Monday 3 March 2014

G7 yailaani Urusi kuihusu Ukraine

  

Maandamano ya kuipinga Urusi, Ukraine.
Kundi la mataifa saba yaliyostawi zaidi kiviwanda almaarufu kama G7 limelaani vikali hatua za kijeshi zilizochukuliwa na Urusi nchini Ukraine-viongozi kundi hilo wakitaja hatua ya Urusi kama ukiukaji wa uhuru wa Ukraine.
Katika taarifa ya pamoja iliyotiwa pia saini na Umoja wa Ulaya EU-Urusi imetakiwa kushughulia wasiwasi wake kuihusu Ukraini kupitia mashauri au upatanishi.
Kundi hilo la mataifa saba tajiri zaidi duniani maarufu kama G-Seven limesema kuwa linachukuwa uamuzi wa kuahirisha matayarisho ya kongamano ambalo lingefanyika nchini Urusi mwezi juni mwaka huu kutokana na vitendo vya Moscow. Taarifa hiyo inakuja wakati vikosi vya Urusi vikiimarisha uthibiti katika rasi ya crimea ambapo Urusi inasema kuwa inalinda raia wake baada ya serikali kupinduliwa mjini Kiev.
Mbunge mashuhuri wa Urusi - Vyacheslav Nikonov, ameimabia BBC kwamba Urusi imejiandaa kwenda vitani kulinda maslahi yake nchini Ukraine na hususan katika mji wa Sevastopol.
"Ukraine ilialikwa kujiunga na Nato na hii ina maana kuwa marekani, au vituo vyake vya kijeshi vitawekwa nchini Ukraine. Urusi itafanya lolote, itahatarisha kuingia vita kuzuia hilo kutokea. Ni kuhusu kituo cha kijeshi, ni kuhusu mustakabal wa Urusi, mustakabal wa Ukraine. Sidhani kama mataifa ya magharibi yanaelewa kwamba Ukraine ni mahali ambapo Urusi ilizaliwa," amesema Nikonov.
Wanajeshi wasiotambuliwa washika doria katika kambi moja ya kijeshi nchini Ukraine.
Awali serikali ya mpito ya Ukraine iliishutumu Urusi kwa kutangaza vita na kuwaamuru wanajeshi wake kuwa tayari kwa makabiliano.Shirika la kujihami kwa mataifa ya Magharibi NATO limetowa wito kwa Urusi kuwaondoa wanajeshi wake nchini Ukrainena kuzitaka pande zote kusuluhisha mgogoro huo kwa njia ya amani. Taarifa hiyo imetolewa baada ya mkutano wa dharura wa mabalozi wa NATO mjini Brussels kujadili mgogoro huo. Katibu mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen, amesema kuwa huenda wachunguzi wa umoja wa mataifa wakatumwa kusaidia kusuluhisha hali ya mambo.
"Tunatoa wito kwa urusi kuheshimu ahadi zake za kimataifa, kuondoa vikosi vyake na kujiepusha na uvamizi katika maeneo mengine nchini Ukraine. Tunatowa wito kwa pande zote kufuata njia ya amani katika kusuluhisha mgogoro huo kupitia mazungumzo, kupitia wachunguzi wa kimataifa chini ya mwavuli wa umoja wa baraza la usalama la umoja wa mataifa au shirika la ushirikiano wa kiusalama ulaya OSCE,'' amesema bwana Rasmussen.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa marekani , John Kerry, anatarajiwa kuzuru Kiev hapo kesho jumanne kuiunga mkono serikali mpya ya Ukraine.
Haya yanajiri wakati mkuu wa jeshi la wanamaji wa Ukraine, Denis Berezovsky, akipokonywa madaraka yake baada ya kusema hadharani kwamba anaunga mkono serikali mpya ya Jimbo la Crimea ambayo inaunga mkono Urusi. Serikali ya Kiev imesema kuwa inamfanyia uchunguzi kwa nia ya kumfungulia mashtaka ya uhaini.

No comments:

Post a Comment