Wednesday, 5 March 2014

Singapore mji ghali zaidi duniani

Singapore umetajwa kuwa mji ghali zaidi duniani kuishi kwa mwaka 2014 na kuipiku miji mingine 131 kwa mujibu wa taarifa ya Economist Intelligence Unit (EIU).

 

Nguvu ya sarafu ya mji huo ikiwa ni pamoja na gharama kubwa ya uendeshaji magari na kuongezeka kwa malipo ya huduma za umma kumechangia Singapore kuwa juu ya miji yote duniani kwa ughali wa maisha.

Pia ni mahali ambapo nguo zinauzwa kwa bei ya juu kabisa kuliko miji yote duniani.
Singapore imechukua nafasi ya mji wa Tokyo, amao ulikuwa unaongoza kwa ughali wa maisha mwaka 2013.
Miji mingine mitano inayoongoza kwa gharama kubwa za maisha duniani ni pamoja na Paris, Oslo, Zurich na Sydney, huku Tokyo ukiporomoka hadi nafasi ya sita.
Mji wa New York unatumiwa kama kigezo cha utafiti wa shirika la EIU kuhusu gharama za maisha katika miji mbalimbali duniani. Wanaangalia zaidi ya bei binafsi 400.

 

Magari ya umma yavuruga shughuli Nairobi

Huduma za usafiri jijini Nairobi zimekwama kufuatia hatua za wenye magari kugoma hii leo wakilalamikia nyongeza ya ada ya kuegesha magari jijini humo
.
Mgomo wa wahudumu wa magari nchini Kenya

Maelfu ya wafanyakazi wamelazimika kutembea kwa miguu na wasafiri wa kutoka jijini kwenda maeneo ya mashambani nao kulazimika kuahirisha safari zao.
Mwenyekiti wa wenye matatu katika eneo la Mlima Kenya, Bwana Michael Kariuki, ambaye aliongea na BBC akiwa nje ya lango la kuingia kwenye afisi ya Gavana wa Kaunti ya Nairobi, alisema mzozo uliopo ni mdogo na waweza kusuluhishwa haraka.
"Juzi tulikuwa na Gavana Evans Kidero na tukakubaliana kiasi tunachopaswa kulipa lakini jana tulipofika wafanyakazi wa kaunti wakakataa kiasi tulichokuwa nacho," Bwana Kariuki alisema.
Jiji la Nairobi ni mojawapo wa kaunti ambazo zimebuniwa chini ya Katiba iliyopitishwa na wapiga kura na kuidhinishwa mwaka 2010 katika hatua ya kuimarisha huduma kwa wananchi.
Kaunti hizo mpya hata hivyo zimejikuta njia panda baada ya kupata madaraka bila fedha za kuandamana nayo; ambapo zimelazimika kuongeza kodi kama njia mojawapo ya kujiimarisha kiuchumi.

Tuesday, 4 March 2014

Mamilioni ya Airtel ‘Mimi ni Bingwa’ yaenda Bukoba

Dar es Salaam. Promosheni ya ‘Mimi ni Bingwa’ imemtangaza Rashid Jacob Kagombola, mkazi wa Bukoba mkoani Kagera kuwa mshindi wa Sh50 milioni katika droo kubwa ya bahati nasibu iliyochezeshwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania mwishoni mwa wiki Dar es Salaam.
Akimtangaza mshindi huyo, Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando alisema: “Leo hii tumefikia mwisho wa Promosheni yetu ya ‘Mimi ni Bingwa’ ambayo imewanufaisha Watanzania wengi. Limekuwa ni zoezi la mafanikio likishirikisha idadi kubwa ya wateja waliojiunga katika promosheni hii iliyokuwa na vipengele tofauti.”
“Ningependa kuwashukuru wateja wetu kwa kushiriki promosheni hii tangu ilipoanza mwishoni mwa Novemba mwaka jana. Airtel bado ina mipango mingine mingi inakuja, tukilenga kuendelea kurudisha kile tulichonacho kwa wateja wetu na kuisaidia jamii inayotuzunguka kukuza viwango vyao vya maisha.”
Alisisitiza kuwa mbali na zawadi hiyo ya Sh50 milioni kutolewa, washindi wa awamu ya pili na ya tatu wa safari iliyogharimiwa kila kitu ya kwenda kuangalia mechi ya Klabu ya Manchester United wataondoka nchini mwezi huu pale klabu hiyo itakapocheza tena kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Naye mshindi wa Promosheni hiyo, Rashid Jacob, akizungumza kwa njia ya simu kutoka Bukoba, aliipongeza Airtel Tanzania kwa kuanzisha promosheni hiyo ambayo amedai imesaidia kubadili maisha ya wateja wake na kuwa na mabadiliko chanya katika jamii na nchi nzima kwa jumla.
“Hii ni miujiza inayotokea maishani mwangu. Siwezi kuamini nami nimeingia katika orodha ya mamilionea Tanzania. Kwangu ni kama kutimia kwa ndoto kwa sababu ya Airtel. Naishukuru Airtel Tanzania. Hakika hizi milioni 50 zitabadilisha maisha yangu kabisa na zawadi nitakayoipatia Airtel ni kubaki kuwa mteja wao mwaminifu wakati wote,” alisema Kagombola.
Wakati wa promosheni hiyo, washiriki wawili wa Mimi ni Bingwa wa kila siku walizawadiwa Sh2 milioni , wawili wa Sh5 milioni katika droo za kila wiki na mmoja tiketi mbili za safari iliyogharimiwa kila kitu kwenda jiji la Manchester.

 

Kardinali Pengo aweka wazi msimamo wa Kanisa

 Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo akiwaonesha waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, nakala ya gazeti la Mwanachi lililoandika habari kuhusu msimamo wa Kanisa juu ya suala la serikali tatu. Picha na Venance Nestory  

Dar es Salaam/Iringa. Siku mbili baada ya Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kutoa waraka wa kulitaka Bunge Maalumu la Katiba kutopuuza mapendekezo ya muundo wa serikali tatu, Askofu Mkuu wa Jimbo Mkuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameibuka na kusema msimamo huo siyo wa Kanisa Katoliki nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kardinali Pengo pamoja na kukiri kuwa tume ilitoa maoni hayo, alikanusha kuwa taarifa zilizotolewa na moja ya magazeti kuwa msimamo wa Kanisa Katoliki ni serikali tatu.
“Maoni ya Tume hayawezi kuwa ni msimamo wa kanisa. Kanisa Katoliki lina utaratibu wa kutoa misimamo yake na huwa inatolewa na Mwenyekiti wa TEC,” alisema.
Hata hivyo, Rais wa TEC, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kutoka Jimbo la Iringa, alisema jana kuwa alikuwa na shughuli nyingi, hivyo asingeweza kuzungumzia suala hilo, labda wiki ijayo.
Akizungumza katika makazi yake mjini Iringa, Askofu Ngalalekumtwa alisema: “Mniache, nina shughuli nyingi…labda mnitafute wiki ijayo,” alisema.
Vilevile, Pengo ambaye alirejea msimamo wake binafsi wa kuunga mkono Muungano wa serikali mbili, alisema kwa namna Rasimu ya Katiba ilivyo, hakuna kigezo cha kulazimisha Kanisa Katoliki litoe msimamo.
Alisema Kanisa Katoliki lingeweza kutoa msimamo iwapo Rasimu ya Katiba ingekuwa na dosari zinazohusu imani au maadili.
“Kwa mfano, (Rasimu) ingekuwa inasema, hakuna Mungu lazima tungekuja juu kwa sababu inaingilia imani yetu,” alisema Kardinali Pengo na kufafanua:
“Vilevile tungeweza kusema inakwenda kinyume na maadili iwapo inaruhusu kuua wazee au inaunga mkono ndoa za jinsi moja.”
Tamko la Tume
Tamko la tume hiyo inayoongozwa na Askofu Mkuu wa Tabora, Paulo Ruzoka liliweka bayana kuwa muundo wa serikali mbili haukutatua matatizo ya msingi na badala yake ulilimbikiza kero zilizosababisha Zanzibar kujiundia katiba yake mwaka 2010 bila kushauriana na Tanzania Bara.
Tamko hilo la kurasa 15 lililosambazwa kwa baadhi ya Wajumbe wa Bunge la Katiba, lilitolewa baada ya mkutano wa kitaifa wa Wajumbe wa Kamati za Majimbo za Haki na Amani za Kanisa hilo na Chama cha Wanataaluma Wakatoliki Tanzania (CPT), uliofanyika jijini Dar es Salaam Februari 5 na 6 mwaka huu.

 

Sitta apiga jaramba kuongoza Bunge

 

Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho, akizungumza na mjumbe wa Bunge hilo, Samuel Sitta (kushoto), ndani ya Ukumbi wa Bunge, Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman   

Dodoma. Siku moja baada ya kuteuliwa na CCM kuwania uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema ameanza kupitia sheria na kanuni zitakazomwezesha kuliongoza huku akiahidi kutenda haki kwa wajumbe wote iwapo atachaguliwa.
Akizungumza mjini Dodoma jana, Sitta alisema: “Nawashukuru wote waliokuwa wakiniunga mkono na niseme wazi kuwa nitatenda haki kwa wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba.”
Alisema kazi kubwa aliyonayo baada ya uteuzi huo ni kuhakikisha kuwa anazipitia sheria na kanuni zinazoongoza bunge hilo na sheria nyingine kwa kuwa ndizo nyenzo zake za utendaji kazi.
Akizungumzia mchakato wa uteuzi ndani ya chama hicho na mchuano uliokuwapo kati yake na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge alisema: “Hii ni hatua ya awali na ya kawaida tu ndani ya CCM. Mara nyingi chama changu kikiona kuna mambo yanayoleta msuguano, basi huamua kuteua jina moja kwa ajili ya kugombea. Wameteua majina mawili kwa demokrasia kabisa. Ninakishukuru chama changu kwa kuniteua na kwa sasa najiandaa na uchaguzi.”
Suluhu: Nitafanya maajabu
Kwa upande wake, Mjumbe wa bunge hilo aliyeteuliwa na CCM kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassan aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba ana uwezo mkubwa wa kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba na hana shaka katika uteuzi wake.
Samia ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), alijisifu akisema ana rekodi nzuri ambayo haitiliwi shaka kwa weledi wake na haoni tatizo kwa yeye kupewa nafasi hiyo.
“Nina rekodi nzuri ya kuongoza Serikali kwa muda mrefu na sijapata doa lolote, kwa hiyo sioni ugumu wowote,” alisema.
Samia aliwahi pia kuwa Waziri wa Ajira na Wanawake na baadaye, Waziri wa Utalii katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kabla ya kuwa Waziri wa Nchi, katika Ofisi ya Makamu wa Rais.
Kinana na mchakato
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alizungumzia mchakato uliompitisha Sitta kuwania nafasi hiyo na kusema ulilenga kuzuia mgawanyiko ndani ya chama.
Hata hivyo, alisema Chenge aliamua kwa hiari yake kujitoa baada ya kukubaliana na Sitta walipoitwa na uongozi wa chama kwa ushauri. Akizungumza katika mahojiano maalumu mjini Dodoma, Kinana alisema: “Kiutaratibu, yeyote ilimradi awe mjumbe wa Bunge la Katiba, angeweza kujitokeza kugombea uenyekiti. CCM, walijitokeza wawili walionyesha nia; Sitta na Chenge.






Mauaji zaidi yatokea Nigeria



Ghasia zaidi zimetokea Kaskazini Mashariki mwa Nigeria ambapo watu 13 wameuawa.
Mkaazi wa kijiji cha Jakana karibu na mji wa Maiduguri jimbo la Borno amesema takriban watu 40 wameuawa katika shambulio lililofanywa na kundi la Boko Haram JUmatatu usiku.
Kaskazini mwa Nigeria imeshuhudia mashambulio ya kundi la Boko Haram licha ya operesheni ya jeshi inayoendelea.
Hapo Jumapili usiku watu 30 waliuawa katika shambulio mji wa Mafa na watu wengine 90 waliuawa katika siku ya Jumamosi katika shambulio la bomu mjini Maiduguri.

Keqiang asema mageuzi ni sharti China 


Li Keqiang akihutubia bunge la Uchina.
Waziri mkuu wa China, Li Keqiang, ameuambia mkutano wa kila mwaka, wa bunge la taifa hilo mjini Beijing, kwamba maendeleo ya kiuchumi yanasalia kuwa jukumu kubwa zaidi la serikali, lakini marekebisho ya kimsingi ni sharti yatekelezwa japo ni machungu.
Bwana Li amewaambia maelfu ya wajumbe katika bunge la taifa hilo, Great Hall of the People, kwamba shabaha ya kila mwaka ya ukuaji wa kiuchumi itasalia kuwa asilimia saba nukta tano.
Akizungumzia tatizo la uchafuzi, amesema kuwa moshi mkubwa unaondelea kutanda katika miji mikubwa ya China, ni onyo la kiasili dhidi ya maendeleo yasiokuwa na mpango.
Waziri huyo mkuu wa China kadhalika ametangaza marufuku dhidi ya majengo mapya ya serikali kama sehemu ya kile alichokitaja kuwa mapambano bila huruma dhidi ya ufisadi.