Tuesday, 4 March 2014

BREAKING NEWSSS!! LIZIWANI KIKWETE ASHINDA KURA ZA MAONI ZA UBUNGE CHALINZE

  

 
Ndg.Ridhiwani Kikwete Mgombea wa ubunge katika Kura za Maoni za CCM jimbo la Chalinze akijipigia Kura leo.
 
...akipanga mstari (katikati) katika uwakilishi wa Kata anayotoka ya Msoga.
Matokeo:
Ridhiwani Kikwete kashinda kwa kupata kura 758 kati ya kura 1321,
Ilikuwa hivi:_
1.Ridhiwani Kikwete kura 758
2.Shaban Iman Madega kura 335
3.Athuman Ramadhan Maneno kura 206
4.Changwa Mohamed mkwazu kura 12
Kura zilikuwa 1363 zilizo Haribika 5 na Halali ni kura 1316
Wagombea wa Ubunge Chalinze kwa tiketi ya ccm walikuwa ni:-
1.Ndg.Ridhiwani Kikwete,
2.Shaban Iman Madega,
3.Athuman Ramadhan Maneno
4.Changwa Mohamed mkwazu
Tarehe 9/3/2014 KUCHUKUA FOMU
Tarehe 11/3/2014 KURUDISHA
Tarehe 15/3/2014UZINDUZI RASMI WA KAMPENI ZA CCM

Tutatetea kwa nguvu uhuru wa habari-Mukajanga

 

Katibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga amesema uwepo wa wanahabari na wadau wa habari kwenye Bunge la Katiba kutasaidia kutetea kwa nguvu zake zote vipengele vinavyotoa haki ya uhuru wa habari kwenye Rasimu ya Katiba.
Mukajanga, ambaye pia ni mmoja wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki kuwa kupendekezwa kwa uhuru huo ni jambo moja na kupitishwa kwa vifungu hivyo ni jambo jingine.
Kwa mujibu wa Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 31 (1) inapendekeza haki ya kila mtu kuwa na uhuru wa kutafuta, kupata, kutumia na kusambaza habari na taarifa.
Pia Rasimu hiyo inatoa haki kwa mtu kuanzisha vyombo vya habari na njia nyingine za upashanaji wa habari bila kujali mipaka ya nchi na vitakuwa huru kupata, kutumia na kusambaza habari.
Kajubi, ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, alisema jambo kubwa ambalo tayari ameshalifanya ni kuwatambua wadau wa habari ndani ya Bunge hilo, ambao atashirikiana nao katika kusukuma agenda hiyo.
“Mapendekezo yetu karibu yote tuliyoyatoa mbele ya Tume ya Jaji Warioba (Joseph) yameingizwa kwenye hii Rasimu. Jukumu letu sisi (wajumbe) sasa ni kushawishi ili yaweze kupitishwa bungeni,” alisema.
Kajubi pia alisema wadau wote wa habari, likiwemo Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na waandishi wenyewe, wana wajibu mkubwa wa kushawishi kuhusu kupitishwa kwa ibara hizo.
Kwa mujibu wa rasimu hiyo, masuala mengine yaliyomo ni haki ya vyombo vya habari kuwa huru kusambaza taarifa kwa wananchi.
Pia kulinda utu, heshima na staha ya wananchi dhidi ya habari hizo.
Ibara ya 31(4) inaibana Serikali na taasisi zake, asasi za kiraia na watu binafsi kuwa na wajibu wa kikatiba wa kutoa habari kwa umma juu ya shughuli na utekelezaji wa shughuli zao.

 

Wana-CCM Dodoma waonya wajumbe

Dodoma. Chama cha Mapinduzi, Kata ya Chang’ombe katika Manispaa ya Dodoma kimeonya kuwa Katiba mpya isipotoa matumaini ya wananchi kupimiwa ardhi, hawataitambua na hawatakuwa tayari kupiga kura ya kuchagua kiongozi yeyote katika maeneo yao.
Wanachama wa chama hicho walitoa kauli hiyo katika kikao chao kilichofanyika Tawi la Mji Mwema.
Walisema Serikali kupitia Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) imewahadaa na kwamba matumaini yao sasa yako ndani ya Katiba.
Wananchi hao pia waliushutumu uongozi wa CCM wa Mkoa wa Dodoma kwa madai ya kushirikiana na CDAkuwanyima haki zao.
Hata hivyo, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Albert Mgumba alikanusha madai hayo na kueleza kwamba chama hicho kinafanya kila njia kupigania haki za wananchi hao.
Mgumba alisema mfumo wa CDA ndiyo tatizo kubwa na kwamba hiyo inachangiwa na muundo wake.
Mwenyekiti wa CCM wa Tawi la Mji Mwema, Hussein Binde alisema wamekuwa wakidanganywa kuwa watapimiwa ardhi yao lakini hakuna kilichofanyika.

 

Wamisri wainyima ulaji Yanga 

Mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu (jezi ya kijani) akiwania mpira na mabeki wa Al Ahly wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliozikutanisha timu hizo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita. Yanga ilishinda 1-0. Picha na Michael Matemanga.  

Dar es Salaam. Klabu ya Yanga imepoteza dola 70,000 za Kimarekani (Sh 111.2 milioni) baada ya kampuni ya MGB ya Misri kushindwa kurusha moja kwa moja ‘Live’ mechi kati ya timu hiyo na Al Ahly iliyochezwa Uwanja wa Taifa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Awali, Yanga iliingia mkataba wa Dola za Marekani 90,000 na kampuni hiyo kwa ajili ya kuonyesha mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania kucheza raundi ya pili na ikapewa malipo ya awali dola 20,000.
Mwakilishi wa Kampuni ya MGB, Francis Gaitho aliuambia mtandao wa Al Ahly.com kuwa wanailaumu Yanga kwa kukwamisha zoezi la kurusha mechi hiyo, akidai waliwafukuza uwanjani wafanyakazi wa televisheni ya Star TV na kamera zao waliokwenda kurusha moja kwa moja pambano hilo.
Alisema baada ya kusaini mkataba na Yanga, waliwalipa fedha za awali kutoka kwenye akaunti yao nchini Misri kwenda kwenye akaunti ya klabu hiyo Tanzania.
Gaitho alisema timu ya watu wa utayarishaji waliotakiwa kuja Dar es Salaam kurekodi mchezo huo ilishindwa kufika kwa wakati kutoka Cairo, hivyo wakalazimika kutafuta kampuni ya Tanzania kufanya kazi hiyo na Star TV ya Tanzania ikabahatika kupata zabuni kutoka kwao.
Alisema kuwa licha wa ubalozi wa Misri nchini Tanzania kuiandikia barua klabu ya Yanga kwamba MGB italipa malipo yaliyobaki baada ya mechi na kudhaminiwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, uongozi wa Yanga iligoma kurekodiwa  kwa mechi hiyo.
“Wakati tulipofikia mwafaka na kukubaliana mechi irekodiwe, kwa bahati mbaya Star TV walikuwa tayari wamekwishaondoka uwanjani na muda ulikuwa umeenda,” alisema Gaitho.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Mussa Katabaro akizungumzia madai hayo katika mahojiano na mtandao wa Bin Zubery alikiri klabu hiyo kupokea malipo ya Dola 20,000 na kudai kuwa klabu yake ilipaswa kulipwa kiasi kingine cha Dola 35,000 kabla ya mechi na Dola 35,000 nyingine baada ya mechi, lakini MGB ilishindwa kutekeleza kipengele hicho cha mkataba. “Mbaya zaidi, katika mkataba wetu na wao tulikubaliana hakuna kupelekana mahakamani, sasa tulipoona wameshindwa kulipa zile fedha.
Katabaro alisema wateja wao hawakuwa wa kweli katika maelezo yao baada ya kudai kwamba kuna mtu alikuwa anakuja na fedha kutoka Misri akakamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cairo wakati si kweli.  
Alisema baadaye walidai ubalozi wa Misri hapa nchini utalipa hizo fedha, lakini ulipoulizwa ulikana na ndipo TFF ilipojitolea kuwaandikia Yanga SC hundi ya dola 35,000 na dola 10,000 kwa Stars TV ili mechi ionyeshwe.
“Sisi tulikubali kupokea hundi ya TFF mechi ionyeshwe, lakini Star TV wakagoma kupokea hundi ya TFF wakaondoka, sisi hatukuwafukuza kama wanavyodai hao jamaa, kimsingi hawa jamaa wametukosesha fedha dola 70,000.
“Kuna kampuni nyingine ya Misri ilijitokeza ikiwa tayari kutupatia dola 100,000 kununua haki za TV za hiyo mechi, lakini sisi tukaheshimu mkataba wetu na MGB, ila mwisho wa siku uungwana wetu umetuponza,”alisema Katabaro

 

Mwelekeo mpya bungeni, Pinda atoa hoja kutuliza hali ya hewa

Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alifanikiwa kutuliza hali ya hewa bungeni baada ya kutoa mapendekezo yaliyoungwa mkono na pande zote zilizokuwa zinavutana kuhusu kupitisha baadhi ya vifungu vya Kanuni za Bunge la Katiba. 

 

Katika mapendekezo yake yaliyoungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa CCM -Zanzibar, Vuai Ali Vuai, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Pinda alisema: “Nataka kuwaomba wenzangu wote kwenye maeneo hayo (yenye malumbano) tukiwa tunayapitia kama hatutaelewana tuyaache kwa muda na kumwomba Mwenyekiti aunde timu ya watu wazima na wenye busara wajaribu kuyatazama. “Tujadiliane, tushindane kwa lugha za staha, tusitumie lugha inayoweza kukasirisha. Isiwe mimi nimesema, mimi nimesema...”
Waziri Mkuu, aliwataka wajumbe wajiepushe na lugha za kuudhi ambazo zinaweza kukwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya.
Pinda alilazimika kuingilia kati baada ya kutokea mgawanyiko mkubwa wa namna ya kupiga kura kupitisha vifungu vya rasimu.
Akiunga mkono ushauri huo, Mbowe alisema Bunge limejaa hisia za hofu ndani na nje, jambo ambalo linatia wasiwasi wa kupatikana kwa Katiba Mpya. Alisema iwapo wajumbe watashirikiana na kuweka kando masilahi ya vyama, idadi yao katika makundi, Katiba inaweza kupatikana.
Vuai alionya kuhusu matumizi ya lugha za kuudhi huku Profesa Lipumba akiwataka wajumbe kuzingatia masilahi ya Taifa kama alivyoagiza Rais Jakaya Kikwete na kutengeneza Katiba ya Watanzania wote bila ya kujali masilahi binafsi.
Upigaji kura bungeni vita
Awali, mjadala wa utaratibu wa upigaji kura katika Bunge hilo ulichukua sura mpya baada ya kudaiwa kuwapo ushawishi unaohusisha utoaji wa bahasha ili kutaka kuungwa mkono katika misimamo inayokinzana.
Habari zilizopatikana zilidai kuwa watuhumiwa katika sakata hilo ni baadhi ya wajumbe ambao ni mawaziri na mbunge mmoja wa CCM. Vigogo hao wanadaiwa kuwashawishi wajumbe ambao hawatokani na vyama vya siasa ili kupitisha agenda ya kura ya wazi kirahisi.
Akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, Mjumbe wa Bunge hilo, Julius Mtatiro ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF, alisema: “Jaribio la kuzuia kura ya siri limechukua njia za aibu, baada ya CCM kutumia fedha kushawishi wajumbe.”
Katika ujumbe huo ambao alikiri kuuandika, Mtatiro aliwataja wajumbe watatu ambao ni mawaziri kuwa waliwakaribisha wajumbe kwenye makazi yao na “kuwaandalia chakula cha kutosha, vinywaji vya kutosha na viburudisho vingine, huku wakipewa bahasha za nauli baada ya vikao hivyo vya siri.” Mmoja wa waliotajwa ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe aliyedaiwa kuwaalika wawakilishi wa wafugaji na kuwapa chakuka na bahasha.
Akijibu tuhuma hizo, pamoja na kukiri kuwakaribisha baadhi ya wajumbe na kula nao chakula, alikana tuhuma za kuwahonga ili waunge mkono msimamo wa chama hicho. Alisema Mtatiro amemdhalilisha, hivyo anawasiliana na mwanasheria wake ili kumfikisha mahakamani.

 

 

Wabunge wa Libya washambuliwa 

Wabunge wawili nchini Libya walipigwa risasi na kuumizwa baada ya kundi la waandamanaji kuwashambulia bungeni katika mji mkuu wa Tripoli.
Walioshuhudia tukio hilo, walisema kuwa wawili hao walipigwa risasi walipojaribu kutoroka kutoka katika eneo hilo.
 
Waandamanaji hao waliokuwa na ghadhabu walilishambulia bunge hilo, huku wakitaka bunge lifungwe na tarehe mpya ya uchaguzi wa mapema itangazwe.
Kumekuwa na wimbi la maandamano nchini humo kutokana na uamuzi wa bunge la nchi hiyo kuahirisha tarehe ya uchaguzi hadi baadaye mwakani.
Waliolishambulia bunge siku ya Jumapili walisema kuwa walighadhabishwa pia na “kutekwa nyara” kwa waandamanaji waliokuwa na kikao nje ya bunge.
Walisema kuwa waliohusika na utekaji nyara huo walikuwa chini ya uongozi wa waasi wanaotumikia amri ya bunge.
Waandamanaji hao ambao wengi wao ni vijana walijihami kwa visu na vijiti,wakalishambulia bunge huku wakiwa na ujumbe kwa wabunge kwa kuimba “jiuzulu,jiuzulu”, kwa mujibu wa taarifa ya ashirika la habari la AFP.
Bunge la nchi ya Libya limeshambuliwa mara kadhaa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Nuri Abu Sahmein ambaye ni spika wa bunge hilo aliambia kituo cha televisheni cha Al-Nabaa kuwa maandamano yaliyokuwa ya amani, yalivurugwa na watu waliojihami.
"Wabunge wawili walipigwa risasi pale walipojaribu kutoweka mahali hapo kwa kutumia magari yao,” alisema.
Haikuwezakana kubaini papo hapo idadi ya wabunge walioumia.
Picha zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha waandamanaji wakivuta kile kilichokusudiwa kuwa kiti cha Spika wa bunge hilo nje ya bunge na kukichoma.
Mwandishi wa BBC Rana Jawad ambaye yuko Tripoli anasema kuwa bunge la Libya limeshambuliwa mara kadhaa na makundi tofauti, yakiwemo makundi ya waasi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Uchaguzi uliokuwa wa amani ulifanywa na nchi ya Libya katika mwezi wa Julai mwaka jana, ila bado nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ingali inang’ang’ana kupata utulivu, miaka mitatu baadaye tangu kufurushwa kutoka maamlakani kwa aliyekuwa rais, hayati Muammar Gaddafi.

 

Kirusi bwete chazinduka

Taarifa ya kirusi aina ya Pithovirus sibericum ambacho kimekuwa bwete kwa miaka zaidi ya 30,000 hadi kilipopelekwa tena kwenye mabara nchini Ufaransa imeendelea kuwa taarifa kuu.

kirusi cha Pithovirus sibericum 

Kirusi hicho cha kale kimerejesha uhai wake baada ya kukaa bwete kwa miaka zaidi ya elfu 30,000 , walieleza wanasayansi .
Kilipatikana kikiwa kimezama kwenye utando wa barafu katika eneo la Siberia, lakini baada ya kuzinduliwa kikawa tena na uwezo wa kusababisha maambukizi .
Wanasayansi wa Ufaransa wanasema hata hivyo kirusi hicho si hatari kwa maisha ya binadamu na wanyama , lakini hii inaonyesha kuwa virusi wengine wanaweza kuzinduka hata baada ya kuwa bwete kwa muda mrefu.
Taarifa ya utafiti huo ilichapishwa katika kituo cha kitaifa cha sayansi nchini Ufaransa (PNAS).
Professor Jean-Michel Claverie, wa kituo cha utafiti (CNRS) katika chuo kikuu cha Aix-Marseille nchini France, alisema: " Hii ni mara ya kwanza tumeona kirusi ambacho bado kina maambukizi baada ya kipindi kirefu kama hiki.
Kirusi hiki ambacho ni kikubwa kinaweza kuonekana kwa macho tofauti na virusi vingine vinavyoonekana tu kwa kutumia microscope, na kilipatikana kikiwa kimezikwa mita 30 chini kwenye barafu iliyoganda.
Wanasayansi wanasema kubainika kwa kirusi cha Pithovirus sibericum kunaonyesha hatari kwamba virusi vya maambukizi vinavyodhaniwa kuwa vimekufa vinaweza kuibuka tena baada ya miaka mingi na kusababisha maambukizi kutokana na shughuli za binadamu.