wote,”
alisema Kagombola.
Wakati wa promosheni hiyo, washiriki wawili wa
Mimi ni Bingwa wa kila siku walizawadiwa Sh2 milioni , wawili wa Sh5
milioni katika droo za kila wiki na mmoja tiketi mbili za safari
iliyogharimiwa kila kitu kwenda jiji la Manchester.
No comments:
Post a Comment