Friday, 7 March 2014
Obama awasiliana na Putin kuhusu Ukraine
Mawasiliano kati ya Putin na Obama.
Rais Obama amefanya mazungumzo
zaidi ya kina na rais wa Urusi Vladmir Putin akisistiza kuwa vitendo vya
nchi yake katika jimbo la Crimea ni ukiukaji wa mipaka na uhuru wa
taifa la Ukraine.
Wakati wa mazungumzo yao ya pili kupitia njia ya
simu katika kipindi cha siku sita zilizopita, bwana Obama amependekeza
njia ya kusuluhisha mzozo huo kidiplomasia inayojumuisha Urusi kuwaondoa
wanajeshi wake katika jimbo la Crimea. Bwana Putin amesema uhusiano
kati ya Moscow na Washington haufai kutatizika kutokana na mzozo wa
Ukraine.Awali bwana alisema kuwa kura ya maoni iliyopendekezwa kuhusu jimbo la Crimea kujiunga na Moscow inakiuka sheria ya kimataifa na sharti ijumuishe serikali ya Kiev iwapo itaandaliwa.
Akizungumza baada ya mkutano mwingine wa Baraza la Usalama uliofanyika faraghani, balozi wa Uingireza katika umoja wa mataifa , Mark Lyall Grant, amesema haiwezekani muafaka kupatikana katika baraza hilo kuhusu mzozo huo.
Bunge la Crimea limepiga kura kujitenga na Urusi.
''Pengine kiwango fulani cha makubaliano kitaafikiwa ili kutuliza mgogoro huu na kisha baraza la usalama pengine litapata suluhu. Lakini hatujafutilia mbali mpango wa kuwasilisha azimio mbele ya Baraza la Usalama wakati wowote na tunafuatilia hali ya mambo kwa karibu tukitarajia baraza la Usalama likutane tena katika siku chache zijazo ikitegemea kitakachotokea mashinani."
Mzozo huo wa Ukraine umechochea wanasiasa pamoja na wageni wengine mashuhuri kususia mashindano ya Olimpiki ya wanariadha walemavu nchini Urusi. Marekani imeondoa ujumbe wake katika michezo hiyo na mawaziri wa Uingereza hawatakuwepo sawia na wenzao kutoka mataifa mengine ya Ulaya.
Wanadiplomasia watimuliwa Venezuela
Serikali ya Venezuela imemtimua Balozi wa Panama na wanadiplomasia wengine wakati huu kukiwa na maandamano ya upinzani nchini humo.
Maafisa hao walipewa saa 48 kuondoka nchini Venezuela.
Takriban watu 20 wameuawa wakati wa maandamano ya kuipinga serikali ya Venezuela mwezi uliopita.
Maduro ameishutumu Panama kupanga njama za kuiangusha serikali yake.
Raia wa Venezuela kwa muda mrefu wamekua wakilalamikia ongezeko la vitendo vya uhalifu, kupanda kwa gharama za maisha na ukosefu wa bidhaa muhimu.
Sasa malaria yakwea milima.
Kimelea kinachosababisha Malaria. Mbu hawapendi mazingira ya baridi.
Watafiti kutoka Uingereza na
Marekani wanasema kuwa mabadiliko ya hali ya hewa huenda yakazua
ongezeko kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kote duniani huku
ugonjwa huo ukienea katika maeneo ya milimani barani Afrika na Amerika
ya Kusini.
Katika matokeo ya utafiti yaliyochapishwa kwenye
jarida la Science, wanasayansi hao wanasema hata ongezeko dogo katika
viwango vya joto siku za usoni huenda likaongeza kwa mamilioni
maambukizi ya malaria.
Mbu anayesababisha malaria.
Watu wanaoishi katika maeneo ya nyanda za juu wanakosa kinga na hivyo kurahisisha maradhi ya malaria kuenea.
Takriban watu milioni mia mbili ishirini kote duniani huambukizwa ukonjwa wa malaria.
Mnyika atishia kuwataja vigogo
Wakati
huohuo, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika ametishia
kuwataja kwa majina vigogo wa Serikali na CCM aliosema wako nyuma ya
‘kashfa’ kuhusu mgogoro huo ili waweze kuhojiwa kwa umma iwapo Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo hatajitokeza kufafanua
kauli alizozitoa bungeni kutuhumu IPTL.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema),
alisema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, akimtuhumu
Waziri Muhongo kwa kudai bungeni Mei 25, 2013 kuwa yeye hakutumwa
wizarani kupekua mafaili ili kufuatilia mlolongo wa kesi za IPTL.
Alisema anachukua hatua hiyo kwa kuzingatia kwamba
madaraka na mamlaka ni ya wananchi... “Serikali inafanya kazi kwa niaba
ya wananchi; hivyo pale Serikali inapochelewa kuchukua hatua kutokana
na udhaifu, uzembe, ufisadi au uongo, ni muhimu wananchi wakashiriki
kutaka uwajibikaji.”
Wavuvi: Mradi wa gesi unatupunguzia samaki baharini
Katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili sasa upatikanaji wa
samaki wa kitoweo katika pwani ya Bahari ya Hindi, eneo la Mkoa wa
Mtwara, umekuwa mgumu.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya
hivi karibuni, umebaini kuwa mabadiliko ya hali ya hewa na zana duni za
uvuvi zinachangia hali hiyo.
Lakini wakazi wa Mtwara ambao baadhi yao
wanategemea uvuvi, wanaamini kuwa upungufu wa samaki, umechangiwa na
ongezeko kubwa la mahitaji ya samaki tofauti na uwezo wa wavuvi
kulilisha soko la walaji.
Pamoja na wavuvi kukiri kuongezeka kwa soko la
samaki, wanasema upatikanaji wake umekuwa mgumu hata kwa wale
wanaotumia zana nzuri katika uvuvi.
Wavuvi wanaamini kuwa uchimbaji wa nishati ya gesi
asilia imesababisha mabadiliko ya hali ya hewa baharini kutokana na
matumizi ya kemikali za kulipua ndani ya bahari wakati wa utafiti na
uchimbaji.
“Hapo awali kabla ya kuanza uchimbaji wa gesi
asilia baharini, tulikuwa na upepo wa matalai, upepo wa mlaji na upepo
wa umande. Pepo hizo zilikuwa mwongozo kwetu kwenye shughuli zetu za
uvuvi,” anasema Ali Hamis Kimbaumbau, mvuvi na mkazi wa mjini Mtwara.
Anafafanua kuwa pepo za matalai na umande ambazo
ni upepo wa kusini huwa ni shwari na zikiambatana na upepo ambao ulikuwa
unatoa fursa kwa wavuvi wanaotumia mitumbwi kwenda baharini. Kipindi
hicho wavuvi walikuwa wanapata samaki ingawa si kwa kiwango kikubwa.
Anabainisha kuwa kwa sasa pepo wanazopata ni za
kaskazi ambazo huambatana na upepo mkali, hali inayozuia wavuvi wenye
mitumbwi isiyotumia mashine kushindwa kwenda baharini. Wavuvi
wanaofanikiwa kwenda baharini hurudi na mapato duni.
Mvuvi mwingine, Salumu Liwanje (36) anasema
wamefikia hatua ya kuamini utafiti na uchimbaji wa gesi asilia baharini
ndiyo chanzo.
Anaeleza kuwa siku moja wakiwa baharini, eneo la
Luvula walibaini nyaya zenye umeme baharini na walirushwa wakati
walipojaribu kugusa maji hayo. Alisema baadaye walisikia sauti ya
milipuko mara kadhaa hali waliyodai inaharibu mazingira ya asili ya
bahari.
“Joto limeongezeka sana baharini. Hiyo hali si ya
kawaida, ukiingia bahari kuu utakutana na joto ambalo si la kawaida
kabisa. Sisi tulizoea nyakati za usiku baharini kunakuwa na baridi kali,
lakini hali ni kinyume kwa sasa,” anabainisha Liwanje.
“Unajua wengine tukisema mabadiliko tunayoyaona
wapo, watakaosema ni walewale wasiopenda mradi wa gesi. Sasa sisi kama
wavuvi tukigusa yale maji yaliyotandazwa nyaya tunarushwa na umeme, je
samaki wataishi eneo hilo? ” anahoji mvuvi huyo.
Wafanyakazi Muhimbili walilia Sh800 mil zao
Dar es Salaam. Wafanyakazi wa Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili (MNH) wameulalamikia uongozi wa hospitali hiyo kwa
kushindwa kuwalipa fedha zao na kuzitumia kinyume na utaratibu
uliopangwa.
Fedha zinazotajwa kutolipwa ni pamoja na Sh800
milioni za posho ya awamu ya tatu zinazotokana na mapato ya wateja wa
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambazo imedaiwa zilitumika kununulia
vifaa tiba vya hospitali hiyo na fedha za likizo za tangu mwaka jana.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyakazi hao
walisema hawajalipwa posho hizo tangu Januari, 2013 baada ya kuelezwa na
mkurugenzi wa hospitali hiyo kuwa fedha hizo zitaelekezwa kununulia
vifaa vya hospitali.
“Tunashindwa kuelewa hawa viongozi wetu! wanatumia
fedha kwa maelekezo tofauti, hii inasababisha kuwapo na migogoro ndani
ya kazi,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Mtoa habari huyo alisema wafanyakazi wameshangazwa
na kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Marina Njelekela
kudai hawatalipwa posho na kwamba fedha hizo zitanunulia vifaa.
“Tunatakiwa kulipwa fedha hizo kama tahadhari.
Mfano unaweza ukamuhudumia mgonjwa wa Ukimwi na ikatokea katika kumtibia
akakuambukiza hela hii unayolipwa ndiyo kazi yake,” alisema.
Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha alikiri uongozi wa MNH kutumia fedha hizo kwa matumizi mengine.
Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii, Dk. Seif Rashid
alisema alipata taarifa hizo na walikaa kikao na Bodi, mkurugenzi na
chama cha Tughe kujadiliana suala hilo kwa kuwa ni la kisheria zaidi.
“Hili suala lipo kisheria zaidi. Niliwaagiza
waende wakakae pamoja wajadiliane waweze kupata mwafaka ili wawalipe
wafanyakazi hao,” Dk. Seif.
Subscribe to:
Posts (Atom)





