Monday 10 March 2014

Foleni yazua maradhi mapya 


Dar es Salaam. Wakati kukiwa na ongezeko kubwa la ununuzi wa magari na kusababisha idadi kubwa ya vyombo hivyo vya usafiri, foleni za magari nchini, hasa jijini Dar es Salaam, imefikia hatua ya kutisha huku ikisababisha madhara makubwa kiuchumi, kijamii na kiafya, ikiwamo magonjwa ya akili.
Misululu ya magari ilikuwa ni ya kawaida kuonekana nyakati za asubuhi na jioni wakati watu wakielekea na kutoka kazini, lakini sasa foleni zimekuwa ni za kawaida katikati ya jiji na maeneo mengine ambayo ukarabati wa barabara unaendelea wakati wote.
Wakati kukiwa na kasi ndogo ya ukarabati wa miundombinu ya usafiri, kumekuwa na ongezeko kubwa la magari jijini Dar es Salaam. Pia kumekuwapo na ongezeko kubwa la idadi ya watu hadi kufikia milioni 4.3 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002 huku vyombo vya usafiri wa umma (daladala) vikitumia njia zisizo sahihi (kutanua), kufanya foleni kuwa kubwa hali inayosababisha jiji kuwa kero kwa muda wote.
Licha ya jitihada za Serikali kutumia treni kusafirisha abiria ili kusaidia kupunguza msongamano wa magari nyakati za asubuhi na jioni, bado tatizo hilo ni kubwa. Hivi karibuni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuri aliagiza Kampuni ya Strabag, inayojenga miundombinu ya mabasi yaendayo kasi, kufungua barabara zilizokamilika ili kupunguza msongamano.
Kutokana na tatizo hilo, wakazi wa Dar es Salaam na maeneo mengine yanayoathiriwa na foleni, wamekuwa wakilazimika ama kusitisha safari au kuchelewa kazini na kwenye shughuli nyingine, huku vyombo vya usafiri vikilazimisha kufanya safari chache na hivyo wamiliki kupata fedha kidogo kuliko matarajio yao.
“Madereva wanapata magonjwa ya akili kutokana na kero za barabarani,” alisema Dk. Innocent Godman, ambaye ni mmoja wa wataalamu wa nyanja tofauti aliyeongea na gazeti hili kuhusu tatizo hilo.
“Kwanza ni msongo wa mawazo kuhusu uchumi kutokana na mafuta mengi kupotea njiani; pili barabara mbovu; tatu hasira za kuchelewa anakokwenda; na nne wanakumbana na askari wa usalama barabarani ambao wanawakamua fedha,” alisema mtaalamu huyo wa magonjwa ya akili na mshauri nasaha kuhusu utumiaji wa madawa ya kulevya.
Tanzania inaelezwa ni nchi inayoongoza kwa kuwa na msongamano mkubwa wa magari katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Zatafuna mabilioni ya shilingi
Katika utafiti wake, Wakala wa Mradi wa Mabasi ya Kasi (DART), Jumbe Katala amebaini kuwa foleni husababisha ajali za barabarani, upotevu wa nishati (mafuta) na muda wa kukaa barabarani mambo ambayo husababisha hasara ya zaidi ya Sh655 bilioni kwa mwaka.
Katika utafiti huo, Katala alibaini kuwa foleni hizo husababisha kudorora kwa uchumi, huku bei ya mafuta ipanda kutokana na mahitaji ya nishati hiyo kuongezeka.
Alisema kuendesha na kuzima gari mara kwa mara kwa sababu ya foleni huongeza matumizi makubwa ya gari na kuongeza kasi ya uchakavu wake, hivyo kusababisha gharama kubwa za matengenezo ya mara kwa mara.

 

No comments:

Post a Comment