Wamisri wainyima ulaji Yanga
Mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu (jezi ya kijani) akiwania mpira na mabeki wa Al Ahly wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliozikutanisha timu hizo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita. Yanga ilishinda 1-0. Picha na Michael Matemanga.
Dar es Salaam. Klabu ya Yanga imepoteza dola 70,000 za
Kimarekani (Sh 111.2 milioni) baada ya kampuni ya MGB ya Misri kushindwa
kurusha moja kwa moja ‘Live’ mechi kati ya timu hiyo na Al Ahly
iliyochezwa Uwanja wa Taifa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Awali, Yanga iliingia mkataba wa Dola za Marekani
90,000 na kampuni hiyo kwa ajili ya kuonyesha mechi hiyo ya kwanza ya
raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania kucheza raundi ya
pili na ikapewa malipo ya awali dola 20,000.
Mwakilishi wa Kampuni ya MGB, Francis Gaitho
aliuambia mtandao wa Al Ahly.com kuwa wanailaumu Yanga kwa kukwamisha
zoezi la kurusha mechi hiyo, akidai waliwafukuza uwanjani wafanyakazi wa
televisheni ya Star TV na kamera zao waliokwenda kurusha moja kwa moja
pambano hilo.
Alisema baada ya kusaini mkataba na Yanga,
waliwalipa fedha za awali kutoka kwenye akaunti yao nchini Misri kwenda
kwenye akaunti ya klabu hiyo Tanzania.
Gaitho alisema timu ya watu wa utayarishaji
waliotakiwa kuja Dar es Salaam kurekodi mchezo huo ilishindwa kufika kwa
wakati kutoka Cairo, hivyo wakalazimika kutafuta kampuni ya Tanzania
kufanya kazi hiyo na Star TV ya Tanzania ikabahatika kupata zabuni
kutoka kwao.
Alisema kuwa licha wa ubalozi wa Misri nchini
Tanzania kuiandikia barua klabu ya Yanga kwamba MGB italipa malipo
yaliyobaki baada ya mechi na kudhaminiwa na Rais wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, uongozi wa Yanga iligoma kurekodiwa kwa
mechi hiyo.
“Wakati tulipofikia mwafaka na kukubaliana mechi
irekodiwe, kwa bahati mbaya Star TV walikuwa tayari wamekwishaondoka
uwanjani na muda ulikuwa umeenda,” alisema Gaitho.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya
Yanga, Mussa Katabaro akizungumzia madai hayo katika mahojiano na
mtandao wa Bin Zubery alikiri klabu hiyo kupokea malipo ya Dola 20,000
na kudai kuwa klabu yake ilipaswa kulipwa kiasi kingine cha Dola 35,000
kabla ya mechi na Dola 35,000 nyingine baada ya mechi, lakini MGB
ilishindwa kutekeleza kipengele hicho cha mkataba. “Mbaya zaidi, katika
mkataba wetu na wao tulikubaliana hakuna kupelekana mahakamani, sasa
tulipoona wameshindwa kulipa zile fedha.
Katabaro alisema wateja wao hawakuwa wa kweli
katika maelezo yao baada ya kudai kwamba kuna mtu alikuwa anakuja na
fedha kutoka Misri akakamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cairo
wakati si kweli.
Alisema baadaye walidai ubalozi wa Misri hapa
nchini utalipa hizo fedha, lakini ulipoulizwa ulikana na ndipo TFF
ilipojitolea kuwaandikia Yanga SC hundi ya dola 35,000 na dola 10,000
kwa Stars TV ili mechi ionyeshwe.
“Sisi tulikubali kupokea hundi ya TFF mechi
ionyeshwe, lakini Star TV wakagoma kupokea hundi ya TFF wakaondoka, sisi
hatukuwafukuza kama wanavyodai hao jamaa, kimsingi hawa jamaa
wametukosesha fedha dola 70,000.
“Kuna kampuni nyingine ya Misri ilijitokeza ikiwa
tayari kutupatia dola 100,000 kununua haki za TV za hiyo mechi, lakini
sisi tukaheshimu mkataba wetu na MGB, ila mwisho wa siku uungwana wetu
umetuponza,”alisema Katabaro
No comments:
Post a Comment