Monday 10 March 2014

Vurugu bungeni zawakera wasomi

Dar es Salaam. Vurugu na mivutano inayoendelea katika Bunge Maalumu la Katiba imewakera baadhi ya wasomi ambao kwa nyakati tofauti, wamesema kinachoendelea sasa ni matokeo ya mchakato mbovu wa namna ya kupata Katiba Mpya.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema kinachoendelea bungeni ni ugonjwa ulioanza tangu mchakato wa Katiba ulipoanza.
“Ugonjwa hauko bungeni bali mfumo mzima, watu wanakosea lakini tusiwalaumu ni sheria yenyewe haiku vizuri,” alisema Ally.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho alisema vurugu za bungeni zinatokana na kuwajumuisha wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wale wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, katika Bunge la Katiba.
“Wabunge wetu ndio chanzo cha vurugu, ndio utagundua wapi tulikosea,” alisema Profesa Shumbusho.
Godfrey Missana wa Dar es Salaam alisema kama wajumbe wa Bunge hilo wanabishana na kutofautiana katika hatua ya kutunga kanuni, hali inaweza kuwa mbaya zaidi wakati wa kuandaa Katiba Mpya.
Alex Charles mkazi wa jijini Mwanza alielezea wasiwasi kama kweli Katiba hiyo inaweza kupatikana Aprili 26 mwaka huu.

 

No comments:

Post a Comment