Tutatetea kwa nguvu uhuru wa habari-Mukajanga
Katibu wa Baraza la Habari Tanzania
(MCT), Kajubi Mukajanga amesema uwepo wa wanahabari na wadau wa habari
kwenye Bunge la Katiba kutasaidia kutetea kwa nguvu zake zote vipengele
vinavyotoa haki ya uhuru wa habari kwenye Rasimu ya Katiba.
Mukajanga, ambaye pia ni mmoja wa wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba, aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki kuwa
kupendekezwa kwa uhuru huo ni jambo moja na kupitishwa kwa vifungu hivyo
ni jambo jingine.
Kwa mujibu wa Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano, Ibara ya 31 (1) inapendekeza haki ya kila mtu kuwa na uhuru wa
kutafuta, kupata, kutumia na kusambaza habari na taarifa.
Pia Rasimu hiyo inatoa haki kwa mtu kuanzisha
vyombo vya habari na njia nyingine za upashanaji wa habari bila kujali
mipaka ya nchi na vitakuwa huru kupata, kutumia na kusambaza habari.
Kajubi, ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari,
alisema jambo kubwa ambalo tayari ameshalifanya ni kuwatambua wadau wa
habari ndani ya Bunge hilo, ambao atashirikiana nao katika kusukuma
agenda hiyo.
“Mapendekezo yetu karibu yote tuliyoyatoa mbele ya
Tume ya Jaji Warioba (Joseph) yameingizwa kwenye hii Rasimu. Jukumu
letu sisi (wajumbe) sasa ni kushawishi ili yaweze kupitishwa bungeni,”
alisema.
Kajubi pia alisema wadau wote wa habari, likiwemo
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na waandishi wenyewe, wana wajibu
mkubwa wa kushawishi kuhusu kupitishwa kwa ibara hizo.
Kwa mujibu wa rasimu hiyo, masuala mengine yaliyomo ni haki ya vyombo vya habari kuwa huru kusambaza taarifa kwa wananchi.
Pia kulinda utu, heshima na staha ya wananchi dhidi ya habari hizo.
Ibara ya 31(4) inaibana Serikali na taasisi zake,
asasi za kiraia na watu binafsi kuwa na wajibu wa kikatiba wa kutoa
habari kwa umma juu ya shughuli na utekelezaji wa shughuli zao.
No comments:
Post a Comment