WAWILI WAONDOLEWA BUNGE LA KATIBA: Baada ya kubainika wanatumia majina yanayofanana!
Uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete wa wajumbe 201 wa Bunge Maalumu la Katiba, umekumbwa na dosari baada ya wajumbe wawili wenye majina na ubini unaofanana, Amina Mweta, kutinga bungeni kila mmoja akidai kuwa mjumbe halali.
Habari
zilizopatikana jana mjini Dodoma zinasema wajumbe hao wanaotokea kundi
la wafanyakazi, wamelipwa posho za awali lakini walizuiwa kuendelea na
taratibu nyingine kusubiri hatima ya utata wa suala lao.
Habari
zilisema baada ya kuwasili bungeni, wajumbe hao walijisajili kwa
nyakati tofauti na kila mmoja kupewa vitambulisho.Mmoja alipata chenye
namba 602 na mwingine 1308.

Wajumbe
hao walikiri kulipwa posho ya kujikimu ya Sh80,000 kwa siku kwa muda wa
siku 13 unaomalizika Februari 28 mwaka huu ikiwa na maana kwamba kila
mmoja alilipwa Sh1,040,000.
Habari
zilidai kuwa Amina Mweta wa kwanza anatoka katika Chama cha Wafanyakazi
wa Serikali za Mitaa (TALGWU) na mwingine anatoka katika Chama cha
Wafanyakazi wa Mawasiliano na Usafirishaji (COTWU).
Mkanganyiko
huo ulitokana na kuwapo kwa sehemu nyingi za usajili wa wajumbe hao
kiasi kwamba watumishi wa Bunge walishindwa kubaini kuwapo kwa Amina
Mweta wawili kutoka kundi moja.
Mmoja wa kina mama hao anatokea wilayani Mwanga, Kilimanjaro na mwingine Songea, mkoani Ruvuma.
Mweta kutoka Mwanga alisema alipigiwa simu na Ofisi ya Bunge Maalumu la Katiba na kupongezwa kwa kuteuliwa na Rais kuwa mjumbe.
“Mimi ni
personal secretary (katibu muhtasi) wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mwanga na nilipigiwa simu na Ofisi ya Bunge wiki iliyopita
nikipongezwa kwa uteuzi huo,” alisema.
Alisema
alipofika na kujisajili baada ya kutoa kitambulisho chenye jina lake,
alipewa kitambulisho na kisha kupewa malipo yake ya posho. Mweta kutoka
Songea alisema alipigiwa simu na Katibu Mkuu wa COTWU kwamba ameteuliwa
na Rais kuwa mjumbe na kutakiwa kuripoti bungeni.
Kama
ilivyokuwa kwa mwenzake wa kutoka Mwanga, alisema naye alijisajili na
kulipwa posho ya siku 13 na jana alishangaa kukuta mjumbe mwingine
mwenye jina kama lake.
Alisema viongozi wa COTWU wamemwambia asubiri wakati wakitafuta usahihi wa nani hasa kati yao mwenye uhalali wa kuwapo bungeni.
Ofisi ya Rais yatoa msimamo
Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alipoulizwa kuhusu mkanganyiko huo,
alisema hajapata taarifa rasmi lakini watakapozipata watathibitisha nani
aliyeteuliwa na Rais kuwa mjumbe wa bunge hilo.
“Aliyeteuliwa
na Rais ni mtu mmoja na ndiyo maana huwa tunapenda watu watumie majina
matatu kwa sababu kwenye nchini kunaweza kuwa hata na watu 10 wote
wanatumia jina moja.
Tukipata
taarifa rasmi tutakachofanya ni kuthibitisha nani haswa aliyeteuliwa na
Rais ambaye ataendelea kuwa mjumbe na huyo mwingine basi itakuwa ni
bahati mbaya,” alisema Balozi Sefue.
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alipoulizwa kuhusu utata huo alisema mjumbe halali ni yule aliyetoka Songea.
Hata
hivyo, alisema kinachowashangaza ni kwama yule mwenzake wa Mwanga
alipotakiwa kurudisha fedha alizopewa kimakosa alisema ameshatumia
sehemu kubwa na kubakiza Sh50,000 tu.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment